Bukobawadau

KAMATI YA MAADILI CCM YATAKIWA KUWASHUGHULIKIA WALIOTANGAZA NIA


Dar es Salaam. Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umeshauri Kamati ya Maadili ya CCM kuwaonyesha mlango wa kutokea wote walioanza kampeni za kugombea urais, ubunge na nyingine kinyume cha maadili ya chama.
Umesema wagombea hao ambao umewaita wasio rasmi, wameonywa mara kadhaa na viongozi wa chama ikiwamo kupitia kwenye vyombo vya habari, lakini wameshindwa kujitambua na kujirekebisha.
UVCCM umedai wagombea hao wasio rasmi katika kampeni zao tayari wameanza kusababisha kutoweka kwa mshikamano ndani ya chama, kwani wamekuwa wakipita nchi nzima kushawishi kwa fedha na rushwa nyingine mbalimbali makundi ya jamii ili kuungwa mkono.
Mkuu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi Taifa, Paul Makonda alisema Kamati ya Maadili ya CCM ina wajibu wa kutafsiri hasira ya wanaCCM dhidi ya kampeni hizo ambazo zinakijeli chama, uongozi wa nchi uliopo na kuleta nyufa.
“Tunachokiona sasa ni tofauti kabisa na malezi na makuzi yetu ndani ya chama, kwani tayari baadhi ya wanaCCM bila uoga wala aibu wameshajitangaza ni wagombea urais, ubunge, udiwani na nafasi nyingine za kupigiwa kura, wameanza kampeni za kishindo za rushwa na vishawishi mbalimbali nje kabisa ya utaratibu, kanuni na maadili ya chama,” alisema Makonda na kuongeza:
“Watu hawa waonyeshwe mlango wa kutokea, tusipoziba ufa huu sasa tujiandae kujenga ukuta mwakani kwa gharama kubwa kupindukia.”
Makonda alisema kwa sababu mwaka huu kuna mchakato wa chaguzi mbalimbali zitakazohitimishwa mwakani na ushaguzi mkuu, mshikimamo wa hali ya juu unahitajika ndani ya chama.
“Kwa sasa ilani ya CCM ya mwaka 2010 imewekwa pembeni, kinachonadiwa ni ilani binafsi za kumwaga fedha nchi nzima, kusambaza elimu kama njugu, bila kueleza vyanzo vya mapato ya Serikali zao za kusadikika,” alisema. Alisema hatua hiyo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za chini, maadili, miiko ya chama.
pamoja na Serikali kwa ujumla ambapo ipo wima katika kuhakikisha kuwa ilani ya CCM ya mwaka 2010 inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Alisema CCM inataratibu zake za kupata viongozi na wote tunazijua, kufanya kinyume na taratibu hizi ni uasi, upungufu wa busara, na ukosefu wa sifa ya uongozi.
“ Hivyo vijana wa CCM tunamuunga mkono Mwenyekiti wa CCM taifa Dk Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti, Philiph Mangula na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama Nape Nnauye waliokemea tabia hii mpya hatarishi kwa chama chetu ya kuhaha kupata uongozi nje ya taratibu na kutumia vishawishi vyenye sura ya rushwa vitakavyokitia doa chama,”
Makonda alisema kuwa maadili na kanuni za chama ni kuwaunganisha wanaCCM wote kuwa kitu kimoja, hivyo dalili zozote nje ya tunu hizo ni usaliti, uasi ambao hauna budi kupigwa vita kwa nguvu zote kwa vijana.
“ Hapa hatutakiwi kumwangalia nyani usoni, gharama ya kuendelea kuvumilia kauli na vitendo hivi vipya na hatarishi katika historia ya chama chetu ni majuto kwa kuwa waswahili hunena bandu bandu humaliza gogo, na bandu bandu hii iliyoanza tusiivumilie, itatuweka pabaya wanaCCM, “ alisema Makonda.
chanzo;mwananchi
Next Post Previous Post
Bukobawadau