MAAZIMIO YA KIKAO CHA DHARURA CHA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) KUHUSU HATUA ZA KINIDHAMU DHIDI YA WANACHAMA ZITTO ZUBERI KABWE, DR. KITILA MKUMBO NA SAMSON MWIGAMBA
UTANGULIZI
Kamati Kuu ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ilikaa kikao cha dharura ili kupokea,
kujadili na kuamua juu ya utetezi wa mashtaka ya ukiukaji wa Katiba, Kanuni na
Mwongozo wa Chama yaliyokuwa yanawakabili aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Zitto
Zuberi Kabwe, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu Dr. Kitila Mkumbo na aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba. Kikao hicho cha dharura
kilifanyika Dar es Salaam kati ya tarehe 3-4 Januari, 2014. Kabla ya kuanza kwa
kikao, Kamati Kuu ilipokea taarifa kwamba Zitto Zuberi Kabwe amefungua mashtaka
dhidi ya CHADEMA katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam. Aidha,
Kamati Kuu ilijulishwa kwamba Mahakama Kuu imetoa amri ya zuio la muda ya
kuizuia Kamati Kuu au chombo kingine cha Chama kutokukaa, kujadili na kuamua
suala la uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe. Kutokana na amri hiyo ya Mahakama
Kuu, Kamati Kuu haikujadili na kuamua juu ya mashtaka dhidi yake.
MASHTAKA
Watuhumiwa wote
watatu walishtakiwa jumla ya mashtaka 11 yanayohusu ukiukaji wa vifungu mbali
mbali vya Katiba ya Chama, Kanuni za Uendeshaji Kazi za Chama, Kanuni za Kusimamia
Shughuli, Mwenendo na Maadili ya Wabunge wa Chama na Mwongozo wa Kutangaza
Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali. Mashtaka
yote yalitokana na watuhumiwa kuandaa kile kinachoitwa Mkakati wa Mabadiliko,
2013 kama ifuatavyo:
1. Kukashifu Viongozi Wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa
Chama Taifa Mh. Freeman A. Mbowe, na Katibu Mkuu Dr. Wilbrod P. Slaa;
2. Kutokuwa wakweli na wawazi kwa kushirikiana na vikundi
vya majungu kwa kuanzisha na kuratibu mtandao wa siri ulioitwa ‘Mtandao wa
Ushindi’ nje ya utaratibu wa Chama ili kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa
nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa;
3. Kutoa tuhuma za uongo dhidi ya viongozi wa Chama na bila
kupitia vikao halali vya Chama;
4. Kujihusisha na vikundi vyenye misingi ya ukabila, udini
na ukanda vyenye makusudi ya kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa jamii;
5. Kujihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha au
kuzua migogoro ndani ya uongozi wa Chama na wanachama wake;
6. Kuandaa na kutekeleza mpango wa kugombea nafasi ya
Mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la kufanya hivyo kwa mujibu wa
Mwongozo wa Chama;
7. Kutengeneza makundi na mitandao haramu ya kuwania
uongozi ndani ya Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
8. Kuwachafua viongozi na wanachama wenye nia au kusudio la
kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama kinyume cha Mwongozo wa Chama;
9. Kujihusisha na upinzani dhidi ya Chama na makundi ya
majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa uchaguzi wa Chama;
10.
Kukashifu Chama na
viongozi wa Chama nje ya Bunge kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge; na
11.
Kuchochea mgawanyiko
ndani ya Chama kinyume cha Kanuni za Maadili ya Wabunge.
UTETEZI WA
WATUHUMIWA
Watuhumiwa wote
walijitetea kwa maandishi. Zaidi ya utetezi huo wa maandishi, Dr. Kitila Mkumbo
na Samson Mwigamba waliitikia wito wa Kamati Kuu wa kujitetea kwa mdomo mbele
yake. Hata hivyo, siku ya utetezi wao, ni Dr. Kitila Mkumbo peke yake aliyejitokeza
kwenye Kamati Kuu na kujitetea kwa mdomo. Katika utetezi wake wa maandishi,
licha ya kukiri kushiriki katika maandalizi ya kile kinachoitwa Mkakati wa
Mabadiliko 2013, Dr. Kitila Mkumbo – kama ilivyokuwa kwa Samson Mwigamba –
alikanusha na kukataa tuhuma zote za kukiuka Katiba ya Chama, Kanuni zake na
Mwongozo wa Chama. Kwa maneno yake mwenyewe, Dr. Mkumbo alikanusha “kila tuhuma
mojamoja na kwa ujumla wake dhidi ya[ke]”, na kwamba mashtaka hayo sio ya kweli
na hakuvunja Katiba, Kanuni wala Mwongozo wa Chama.
Aidha, licha ya
kukiri kwake katika kikao cha Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana kwamba
walioshiriki kuandaa Mkakati huo ni pamoja na mtu anayejulikana kama M2, mara
hii Dr. Kitila Mkumbo aliiambia Kamati Kuu kwamba “waraka husika ulikuwa ni wa
siri na haukuwahi kusambazwa wala kushirikisha … wanachama au viongozi wa
CHADEMA isipokuwa mimi binafsi na Samson Mwigamba….” Vile vile, ijapokuwa
katika Kamati Kuu ya Novemba mwaka jana Dr. Mkumbo alidai kutokumfahamu kabisa
M2, mara hii aliiambia Kamati Kuu kwamba anamfahamu fika M2 lakini hayuko
tayari kumtaja mbele ya Kamati Kuu hadi atakapowasiliana naye!
USHIRIKI WA ZITTO
ZUBERI KABWE KATIKA MKAKATI WA MABADILIKO
Itakumbukwa kwamba
katika kikao cha Novemba 2013, Dr. Kitila Mkumbo na Zitto Zuberi Kabwe walikataa
kata kata kuhusika kwa Zitto Zuberi Kabwe katika maandalizi ya Mkakati wa Mabadiliko.
Aidha, Zitto Zuberi Kabwe alidai mbele ya Kamati Kuu kwamba alikuwa ameusikia
Mkakati huo kwa mara ya kwanza kwenye Kamati Kuu, na amerudia kauli hiyo mara
nyingi na hadharani tangu avuliwe nafasi zake za uongozi. Hata hivyo, wakati wa
mahojiano na wajumbe wa Kamati Kuu, Dr. Kitila Mkumbo alikiri kwamba yeye na
waandishi wenzake wa Mkakati walimpa Zitto Zuberi Kabwe briefing juu ya Mkakati
na kwamba alikuwa anaufahamu. Ukweli huu pia umethibitishwa na mawasiliano ya
baruapepe iliyotumwa na Zitto Zuberi Kabwe mwenyewe kwa mtu anayeitwa ‘CHADEMA
Mpya 2014’ tarehe 27 Oktoba, 2013, karibu mwezi mmoja kabla ya kikao cha Kamati
Kuu ya Novemba iliyowavua madaraka.
Zaidi ya hayo, baada
ya kuonyeshwa waraka wa Chama juu ya mabadiliko ya Katiba ya Chama uliotumwa na
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama wakati huo Shaibu Akwilombe Julai 2006
unaothibitisha kwamba mabadiliko ya Katiba yaliyoondoa ukomo wa uongozi
yalifanywa kwa uwazi na kwa kushirikisha ngazi zote za Chama, Dr. Kitila Mkumbo
alikataa kata kata kujadili suala hilo kwa madai kwamba tayari walishapeleka malalamiko
yao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Kuhusu tuhuma zao
kwamba kuna ufisadi na ubadhirifu wa fedha za Chama unaofanywa na Mwenyekiti wa
Chama, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Fedha Anthony Komu na kwamba taarifa za
matumizi ya fedha ni siri ya viongozi hao watatu, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa
mbali mbali za fedha zilizowasilishwa mbele ya vikao vya Kamati Kuu a Chama
ambavyo yeye mwenyewe na Zitto Zuberi Kabwe walishiriki kama wajumbe wa Kamati
Kuu. Aidha, Dr. Mkumbo alionyeshwa taarifa za kibenki zinazoonyesha jinsi
michango ya Mzee Jaffer Sabodo na michango mingine ya watu binafsi
zilivyopokelewa na kutumiwa na taarifa zake kuwasilishwa kwenye vikao vya
Kamati Kuu walivyohudhuria yeye na Zitto Zuberi Kabwe.
Zaidi ya hayo, Dr.
Mkumbo alionyeshwa nyaraka za manunuzi ya vifaa vya Chama kama vile vile
pikipiki, kadi, bendera, n.k, na jinsi ambavyo uamuzi wa manunuzi hayo
yalifanywa na Kamati Kuu ambayo wao wenyewe ni wajumbe na walihudhuria vikao
husika. Vile vile, Dr. Mkumbo alionyeshwa ushahidi wa maandishi kwamba
Mwenyekiti wa Chama hakuhusika kwa namna yoyote ile katika manunuzi hayo na
hakuna karatasi yoyote inayoonyesha saini ya Mwenyekiti katika manunuzi ya
vifaa hivyo. Aidha, Dr. Mkumbo hakuweza kuthibitisha kwa namna yoyote kwamba
CHADEMA ina mkataba wowote na watu binafsi wanaouza vifaa vya uenezi vya Chama
kwa vile Kamati Kuu ya Chama katika vikao ambavyo vilihudhuriwa na Dr. Mkumbo
na Zitto Zuberi Kabwe ilikwisharuhusu wafanya biashara binafsi kuagiza vifaa
hivyo na kuviuza kwa wanachama wanaotaka kuvinunua. Kwenye yote haya, Dr.
Kitila Mkumbo hakuwa na lolote la maana la kuiambia Kamati Kuu.
MAAMUZI YA KAMATI
KUU
Baada ya kusikiliza
utetezi wa Dr. Kitila Mkumbo na baada ya kumhoji kwa kirefu, Kamati Kuu
imeridhika bila mashaka yoyote kwamba Mkakati wa Mabadiliko 2013 haukuwa na
lengo la kumwezesha Zitto Zuberi Kabwe kutwaa nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa
Chama peke yake. Mkakati huo ulikuwa na malengo makubwa zaidi ya kukibomoa
Chama kwa kukichafua kwa wananchi na kuwachafua viongozi wake wa juu kwa
kutumia tuhuma za uongo za ufisadi. Hii ni kwa sababu, kwa maoni ya Kamati Kuu,
Chama cha siasa ambacho viongozi wake wa juu wanatuhumiwa kwa ufisadi hakiwezi
kuaminiwa na wananchi kama tumaini lao la ukombozi.
Kamati Kuu
imeridhika kwa ushahidi wa nyaraka mbali mbali zilizoandaliwa na Zitto Zuberi
Kabwe mwenyewe ama na mawakala wake wakitumia vitambulisho bandia katika
mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwamba mkakati wa kukibomoa Chama
umeandaliwa na kutekelezwa kwa muda mrefu. Mkakati huo ulihusisha pia hujuma
dhidi ya Chama kwa kuwaengua wagombea wake katika chaguzi mbali mbali kama
ilivyotokea katika majimbo ya Mpanda Mashariki, Musoma Vijijini na Singida
Mjini ambapo Zitto Zuberi Kabwe alishiriki moja kwa moja.
Kwa sababu zote
hizo, Kamati Kuu imeazimia ifuatavyo:
1.
Kwamba
kuanzia tarehe ya uamuzi wake, Dr. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba wafukuzwe
uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA); na
2.
Kwamba,
kwa vile Zitto Zuberi Kabwe amekishtaki Chama kinyume na matakwa ya Katiba ya
Chama na Kanuni zake, na kwa vile Mahakama Kuu imeamuru vikao vyote vya Chama
visijadili wala kuamua suala lolote linalohusu uanachama wa Zitto Zuberi Kabwe,
viongozi wa ngazi zote za Chama, wanachama, washabiki na wapenzi wa CHADEMA popote
walipo katika nchi yetu na nje ya Tanzania wasishiriki wala kusaidia kwa namna
yoyote mikutano yoyote ya nje au ya ndani au shughuli nyingine yoyote ya
kisiasa itakayofanywa na Zitto Zuberi Kabwe na mawakala wake kwa jina la
CHADEMA.
--------------------------------
Dr. Wilbrod P. Slaa
KATIBU MKUU