Bukobawadau

MARUK VANILLA Wafurahia Msimu wa Mavuno ya Pilipilimanga Mkoani Tanga

Muonekano wa Pilipilimanga baada ya kuvunwa.
Pilipilimanga ikikaushwa juani.
Pilipilimanga ikiwa tayari kufungwa na kusafirishwa.
Uvunaji wa Pilipilimanga ukiendelea.


Maruk Vanilla, kampuni ya wakulima wa Kagera wenye malengo yanayoshabihiana katika kukuza mazao mbadala ya kibiashara mwaka huu imeshiriki msimu wa mavuno na ununuzi wa pilipilimanga Mkoani Tanga.

Maruk Vanilla ambayo kwa Kagera inajihusisha zaidi na ukulima pamoja na ununuzi wa mapodo ya vanilla imedhamilia kwa dhati kuhakikisha Kagera pia inakuwa mzalishaji mkubwa wa pilipilimanga. Akitetea dhamira hii Mkurugenzi Mtendaji wa Maruk Vanilla Bwana Murshid Hassan alisema “hali ya hewa ya Tanga inafanana na ya Kagera. Vilevile mazao yanayoshamili kwenye ardhi ya Kagera yanastawi vema pia Tanga. Hivyo  tuna imani kubwa kwamba pilipilimanga itafanya vema kabisa Kagera” Bw. Murshid aliongeza pia kwamba zaidi ya miche 400 iliyosambazwa na Kampuni yao kwa majaribio kwa wakulima wa Bukoba, mingi imeendelea vema na kutia moyo.

Pilipilimanga ni zao linalochukua miaka miwili hadi mitatu kuanza kutoa matunda. Na kadri mti unavyozidi kukua ndivyo na uwezo wake wa kuzalisha unavyoongezeka. Tofauti na mazao mengine ya Biashara, pilipilimanga ni zao lisilohitaji nguvu sana kulistawisha wala muda mwingi wa kulishughulikia. Soko lake ni kubwa sana ndani na nje ya nchi. Pilipilimanga hutumika kama kiungo cha vyakula. Mathalani kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu, Waislamu wengi hutumia kiungo hiki katika uji. Kama ilivyo kwa mazao mengine, uzalishaji wetu wa ndani wa pilipilimanga hautoshelezi mahitaji. Hivyo Tanzania huagiza tani za zao hili kutoka India na Pakistan.

Maruk Vanilla wanatoa wito kwa wakulima pamoja na wadau wote wa maendeleo wenye nia ya kutaka kujiunga na kuvumisha ukulima wa  pilipilimanga mkoani Kagera kuunganisha nguvu. Kwa sasa Maruk Vanilla wanaendelea na jitihada za kuandaa vitalu vikubwa vya miche ya pilipilimanga. Yeyote mwenye nia ya kushiriki kwenye zao hili awasiliane na Maruk Vanilla, P.O Box 1361, Bukoba. E-mail: marukuvanilla at gmail.com au kwa simu namba: 0786972958/0713177372
 Next Post Previous Post
Bukobawadau