Bukobawadau

MRAJIS WA VYAMA VYA USHIRIKA NI KIKWAZO KWA USHIRIKA

Na Prudence Karugendo
BAADHI ya wanaushirika nchini wanaichukulia, kwa tuhuma, nafasi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini kuwa ipo kuukwamisha ushirika na kuudumaza badala ya kuustawisha na kuufanya ushamiri. Kwa sababu hiyo, wanajiuliza, nafasi hiyo ni ya nini inayofanya mambo kinyume na makusudio ya kuanzishwa kwake?
Wapo wanaodhani kwamba cheo cha Mrajis wa Vyama vya Ushirika kilianzishwa baadaye kabisa,  kama moja ya mikakati ya serikali ya kuuboresha na kuuimarisha ushirika nchini, sasa wanashangaa kuona mambo yanakwenda kinyume chake.
Wanaushirika wanasema kwamba haileti maana yoyote kuona kitu kinasajiliwa ilmradi tu, kwa maana ya ushirika, na kisha kinapotea bila kuonyesha manufaa yoyote yaliyochochea kikasajiliwa, na hasa ikizingatiwa kwamba kitu chenyewe kinagusa maisha ya watu walio wengi, wakulima,  kwa maana ya kuwa mhimili wa uchumi wao.
Katika makala hii nataka niitazame nafasi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika nikiwa upande wa Vyama Vikuu vya Ushirika vinavyoulinda uchumi wa wakulima, kwa kukishughulikia kile wanachohangaika kukizalisha katika kujaribu kuuinua uchumi wao sambamba na maisha yao.
Sio kweli, kama yalivyo mawazo ya baadhi ya wanaushirika, kwamba nafasi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika iliundwa baadaye wakati ushirika ukiwa umeishaanzishwa muda mrefu. Mrajis wa kwanza nchini aliteuliwa tarehe 4 / 3/ 1932, muda mfupi baada ya serikali ya kikoloni kupitisha Sheria ya Vyama vya Ushirika, tarehe 22 / 2 / 1932.
Kwahiyo wakulima wanapoamua kuunda ushirika wao, wakafuata itifaki zote zinazotakiwa kisheria, wanachokilenga ni kuziona juhudi zao katika kilimo zikiwalipa jasho lao. Kuwainua kiuchumi na kuwaondolea ufukara. Sio jambo la kwenda tu kwa Mrajis kuusajili ushirika wao na mambo kuishia hapo.
Kwa maana hiyo Mrajis wa Vyama vya Ushirika anapaswa kuwa kichocheo cha wakulima kutamani kuanzisha ushirika. Sababu ushirika unaposhamiri kwa upande wa wakulima kilimo nacho kinashamiri sawia, pia maana ya kuwepo kwa Mrajis inajionyesha mara moja na kuwavutia wakulima.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika anapofanya kazi yake kadiri inavyotakiwa ushirika unapanuka haraka kutokana na wananchi wengi kutamani kuanzisha vyama vya ushirika, watafanya hivyo kwa vile watakuwa wanayaona mafao yake yalivyo manono.
Mrajis wa kwanza hapa Tanganyika, pamoja na kazi hiyo ya kusajili vyama vya ushirika,  alikuwa akifanya kazi nyingine vilevile. Lakini ilipofika mwaka 1945 ilibidi aache kazi nyingine ili atumie muda wake wote wa kazi kwenye shughuli za vyama vya ushirika. Huo ni umuhimu wa ushirika ulioonwa na wazungu, wakoloni!
Hata serikali ilipotengeneza cheo cha Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Ushirika mwaka 1951, ilibidi cheo hicho kiunganishwe kwa mtu mmoja kwa vile madhumuni yake hayakutofautiana sana na ya Mrajis. Kwahiyo kati ya mwaka 1951 – 1971, kazi zote mbili zilikabidhiwa kwa mtu mmoja, Mrajis wa Vyama vya Ushirika.
Kutokana na serikali kuuona umuhimu wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika, pamoja na umakini uliokuwa ukionyeshwa na Mrajis wakati huo, ndiyo maana ushirika ulishamiri sana nchini kiasi kwamba katika kipindi cha karibu miaka 40, kati ya mwaka 1932 – 1971, idadi ya vyama vikuu vya ushirika nchini ilifikia 1854!
Idadi hiyo ni tofauti kabisa na idadi ya vyama vikuu vya ushirika vilivyoanzishwa, kama kweli vipo, katika kipindi chamiaka 40 iliyofuatia,  kati ya 1970 – 2010.
Kutokana na mabadiliko ya sera za nchi yaliyochangia mabadiliko ya mara kwa mara katika Sheria za Vyama vya Ushirika nchini, na hivyo umakini kutoweka na uzembe kutawala katika nafasi ya Mrajis, tumeweza kushuhudia maangamizi ya vyama vya ushirika yaliyovifanya vyama vikuu vibaki 44 tu nchini kote ilipofika mwaka 2004.
Na si ajabu ninapoandika makala hii vikawa vimebaki vyama vikuu visivyozidi 5 nchi nzima. Navyo vilivyopo ninaonekana kuchungulia kaburi.
Pamoja na idadi ya vyama vikuu vya ushirika nchini kupungua kwa kiasi hicho cha kusikitisha na kutia majonzi, huku vyama vilivyobaki vikionekana kuchechemea kama mgonjwa aliye mahututi, pasipo na jitihada za wazi za kuvinusuru, nafasi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika ndio kwanza inaanza kushamiri! Swali linalojitokeza ni la kwa nini nafasi hiyo ishamiri wakati madhumuni yaliyoifanya ikaanzishwa yamenyauka?
Wakulima wanaounda vyama vya ushirika wanawezaje wakajivunia nafasi hiyo ya Mrajis wakati wakiuona ushirika wao ukifa kifo cha kizembe? Au tuseme malengo ya nafasi hiyo yamebadilika, yamekuwa ya kuunyonga ushirika badala ya kuutengeneza na kuuendeleza?
Mbali na hilo la Mrajis kutovijali vyama vya ushirika, linajitokeza lingine la nafasi hiyo kuvichukulia vyama hivyo kama mkusanyiko wa watoto wenye mtindio wa ubongo, watoto wasioweza kujiamria lolote bila kuelekezwa la kufanya, tena kwa usimamizi wa karibu!
Utaraibu wa kwamba vyama vikuu vya ushirika haviwezi kufanya baadhi ya mambo yake bila idhini ya Mrajis ni jambo linaloleta utata katika vyama hivyo. Sababu kama watu wazima wanaweza wakaamua kuunda ushirika wanaouona una manufaa kwao kutokana na wanachokizalisha, inawezekanaje pale wanapotaka kupanua manufaa yao mtu mwingine, tena asiyekuwa mnufaika kwa lolote katika ushirika husika, awaamurie ni kipi cha kukifanya na kipi cha kukiacha? Hapo ndipo Mrajis anapoonekana ni kikwazo.
Jambo la kushangaza, kama sio kusikitisha, Mrajis anaweza akauona uovu unaofanyika ndani ya vyama vya ushirika dhidi ya makelele yanayopigwa na wanaushirika wakiomba msaada wake, yeye akaamua kufumba macho kama vile haoni kitu, akashindwa kutumia mamlaka yake aliyopewa kisheria kuingilia kati na kuufutilia mbali uovu unaopigiwa kelele!
Mfano  wanaushirika wanapopiga sana kelele bila msaada wowote toka kwa Mrajis mwishowe wanaishiwa nguvu na kunyamaza. Na huo ndio unakuwa mwisho wa ushirika husika. Vyama vikuu vingi vya ushirika vimeangamia kwa mtindo huo.
Hiyo maana yake nini? Hivyo tuendelee kujiaminisha kuwa bila Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini ushirika hauwezekani? Kama nafasi hiyo ipo kuuangamiza ushirika, basi ushirika unawezekana bila nafasi hiyo?
Ngoja nitoe mifano miwili iliyo hai. Kuna chama cha msingi kilichokuwa kati ya vinavyounda chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. cha Kagera.  Chama hicho cha msingi cha Magata, wilani Muleba, kimejitoa katika KCU na kinafanya mipango ya kuwa chama kinachojitegemea. Lakini kikwazo ni Mrajis Msaidizi mkoani humo.
Moja ya kanuni za vyama vya ushirika inasema kwamba “Chama chochote chenye madhumuni ya kuendeleza uchumi wa wanachama wake kufuatana na masharti ya vyama vya ushirika kinaweza kuandikishwa”. Lakini pamoja na kulielewa hilo Mrajis Msaidizi bado anakiwekea vikwazo, mbali na mambo mengine, ana madai ya kwamba kuna watu wawili wameongezeka katika Bodi ya chama hicho ambao yeye hawataki! Watu hao ni Enock John Babu na Yusuf Kakwata.
Wanaushirika wa Magata wanasema kwamba hizo ni sababu binafsi  za Mrajis Msaidizi kutokana na mazoea yake ya kuvichagulia vyama vya msingi watu wa kuingia kwenye Bodi za vyama hivyo badala ya wajumbe wa Bodi kuchaguliwa na wanaushirika.
Mfano wa pili ni wa Ilango, Kata ya Buterankuzi, Bukoba Vijijini. Wanaushirika wa Ilango wanata kuanzisha chama chao cha msingi ili wakajitenge na chama cha msingi cha Itongo, Kata ya Ibwera, Bukoba Vijijini. Sababu zilizowafanya wafikie uamuzi huo ni pamoja na umbali wa kutoka kata moja kwenda kata nyingine kwa ajili ya kupeleka mazao.
Kanuni mojawapo ya vyama vya ushirika inasema kwamba kwa upande wa vyama vya mazao wakifika watu 50 wanaweza kuanzisha chama cha msingi. Wanaushirika wa Ilango tayari wako 70. Na tayari wameishajenga ghala kubwa la kuhifadhia mazao, hasa kahawa, lililofunguliwa na Afisa Ushirika wa Wilaya ya Bukoba, 2013. Pamoja na hiyo wanasema tayari wameishafungua akaunti Benki.
Ibarahim Rwamlaza ni mwenyekiti wa wanaushirika hao wanaotaka kuanzisha chama hicho cha msingi cha Ilango. Rwamlaza anasema kikwazo pekee walicho nacho ni Mrajis Msaidizi. Anasema haelewi ni kwa nini Mrajis Msaidizi anawafanyia hivyo.
Naamini kwamba nafasi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika inatokana na Sheria ya Vyama vya Ushirika iliyoundwa na Bunge. Kwa maana hiyo ni muhimu Bunge letu, linaloundwa na wawakilishi wa wananchi, likairejea Sheria hiyo ya Vyama vya Ushirika na ikiwezekana kuifutilia mbali nafasi hiyo ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika.
Bunge linaweza kuutafuta utaratibu mwingine ulio bora utakaouwezesha ushirika kushamiri tena nchini kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, hasa tangu enzi za wakoloni. Hiyo ni iwapo kama wabunge wanawajali wananchi wanaowawakilisha.
Haiwezekani nafasi zilizopo nchini kwa ajili ya masuala ya ushirika, kama ilivyo Wizara ya Ushirika, Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Shirikisho la Vyama vya Ushirika nakadhalika, vishamiri wakati ushirika wenyewe ukiwa umekata roho.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau