Bukobawadau

PAPA NA NYANGUMI NI MIFANO IPASWAYO KUTUFIKIRISHA

Na Prudence Karugendo
 NILIPOANDIKA  juu ya Watanzania  kuponzwa na utulivu na wema wetu baadhi ya wasomaji walinipongeza na wengine kunilaumu. Vyote viwili, lawama na pongezi, sikuvitilia maanani kwa vile waliofanya vile niliona kuwa hawakunielewa vizuri.
Walionipongeza wengi wao walisukumwa na mtizamo wa ubaguzi wa rangi. Hawa imani yao ni kwamba uzalendo ni rangi, ukiwa mweusi basi wewe ni mzalendo, kwao haijalishi kama unatoka Msumbiji, Rwanda, Kongo au kwingineko nje ya nchi hii. Au kama unafanya matendo yasiyoendana na uzalendo. Ilmradi wewe ni mweusi basi, kwao inatosha. Mimi huo sio uliokuwa mtizamo wangu, mtizamo wangu ulikuwa uasilia wa nchi yetu na moyo wa kuipenda na kuifia nchi yetu.
 
Vilevile kuna walionilaumu kuwa nilichokiandika ni ubaguzi wa rangi. Hawa waliona kama nataka kurudisha mambo nyuma kwa kuyataja mambo ambayo wao wanaona yamepitwa na wakati. Pia katika kundi hilo la lawama kuna waliodhani naongelea vita ya papa na nyangumi ambavyo wanaona ningeviacha badala yake  nikayatizama maisha ya mwananchi wa hali ya chini.
 
Nataka nieleweke kwamba mimi siyo mbaguzi wa rangi hata kidogo, wala sikuandika kuonyesha chuki yangu kwa Wahindi. Mimi ninao marafiki zangu wengi  Wahindi, kama ningekuwa nawachukia ningewezaje  kuwa na urafiki nao?  Mimi ninachokichukia ni hulka ya Wahindi inayojionyesha imo katika utamaduni wao, ubaguzi. Hata wao uwa nawambia hivyo. Wanabaguana hata wao kwa wao!
 
Sioni kwa nini tukalazimike kuuheshimu utamaduni wao huo wa kishenzi wanaouendeleza hadi huku kwetu kiasi cha kufikia kutubagua hata sisi tuliowakaribisha. Utamaduni ukiwa wa kishenzi, wa kuumizana ndani ya jamii yoyote, unapingwa kwa kuzingatia wakati uliopo. Ndiyo maana ukeketaji wa wanawake unapingwa kwa nguvu zote japo tendo hilo limo katika baadhi ya tamaduni.
 
Wasomaji wengine walidhani kwamba niliandika kuonyesha upande niliopo kati ya nyangumi na papa. Ukweli ni kwamba nilikuwa sijashawishika kuvutika upande wowote kwa vile ni upande mmoja tu  uliokuwa umetoa mashambulizi yake ya kushtukiza. Ile ilikuwa ni bahati mbaya tu kwamba makala yangu ilitoka kipindi kile mashambulizi yale yanaanza, wala makala yangu haikuwa na uhusiano wowote na mashambulizi yenyewe.
 
Vilevile kuna ambao kwa neno  la Kiingereza naweza kuwaita “naive”, sipati haraka neno la Kiswahili lenye maana hiyo, walionipa ushauri wa kwamba vita hiyo tungeiacha tukaongelea maisha ya wananchi wa hali ya  chini. Ingawa sikuwa kwenye vita hiyo lakini niliwaeleza kuwa kama wewe ni samaki mdogo huna jinsi ya kuviona vitimbwi vya papa na nyangumi havikuhusu wakati mko kwenye bahari ileile moja.
 
Nieleze kidogo kuhusu watemi hawa wawili wa baharini. Papa nisamaki mdogo kulinganisha na nyangumi ila ni mkorofi sana kuliko nyangumi. Nyangumi akilinganishwa na papa kitabia ataonekana ni mtulivu sana na wakati mwingine kuonekana mwenye huruma. Ila angalia, kwa ukubwa wake wa umbo havuliwi kirahisi kama papa mwenye makeke. Na kwa wema wake huachia domo lake kubwa samaki wadogo waingie wakidhani wamepata mahali salama pa kujihifadhi kumbe ndio kwanza wanageuzwa asusa.
 
Vilevile papa anaweza kutunisha mgongo wake ukaonekana kama kisiwa kidogo kiasi cha kuwapa matumaini hata wavuvi kuwa wamepata mahali pa kujipumzisha, kumbe ile ni hadaa ya nyangumi, anataka azame na kuwazamisha wote walioweka matumaini mgongoni kwake. Huo ndio ubaya na hatari ya nyangumi tofauti na papa ambaye kutokana na ukorofi wake kila kiumbe cha baharini kimeishaelewa kiishi naye vipi, hata  wavuvi nao  wameishausoma ukorofi wake ndiyo sababu ya papa kuvuliwa mara kwa mara tofauti na nyangumi.
 
Kwahiyo nadhani kutajwa kwa mfano wa nyangumi hakukusukumwa tu na jazba iliyotokana na mfano wa kwanza wa papa, bali huu unaonekana ni mfano uliotolewa kiumakini kwa kuzingatia mwenendo wa hali halisi ulivyo nchini mwetu na hasa katika vita hii tuliyomo ya kupambana na ufisadi. Vita hii ambayo kila mmoja anaweza kunyoosha kidole kwa mwenzie kuwa ndiye adui ili kuyazubaisha mashambulizi ya pamoja inatugeuza kama watu tuliozama baharini tukiwa tunatapatapa tukitafuta  pa kushika ili kujinusuru, hapo ndipo tunapotahadharishwa na hadaa za nyangumi ambaye kwa upole wake anaweza kutufunulia domo lake ili tuingie tukidhani kwa kufanya vile tumejinusuru kumbe ndio kwanza tumejigeuza chakula chake.
 
Hii inapaswa ibomoe fikira za kwamba vita hii dhidi ya ufisadi tunaweza kuifanikisha kwa kutumia mbinu  za ubaguzi, ukabila au madhehebu. Yeyote anayetushawishi kutumia mbinu hiyo tayari anakuwa amejigeuza nyangumi kwa kujifanya mpole na kutufunulia domo lake tuingie wenyewe eti kwa kutuonea huruma baada kutuangalia tunavyotapatapa. Kumbe kuingia kwetu ndani ya domo lake ndio unakuwa mwisho wa yote. Hakuna cha vita dhidi ya ufisadi kitakachokuwa kinaendelea maana tutakuwa tumemezwa na ufisadi wenyewe.
 
Kwahiyo tunapopigana vita hii inabidi tujihadhari na chuki, husda, vinyongo, ushindani nakadhalika. Mambo haya tusipoyaangalia ni lazima yatugawe katika makundi niliyoyataja hapo juu. Ni rahisi mtu kusema anashambuliwa kwa vile ni wa  madhehebu fulani, kabila fulani au rangi fulani, na hivyo kuwashawishi walio mstari wa mbele katika mapambano kuvunjika moyo kwa vile anayeshambuliwa kaishajionyesha ni wa rangi yao, kabila lao au madhehebu yao.
 
Kwahiyo mashambulizi yanagawanyika na si ajabu yakageuka ya kushambuliana wenyewe kwa wenyewe badala ya kumshambulia adui. Vita inakwama na adui anashinda kirahisi.
 
Katika makala yangu niliyokuwa nawataja Wahindi kwa tabia yao chafu ya ubaguzi sikusukumwa na mtizamo wa rangi yao, tatizo langu ni tabia yao. Kwahiyo walionipongeza kwa misingi ya ubaguzi wa rangi kwamba kwa kuwataja Wahindi pengine nilimaanisha na Wazungu, Waarabu Waajemi nakadhalika, hao walikuwa wamepotea kabisa. Hawa wengine, japo rangi zao zinashabihiana na ya Wahindi, weupe, tabia zao ni tofauti kabisa. Kitu cha Mhindi hakiguswi na asiyekuwa Mhindi. Angalia hata dini yao Hindu, ni ya Wahindi watupu,  tofauti na hizi dini nyingine tulizozizoea, Ukristu na Uislamu.
 
Ningewataja Waarabu na Wazungu kweli ningekuwa mtu wa ajabu, sababu hawa ni watu ambao nina undugu nao wa damu. Ninao binamu zangu Waarabu, ninao shemeji zangu wengi Waarabu kwa maana hiyo ninao wapwa zangu wengi wenye asili ya Uarabu. Vilevile niye baba mdogo mzungu, mkwe wangu mzungu, shemeji zangu wawili wazungu.  Kwahiyo ninao wadogo zangu wazungu, wapwa zangu wazungu  nakadhalika. Watu hawa nitawasemaje kwa mtizamo wa ubaguzi wa rangi?
 
Wahindi ndio wanaotubagua, najiuliza kwa nini?
 
Kama nilivyosema,  Waarabu na Wazungu tunaishi kiundugu, kule kwetu wamelima mpaka mashamba ya migomba “ebibanja” na kujenga nyumba za kudumu. Sio watu wanaopendelea kuishi mijini tu wakiwa wamekaa mkao wa kuondoka wakati wowote kama wenzetu Wahindi. Hilo tuliangalie kwa umakini.
 
Lakini hatahivyo kitendo cha Wahindi kutubagua hatuwezi kukigeuza kichaka cha kuficha maovu yetu. Kwamba mtu anapofanya matendo yanayoisaliti jamii yake, ufisadi, atuelekeze kwenye kichaka kile cha Wahindi, au watu kutoka nje,  kuwa ndimo ulimo uchafu wote ili yeye asigeuziwe shingo. Inabidi kwanza tujisafishe sisi wenyewe na kujihakikisha kuwa tumetakata kabla ya kampeni yetu ya usafi kuihamishia kwingine.
 
Tusikubali mtu yeyote kati yetu kuiingilia kampeni hii na kutushawishi kufanya usafi nje kwa madai kwamba ndiko kulikochafuka sana na kukuacha ndani. Kwa namna hiyo ni lazima mtu huyo atakuwa amekalia rundo la uchafu hasiotaka uondosheke. Mtu huyo ni hatari kwetu. Katika kampeni hii ya usafi, vita dhidi ya ufisadi, mtu wa aina hiyo inabidi tumchukulie kama uchafu na pengine kutulazimu kumsafisha pamoja na uchafu wake. Bila kufanya hivyo tutakuwa tunajisumbua na kupoteza nguvu zetu bure, kusafisha nje tukiuacha uchafu ndani.
 
Hii ni kwa sababu nchi yetu ilivyo hakuna namna yoyote ambayo watu wa rangi fulani, hususan wenye rangi ya asili ya nje, wanavyoweza kufanya ufisadi unaohatarisha nchi bila ya kuwa na mwongozo wa watu wenye asili ya ndani.
 
Hicho ni kitu kisichowezekana. Ushauri wa kuwasakama watu wa rangi fulani tu kuwa ndio wanaoihatarisha nchi kiufisadi nauona kuwa ndio hatari zaidi kuliko hata huo ufisadi uanotajwa. Nasema hivyo nikizingatia ushahidi ambao umeishajionyesha ambapo watu wenye asili ya nje wameishaishinda serikali mahakamani mara kadhaa na kuamuriwa serikali iwalipe mara nyingi ya kiasi wanachokuwa wanatuhumiwa nacho. Hiyo ndiyo sababu inayonifanya  niuone ushauri wa aina hiyo kuwa ni wa hatari kwa nchi yetu.
 
Endapo serikali itauzingatia ushauri huo si ajabu Hazina ya nchi ikawa inafanya kazi ya kulipa tu fidia huku kila kitu kikiwa kimesimama. Kwahiyo vita yetu dhidi ya ufisadi ni lazima tuipeleke kwa uangalifu tusije tukajikuta tunaiingia kwenye mtego wa adui na kuangamizwa sote, au tukafanya uzembe kama huu unaotaka kujitokeza tukaishia kujilipua wenyewe.
 
Pia wapo wenye ushauri wa kwamba tunapowasaka mafisadi tusiangalie maisha binafsi ya mtu, huu ni ushauri wa ajabu! Maana kwa kuufuata ushauri wa aina hiyo inabidi hata  vita hii ya ufisadi tuachane nayo kwa vile ufisadi umejificha ndani ya maisha binafsi ya watu. Hakuna anayefanya ufisadi kwa ajili ya umma. Kila ufisadi unalenga katika maslahi binafsi dhidi ya maslahi ya umma.
 
Namalizia kwa kusema kwamba nimelazimika kuonyesha msimamo wangu baada ya makala yangu moja kuwa imewapotosha watu nakuonekana mimi naunga mkono ubaguzi wa rangi kitu ambacho kwangu ni mwiko.
  
Nasema kwamba vita dhidi ya ufisadi inapaswa kupiganwa kwa kuwalenga tu maadui, ufisadi na mafisadi, bila kuangalia rangi zao, makabila yao, wala madhehebu yao. Anayejaribu kutushawishi kuwa rangi fulani ndiyo ya ufisadi inabidi tumuogope kama ukimwi. Maana sumu hiyo ikishatuingia haitutoki asilani, nchi itakuwa imeugua ukimwi wa aina yake. Inabidi tumpuuze huku tukijiuliza lengo lake ni lipi hasa? Isije ikawa anatutishia papa ili tupande mgongoni kwake tukidhani ni kisiwa salama kumbe ni nyangumi anayetaka azame na kutuzamisha wote.
 
 
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau