CCM WAMSHTAKI MASSAWE KWA JK
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemshtaki kwa Rais Jakaya Kikwete, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Fabian Massawe, kikidai kuwa ndiye chanzo cha mgogoro kati ya Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani na madiwani.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Massawe kujitumbukiza katika mgogoro huo, akidai anasuluhisha pande hizo mbili kwa kutumia viongozi wa dini na wazee maarufu, huku akitambua kwamba ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, iliyochunguza tuhuma za ufisadi haijatolewa.
Tanzania Daima Jumatano limedokezwa na kigogo mmoja wa makao makuu ya CCM, kwamba hatua hiyo ya Massawe imeleta shaka ya kwamba kuna jambo anataka lisijulikane katika ripoti ya CAG itakayokabidhiwa hivi karibuni.
“Huyu mkuu wa mkoa tumebaini ndiye chimbuko la matatizo yote ya Bukoba kwa namna anavyojaribu kumlinda mtuhumiwa. Yaani amefikia hatua ya kutaka kuonyesha umma kuwa mgogoro huo unasababishwa na imani za kidini.
“Chama kilikwishaamua kupitia Kamati Kuu, tukaomba serikali imwagize CAG afanye ukaguzi wa miradi ya kifisadi anayodaiwa kuitekeleza meya, sasa ripoti haijatolewa halafu yeye anaitisha vikao kuwababaisha madiwani,” alisema.
Kiongozi huyo ambaye alizungumza kwa sharti la kuhifadhiwa jina lake, alisema kuwa tayari wameagiza chama Mkoa wa Kagera kiwapatie muhtasari wa kikao hicho alichokifanya Massawe kwa ajili ya uamuzi zaidi.
“Huyu mtu ni tatizo na kwa jinsi inavyoonyesha, ripoti ya CAG imemkaanga meya, ndiyo maana Massawe anahaha kumnasua. Sisi tumeamua kumshtaki kwa rais ambaye ndiye mteuzi wake ili achukue hatua zaidi maana anavuruga chama,” kilisema chanzo hicho.
Juzi, Massawe aliitisha kikao na madiwani hao wanaompinga meya wakiwemo nane wa CCM na saba wa upinzani, mbele ya Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, Sheikh wa Wilaya ya Bukoba, Haruna Kichwabuta na wazee maarufu kwa kile alichodai ni kuwapatanisha na meya ili vikao vya baraza viweze kufanyika wapitishe bajeti ya mwaka 2014/15.
Kati ya madiwani hao 15, saba wa CHADEMA na CUF hawakuhudhuria kikao hicho wakidai kutokitambua huku sita wa CCM waliingia na kuondoka bila muafaka kupatikana.
Amani aliingia kwenye mgogoro na madiwani wake wanane wa CCM pamoja na mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki na wenzao saba wa CHADEMA na CUF wakitaka kumwondoa kutokana na tuhuma za kuendesha miradi ya kifisadi.
Baada ya mgogoro huo kuwa mkubwa na CCM ngazi ya taifa kushindwa kuumaliza, hatimaye Kamati Kuu ya chama hicho ilimwomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kupitia Wizara ya Tamisemi kufanya ukaguzi maalumu wa tuhuma hizo kupitia CAG.
Oktoba 10, mwaka jana, CAG alianza ukaguzi huo na tayari amekamilisha ripoti yake akisubiri kuikabidhi, lakini kumekuwa na juhudi za makusudi za kutaka kupotosha taarifa hiyo ili isiwasilishwe kwa madiwani.
Wakizungumza na gazeti hili kwa simu juzi kutoka mjini Bukoba, baadhi ya madiwani hao walieleza kushangazwa na kitendo hicho cha Massawe ilihali wanasubiri ripoti ya CAG.
“Sisi tumemuuliza mkuu wa mkoa, wakati mgogoro huo ukiendelea hadi leo ambapo vikao havifanyiki, hao viongozi wa dini na wazee walikuwa wapi kutafuta muafaka hadi wangoje CAG amalize ukaguzi na ripoti inakaribia kutolewa ndipo waje kutusuluhisha?
“Kwanza kama tungekubali huo mtego wao, wananchi wetu wangetushangaa na kamwe wasingetuelewa kuona kile tulichokipigania kinakaribia kutolewa hadharani kujua ukweli halafu tunageuka,” alisema mmoja wao.
Massawe inadaiwa kuwa alijaribu kuwasihi madiwani hao akidai kuwa ripoti ya CAG haipo, na kwamba kama itakuwepo huenda ikachelewa kwa muda wa miezi miwili, na hivyo kuwataka waingie kwenye vikao vya baraza kupitisha bajeti.
Kwamba baada ya suluhu hiyo kukwama, Massawe aliahidi kutumia mabavu ya kumwagiza mkurugenzi wa halmashauri aitishe kikao cha Baraza la Madiwani akitishia kuwa diwani ambaye hatahudhuria atachukuliwa hatua za kuwajibishwa.
Waliohudhuria kikao cha juzi kutoka CCM ni Alexander Ngalinda wa Kata ya Buhembe ambaye pia ni Naibu Meya, Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya, Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo), Richard Gaspar (Miembeni) na Murungi Kichwabuta wa Viti Maalumu.
Balozi Kagasheki na Dauda Kalumuna wa Kata ya Ijuganyondo hawakuweza kuhudhuria kikao hicho kutokana na kuwa katika majukumu yao mengine.
Miradi iliyokuwa inalalamikiwa ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Upo pia ujenzi wa soko ambapo meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani. Vile vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi wa kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.
TANZANIA DAIMA.