Bukobawadau

HUU NI UBAGUZI WA RANGI UNAONUKA KULIKO WA MAKABURU

Na Prudence Karugendo

Pengine swali moja lilisahaulika wakati jengo la ghorofa kumi lilipoporomoka hivi karibuni katikati ya jiji la Dar es salaam. Tunaweza kujiuliza ni kwanini waliofukiwa na vifusi vya jengo hilo na badhi yao kukutwa na mauti walikuwa watu weusi peke yao.

Nyumba iliyofukiwa na vifusi vya jengo lililoporomoka ilikuwa ikikaliwa na familia ya Watanzania wenye asili ya Kiasia, Wahindi, na ikasemwa wazi kwamba kabla ya jengo kuporomoka lilishaonyesha dalili zote kiasi cha kuwafanya wakazi wa nyumba za jirani kuchukua tahadhari kwa kuzihama nyumba zao. Basi kwanini wafanyakazi wa ndani wa nyumba hizo walisalia mpaka kukutwa na ajali?

Kwa bahati hata picha zilipigwa zikionyesha baadhi ya raia wenye asili ya kiasia wakiondoka katika nyumba hizo kabla ya ajali huku wakiwa na mabegi yao mikononi. Kwa vyovyote kila mmoja alishajua hatari iliyokuwa njiani kutokea. Ni vyema sasa tukajua wale waliosalia ambao wote inasemekana walikuwa watumishi wa ndani walisalia si kwa hiari yao bali walilazimishwa kubaki kulinda nyumba bila kujali usalama wao utakuwaje.

Hilo linaweza kuonekana ni wazo lililochelewa kuzitokeza au lenye dhamira ya uchochezi, lakini kwa minajili ya kutambua haki za wale waliofukiwa na vifusi vile na kupata vilema au kupoteza maisha, ni lazima wazo hilo lijitokeze ili kama sio kwa ajili ya kutafutia stahili za kisheria za kila upande basi angalau kuweka kumbukumbu sawa kwa ajili ya siku zijazo. Kwanini waswahili wale walibakishwa kwenye nyumba iliyokuwa katika hatari ya kufukiwa na jengo lililokuwa limeishaonyesha dalili zote za kuporomoka?

Baada ya jengo hilo kuporomoka watu kadhaa walishikiliwa na polisi akiwemo mhandisi wa manispaa ya Ilala, mmiliki wa jengo husika pamoja na mkandarasi wake. Kwa vyovyote hawa ni wale ambao walihusika na uzembe au ubadhilifu katika mwenendo wa ujenzi uliopelekea jengo hilo kukosa uimara na kuporomoka. Hayo tuyaweke pembeni, maana yalikuwa ni masuala ya kisheria.

Katika mkasa huo ni lazima wapo watakaofidiwa. Kwa vyovyote hao watakuwa wale wenye nyumba zilizoporomokewa. Ndio maana swali la msingi juu ya wale walioathirika kwa kufukiwa na vifusi linaibuka. Sio tu juu ya watafidiwa vipi kutokana na janga lililowakuta, lakini hata mazingira ya kufukiwa kwao. Ni kweli waliridhia kubaki katika nyumba iliyokuwa katika kitisho cha kuporomokewa kutokana na ubishi wao au walilaghaiwa na kulazimishwa kubaki ili kulinda mali za waajiri wao.

Nina hakika wale walionusurika wanaweza kusema kitu kama watahojiwa kwa umakini. Ni kitu gani hasa kiliwapa ujasiri wa kubaki katika jengo lile huku wakiwaona wenzao ambao ni waajiri wao wakiondoka. Wao waliamua au walikubali kubaki ili wafanye nini na ni tumaini gani walilokuwa nalo au walilopewa juu ya usalama wao? Nini kilichowafanya waamini kwamba kitisho kile kilichokimbiwa na waajiri wao wenyewe kisingewakuta? Kama ilikuwepo ahadi yoyote waliopatiwa waseme kama imeshatimizwa na kama bado itatimizwa lini na nani?

Nashawishika kujiuliza maswali yote haya kwa vile siamini kama inawezekana kwa mtu mwenye akili timamu aridhie kubaki katika sehemu yenye hatari iliyo wazi kama ilivyokuwa katika jengo lile lililoporomoka. Hata hivyo kwa vile imetokea na imethibitika kwamba watu wale hawakuwa wendawazimu basi ninayo kila sababu ya kutia shaka kwamba palikuwepo ulazimishwaji au hata ubembelezwaji wa kubaki ndani ya jengo lile ambao pengine ulikubalika kutokana na woga wa kupoteza kazi.

Wakati tukiendelea kutafakari hayo, kikarushwa kipindi cha Power Breakfast cha kila asubuhi katika redio ya Cloud FM, tulisikia habari ya dada yetu wa Kitanzania, Eliza Kawugo, aliyehadaiwa na kupelekwa kufanya kazi za kitumwa nchini Uingereza na mama wa Kihindi aliyeitwa Mrs Alibhai. Ni kwa msaada wa akina mama wa Kitanzania pamoja na ubalozi wetu, huko ndio binti yule alikoweza kusaidiwa na kufunguliwa kesi mahakamani ambayo ilimalizika kwa kutakiwa alipwe fidia ya kiasi cha takribani paundi 59,000 za Kingereza.

Unaweza kujiuliza ni wangapi wanaoweza kuwa katika utumwa kama huo ambao habari zao hazijajulikana na hawana jinsi yoyote ya kujinasua. Na kwa bahati mbaya hao hawako tu nje ya nchi lakini hata humu humu ndani. Kwa bahati siku ileile tuliyosikia habari ya Uingereza magazeti na redio za hapa nchini zilitangaza habari za dada aliyekufa kutokana na kulazimishwa kufanya kazi huku akiwa mgonjwa nyumbani kwa mwajiri wake wa Kiasia.

Pengine wote tunao uzoefu wa mahusiano yanayokuwepo mara nyingi baina ya wafanyakazi na waajiri wenye asili ya Kiasia katika mahala pa kazi. Hasa kazi zenyewe zinapokuwa za nyumbani ambazo sulubu zake ni vigumu kuonekana na jamii. Mara nyingi thamani ya utu inawekwa chini mno kiasi ni shida tu zinazowafanya ndugu zetu wakubali kuendelea na kazi hizo.

Leo nitaongelea vitendo vya unyanyasaji na ubaguzi wa rangi vilivyokithiri kwa wafanyakazi weusi mbele ya waajiri wa Kiasia. Wengi tumeshafanya kazi katika makampuni yanayomilikiwa na wenzetu hawa hususani jamii ya Kihindi. Hata kama siyo hizo kazi za ndani lakini hata zile za maofisini na viwandani mambo hayana tofauti sana. Utu wa mtu mweusi unawekwa chini mno, na mara nyingi rangi ya mtu ndio inakuwa kigezo kikuu cha viwango vya mishahara, vyeo na hata vipaumbele vya usalama kazini.

Binafsi nimeishashuhudia sehemu nyingi ambapo ajira haina tofauti kabisa na utumwa. Watu wanatukanwa, wananyanyaswa, mahala pengine wanapekuliwa bila staha za kijinsia, mishahara duni na mwisho wa yote kufukuzwa kazi wakati wowote mwajiri anapojisikia.

Yote hayo yakifanyika katika misingi ya wazi kabisa ya ubaguzi wa rangi. Kwa kawaida ukimwona Mhindi ujue ni bosi na Mswahili ni mtu wa chini hata kama awe na umri, elimu, au uzoefu kiasi gani.

Kwa bahati mbaya viongozi wetu wa serikali na vyombo vya dola ndio wamekuwa kinga kuu ya unyanyasaji na ubaguzi huu. Kila siku wafanyakazi wanatishwa kwa picha za ukutani ambazo wabaguzi hawa wanapiga pamoja na viongozi katika hafla mbalimbali. Na kama hawataamini picha hizo basi watashuhudia kwa macho yao viongozi hao wakipishana kuingia ofisini kwa bosi kuomba misaada na kuchukuwa milungula. Mara moja mfanyakazi anagundua kwamba hana jinsi ya kutetea haki yake kwa vile sehemu zote anazotegemea kupeleka kilio chake ni maswahiba wa mwajiri wake.

Itakuwa ni kichekesho kikubwa kwa serikali yetu kusema haitambui haya kwa vile hata kamati ya bunge ilishawahi kutembelea makampuni fulani katika miaka ya mwanzo ya 2000 na kuthibitisha unyanyasaji na ubaguzi wa rangi unaofanyika katika makapuni hayo. Sikumbuki hatua yoyote iliyochukuliwa zaidi ya kuombwa wajirekebishe. Basi kamati ile ipite tena ghafla leo katika makampuni yaleyale ione kama kuna marekebisho yoyote yaliyofanyika au mambo ndio kwanza yamezidi kuharibika.

Najipa ujasiri wa kuandika maneno haya japo najua kwamba ni tiketi nzuri ya kuitwa kaburu. Na wala watakaoniita kaburu sio waasia. Ni Waswahili walewale ambao ndugu zao wananyanyaswa na kubaguliwa katika ajira za Waasia. Ni wale wanaorambishwa asali kwa mgongo wa chupa kwa kupewa vyeo bandia huku wakishuhudia wazi kwamba hawana mamlaka kamili ya vyeo hivyo. Ni wale viongozi na wanasiasa wetu ambao kila sekunde utawaona wakipishana kuombaomba katika ofisi za Wahindi.

Utawasikia wakimnukuu Mwalimu, Baba wa Taifa, kwamba mbaguzi yeyote ni kaburu. Lakini cha kushangaza ni kwamba ukaburu huu huwahusu Waswahili peke yao ambao kwa kawaida huishia kusema tu. Na mara nyingi wakihoji jinsi wasivyotendewa haki katika mahusiano ya kijamii na migawanyo ya rasilimali. Lakini kwa wenzetu wenye asili ya Kiasia ambao hutenda ubaguzi wao waziwazi kamwe hawaitwi makaburu!

Nimalizie kwa kusema kwamba simchukii Mhindi wala mtu mwingine yeyote. Na kwa bahati wengi ni marafiki zangu. Lakini nina imani urafiki huu utakuwa mzuri zaidi kama nao watawaona Waswahili kuwa ni watu wenye thamani kama yao. Hatulingani kwa mambo mengine kama elimu, fedha, uzoefu na kadhalika, lakini kwa kwa rangi zetu ingetakiwa tuwe sawa.

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau