Bukobawadau

TASWIRA MHADHARA ALIOTOA SHEIKH NURDIN KISHIK JIONI YA LEO MJINI HAPA JAN 9,2014

Sheikh Nurdin Kishik akitoa mawaidha kwa waumini wa Kiislamuwaliojitokeza kumsikiliza katika Mhadhara uliofanyika leo katika viwanja vya Shule ya Kiislam ya Jamia iliyopo Kata ya Bilele katikati ya Mji wa Bukoba
 Sheikh wa Mkoa wa Kagera, Sheikh Haruna Kichwabuta akitoa neno na kumkaribisha Mgeni wa leo Sheikh Nurdin Kishik.
Mambo mengi juu ya Uislam ameyaongelea,Hapa Bukobawadau Blog tunafanya  kunukuu baadhi ya maneno yaliotokana na mhadhara huu kwa siku ya leo“Leo nimekukamilishieni dini yenu, na kukutimizieni neema zangu juu yenu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndio dini yenu”(TMQ 5:3)
Katika aya hii na nyenginezo, Allah (SWT) anatukumbusha sisi umma wa Kiislamu thamani na umuhimu wa ujumbe wa Kiiislamu. Ujumbe huu ambao ni tofauti na risala zinginezo kwa namna nyingi.
Ni ujumbe wa mwisho kwa wanaadamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu (Allah). Wafuasi wa ujumbe huu wana wajibu wa kuubeba, kuutawalisha, na kuufikisha kwa mataifa mengine hata bila la ya kuwepo kwa Mtume Muhammad (SAAW). Hali ambayo ni kinyume na zama za Mitume mingine iliyowaongoza umma zao kabla ya Mtume Muhammad (SAAW).
 Sheikh Haruna Kichwabuta na Sheikh mkuu wa Wilaya ya Muleba wakimsikiliza kwa Umakini Sheikh Khishki
Umma wa Waislamu wakimsikiliza Sheikh Kishki katika Mhadhara uliofanyika jioni ya leo.
Ujio wa ujumbe huu unatokana na ahadi ya Mwenyezi Mungu, na zaidi umma wa Kiislamu utakuwa ni umma wa mwanzo kuingia peponi. Kwa hivyo, walioikubali dini hii na kuubeba ujumbe huu, kwa hakika wamepata bahati kubwa mno isiyo na mfano.
Katika tareekh, umma wa kiislamu uliufahamu utukufu wa risala ya Kiislamu kwa kuutekeleza na kuulinda.Waislamu walishikamana na kuulinda ujumbe wa Kiislamu hata katika hali ngumu ya kutawaliwa na kuporwa ardhi yao chini ya utawala wa kikatili na kishenzi wa Wamongolia (Mongols). Kwa udhati, katika kipindi hiki cha Waislamu kuporwa ardhi yao walidiriki kuwaathiri wavamizi hao kwa kwa mfumo wa Kiislamu. Na Kwa hakika ni kitu cha kushangaza mno kwamba watawala hao waporaji wa ardhi ya Waislamu waliathiriwa na kubeba Uislamu uliokuwa ni risala ya wataliwa. Si tu waliubebaUislamu bali waliulingania kwa nguvu zote. Jambo hili linathibitisha ufahamu wa hali ya juu waliokuwa nao Waislamu.
Leo kwa masikitiko na huzuni kubwa tunashuhudia baadhi ya Waislamu kupuuza ujumbe wa Kiislamu au kufuata baadhi ya vitu kutoka ujumbe huu. Baadhi wanajaribu kuchanganya fikra na tamaduni zilizo kinyume kabisa na itikadi ya dini hii. Leo wakati mwingi baadhi ya sheria za Uislamu zinatekelezwa pamoja na zile zilizo nje ya Uislamu. Wengi miongoni mwa Waislamu wanafahamu Uislamu katika upande wa mambo ya kiroho na ibada binafsi tu, na wamekuwa wakiufikisha na kuuwasilisha Uislamu kwa wengine kama ni hivyo tu, na sio mfumo kamili wa kimaisha.
Mbali ya yote hayo, mfumo wa Uislamu bado upo hai na haujabadilika ndani ya Qur’an na Sunnah. Ni kutoka na vyanzo viwili hivi ndipo Uislamu unaweza kufafanulika na kufahamika uasili wake, kwa kupitia nguzo zake muhimu za misingi ya sheria za Kiislamu (Usul al- Fiqh).
Uislamu haukuteremshwa wote kwa wakati mmoja, na pia sio mkusanyiko wa baadhi ya sheria kama zilivyo nyaraka nyengine za kisheria. Bali ni mfumo unaotoa ufumbuzi za matatizo ya kila siku yanayomkabili mwanaadamu leo kama yalivyokuwa yakimkabili Mtume SAAW na masahaba zake.
 Uislamu umefananua na kuweka wazi muongozo kwa Mtume (SAAW) na wafuasi wake kuhusiana na vipi kuishi maisha Kiislamu. Aidha, Uislamu si tu umefafanua muongozo wake na fikra zake, bali pia umetupatia sheria zote kwa ukamilifu zanazohusiana na maisha ya binaadamu na yote yanayomkabili. Kutawalishwa kwa sheria hizi na fikra zake katika jamii kulileta utulivu, amani, haki na uadilifu kwa jamii nzima.
 Sehemu ya viongozi wa dini  mjini hapa
 Itikadi (aqeeda) ya Uislamu ni tofauti kabisa na itiqadi/ aqeeda ya kibepari au tuseme mfumo wa demokrasia kwa hali zote. Uislamu umemkomboa mwanaadamu kutokana na utumwa na hisia za binaadamu mwenzake, na kumfanya kuwa mtumwa wa kweli wa Muumba wake Allah (SWT). Itikadi (aqeeda) ya Uislamu humtaka mtu kufikiri na kutafuta radhi za Mola wake kuwa ndio lengo lake kuu. Na sio kuwa na lengo kuu la kutafuta maslahi binafsi na starehe fupi za kilimwengu.
 Sheria za Kiislamu kama ilivyo itikadi (aqeeda) yake, zote zimeteremshwa na Allah (SWT). Sheria hizi hazimpendelei yeyote katika jamii awe masikini au tajiri, muajiri au muajiriwa, mtawala au mtawaliwa nk. Kwani deleo hutokana zaidi na mapungufu ya sheria zilizopangwa na binaadamu, kwa kufuata matamanio na hisia za nafsi zao. Hivyo hakuna Muislamu mwenye ufahamu sahihi wa dini yake atakayejutia au kusita sita kuzitawalisha sheria tukufu za Kiislamu. Hata hivyo, bado kuna baadhi ya Waislamu wana uzito katika nyoyo zao kuzitawalisha sheria hizo, na miongoni mwa sababu kubwa ni kukosa wa ufahamu wa kina wa fikra zinazohusiana na misingi ya sheria za kiislamu (usul fiqhi)
'Mwisho wa kunukuu.'
 Vyombo mbalimbali vilikuwepo katika kuchukua tukio hili
 Sheikh Kishik akitoa utambulisho.
Sheikh Nurdin Kishik akitoa shukrani kwa uongozi wa Bakwata pia uongozi wa Qudus
Sehemu ya waumini katika hali ya usikivu.
Katibu wa ( A.M.Y.C) akitoa shukrani kufuatia  ugeni huu.
Sheikh Nurdin Kishki katika na Sheikh wa Mkoa wa Kagera Sheikh Haruna Kichwabuta
 Mhadhara ukiendelea
 Sehemu ya wanawake katika mhadhara huo.
 Hivi ndivyo hali ilivyokuwa jioni ya leo katika viwanja vya Jamia Mjini hapa
Sheikh Nurdin Kishki akisalimiana na waumini wa Kiislam.
 Ndivyo ilivyo hali ya madaraja kwa viongozi,hapa kila muumini anataka kusalimiana na sheikh Nurdin Kishik.
 Mwisho wa mhadhara huu hali ilikuwa hivi.
 Sheikh Kishik akiingia kwenye gari.
 Waumini wakimpungia mkono wa kwaheri Sheikh Kishik
 Anaonekana Sheikh Nurdin Kishik akiwapungia mkono waumini waliojitokeza kumsikiliza.
Mwisho wa matukio juu ya Mhadhara wa Sheikh Kishki Mjini hapa Jan 9,2014

Next Post Previous Post
Bukobawadau