Bukobawadau

MAHAKAMA YAMWACHIA HURU LIYUMBA

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwachia huru Mkurugenzi wa zamani wa Utawala na Utumishi (DPA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba kutokana na upelelezi uliofanywa kuwa mbovu na wakili aliyekuwa akiiendesha kesi hiyo kuwa mzembe.
Liyumba alikuwa akikabiliwa na kesi ya kukutwa na simu akiwa gerezani Ukonga, Dar es Salaam, wakati akitumikia kifungo cha miaka miwili, kilichotokana na kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya ofisi ya Umma.
Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando alisema mahakama inamwachia huru Liyumba kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka lililokuwa likimkabili pasipo kuacha shaka.
Alisema wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, shahidi wa upande wa mashtaka ambaye ni Ofisa Magereza, Patrick alidai kuwa simu aina ya Nokia 1280 ilikutwa mikononi mwa Liyumba wakati akiwa gerezani, huku Liyumba akidai kwenye utetezi wake kuwa siku hiyo alikwenda nayo Patrick na kujifanya alimkuta nayo.
‘Wakati huo tulitegemea angeileta simu, lakini alitoa mkebe wa kuhifadhia miwani na kuutenda kuwa kielelezo cha ushahidi na badala ya simu. Akaitoa kama utambulisho tu, wakati shahidi mhusika Patrick alikuwapo mahakamani na kutambua vielelezo vyote alivyodaiwa kukutwa navyo Liyumba siku ya tukio.
Alisema hata huo utambulisho wa simu uliochukuliwa na mahakama, ulichukuliwa kimakosa kwa sababu aliyepaswa kuomba kufanya hivyo alipaswa kuwa shahidi na siyo Wakili wa Serikali kama alivyofanya Kaganda.
Kwa upande wa mchunguzi wa kesi hiyo, Hakimu Mmbando alisema alipaswa kubainisha ile laini ya simu yenye namba 0653 004662 ilikuwa ni ya nani kati ya mshtakiwa na shahidi kwa sababu kulikuwa na utata.
“Kuna uwezekano ni kuwa ni kweli Liyumba alikutwa na simu gerezani, lakini kutokana na upelelezi mbovu wa kufuatilia namba iliyotumiwa ilikuwa ni ya nani, mazingira ya kuingizwa gerezani inaonesha wazi kuwa mchunguzi alikuwa mzembe na uchunguzi mbovu.” Alisema Hakimu Mmbando.
Next Post Previous Post
Bukobawadau