Bukobawadau

UBABE,UKOSEFU WA HOJA NA HEKIMA VINAIPELEKA NCHI KUZIMU!

Na Prudence Karugendo
TANZANIA, tangu ikijulikana kama Tanganyika, imejivunia amani na utulivu kiasi cha kujiita kwa mbwembwe kuwa ni kisiwa cha amani, kama ilivyo kwa kisiwa cha kijani katikati ya jangwa.
Lakini hatahivyo, amani na utulivu si vitu ambavyo tunaweza kudai kuwa vinatudondokea tu kutokana na Mungu kutupendelea, vitu hivyo vinatengenezwa na sisi wenyewe katika mfumo tulioamua kuuishi. Katika jamii yoyote iwayo kutendeana haki, uongozi kujiepusha na ubabe pamoja na kuwa na uwezo wa kujenga hoja zinazowashawishi wanajamii  kutokuwa na fikra za kuanzisha vurugu, ni mambo muhimu na nyeti katika kuifanya jamii husika iwe na vitu hivyo, amani na utlivu.
Ukosekano wa vitu kama haki, hekima, busara na kutopenda kuonyesha ubabe katika jamii, ni mwanzo wa vurugu zinazoweza kuipeleka nchi yoyote katika maangamizi. Ni kwa sababu hakuna mwanadamu aliye tayari kuuona ukosekano huo ukitamalaki na yeye akavumilia hali hiyo hata awe mnyonge kiasi gani.
Nchi yetu, Tanganyika,  kwa mfano, ilijaaliwa kupata uongozi wenye hekima na uwezo wa kujenga hoja hata kabla ya kujitawala yenyewe.
Ikumbukwe kwamba Tanganyika iliondolewa kwenye ukoloni baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia iliyoisha kwa mkoloni wake, Ujerumani, kusalimu amri mwaka 1918. Baada ya hapo Tanganyika ikawekwa chini ya uangalizi wa Jumuiko la Mataifa (League of Nations), kabla ya Umoja wa Mataifa (United Nations)  na kazi hiyo ya uangalizi ikaachiwa ifanywe na Uingereza.
Lakini baadaye Uingereza ikanogewa na kuigeuza Tanganyika  koloni lake ambalo lakini haikulijali sana kama yalivyokuwa makoloni yake mengine.
Wakati tumeanza kudai uhuru ili tujitawale sisi wenyewe, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, bingwa wa kujenga hoja, alitamka kwamba Waingereza walipaswa kutuachia uhuru wetu sababu sisi hatukuwa koloni lao, kwamba kama wangeng’ang’ania tungewashitaki Umoja wa Mataifa. Na endapo kule tusingesikilizwa basi tungewashitaki kwa Mungu!
Nilibahatika kupata fursa ya kumuuliza Mwalimu alikuwa na maana gani kwa kauli yake hiyo ya kuwashitaki Waingereza kwa Mungu, akanifafanulia kwamba ilikuwa na maana ya kushika silaha kisha kuingia msituni na kuudai uhuru wetu kwa nguvu. Akaongeza kwamba alipolifikiria hilo la kushitaki kwa Mungu machozi yakamtoka.
Kwa upande mwingeni, wenzetu wa Zanzibar waliamua kushitaki moja kwa moja kwa Mungu, mashitaka yao yakakubaliwa, na ndiyo Mapinduzi ya mwaka 1964. Pengine ndiyo maana yanaitwa Mapinduzi Matukufu mpaka sasa.
Kwa upande wa Tanganyika hoja za Mwalimu zilikuwa na nguvu sana kuliko hata risasi, hivyo hakukuhitajika silaha, Waingereza wakanywea na kutuachia uhuru wetu. Uhuru bila kumwaga damu, jambo lililo nadra sana.
Lengo la makala hii ni kuonyesha kwamba uongozi unapokuwa na hoja unaiepusha jamii unayoiongoza na upelekaji wa mashitaka kwa Mungu. Sababu gharama yake ni kubwa mno. Ndiyo maana machozi yalimtoka Baba wa taifa alipolifikiria hilo. Ila bahati nzuri ujenzi wake wa hoja ukaipusha nchi na kitu hicho.
Kitu kingine ninachotaka kukiangalia hapa ni kuhusu viongozi kutenda haki. Inapotokea uongozi wa nchi ukashindwa kutenda haki, jamii inayoongozwa au sehemu yake, inajikuta ikilazimika kupeleka mashitaka kwa Mungu. Hiyo ni kwa sababu kote ambako mashitaka husika, ya kukosekana kwa haki, yangepelekwa kunatokana na uongozi ulioshindwa au kutotaka kutenda haki.
Maana baada ya uongozi au utawala kutotaka kutenda haki kinachofuatia ni ubabe wa kuwafanya wanaonyimwa haki zao wanyenyekee na kuutii utawala husika. Jamii itatawaliwa kadri ya matakwa ya watawala yalivyo. Na katika kuitawala jamii yoyote ubabe wa aina hiyo lazima uwe na mwisho wake. Kamwe mwisho huo hauwezi kuwa mwema hata siku moja. Mara nyingi huo unakuwa ni mwisho wa kimaangamizi.
Tunaweza tukajikumbusha baadhi ya matukio yaliyotokana na ubabe katika utawala. Nchi ya Uganda iliwahi kuwa na mtawala mbabe, Idd Amin Dada. Ubabe wake ulifurika Uganda nzima na kulazimika kusambaa mpaka Tanzania, huku yeye akijiita, pamoja vituko vingine, kuwa ni rais wa maisha wa nchi hiyo!
Ndipo Tanzania ikalazimika kupeleka mashitaka  kwa Mungu, ikaingia vitani ili kujinusuru na ubabe pamoja na vituko vingine  vya mtu huyo. Maisha ya baadhi ya wananchi na askari wa pande mbili, Tanzania na Uganda, yakateketea zikiwemo mali na miundombinu. Lakini ubabe wa mtawala huyo ukakomeshwa ila kwa gharama hiyo kubwa.
Mbali na hiyo, tumeshuhudia ubabe wa mtawala wa Irak, Saddam Hussein, ulivyokomeshwa na kuiacha nchi hiyo haitamaniki. Mpaka leo nchi hiyo imeshindwa kutulia na kubaki ikionekana kama jahanamu, mahali pa kusadikika ni pachafu, kiimani.
Lakini kama hekima ingemtokea mtawala huyo, akaachana na ubabe, hali ya mambo nchini Irak isingekuwa kama ilivyo kwa sasa, na pengine yeye ingemsaidia kuyanusuru maisha yake.
Vilevile tumeona jinsi uvumilivu ulivyowaishia wananchi wa Tunisia baada ya watawala wao kushindwa kutenda haki, kukosa uwezo wa kujenga hoja, badala yake wakaendekeza ubabe. Wananchi wakaamua kupeleka malalamiko yao kwa Mungu. Na kawaida Mungu hawatupi mkono waja wake.
Vivyo hivyo nchini Misri na nchini Libya. Kule Libya, pamoja na mema yote aliyoyafanya, Muamar el Gadaffi, kwa wananchi wake, lakini ubabe wake wa kuwanyima watu wake haki ya kujifanyia maamuzi umemgharimu maisha yake baada ya wananchi hao kufikisha kilio chao kwa Mungu. Mpaka sasa Misri na Libya hakujatulia, na hakuna anayejua patatulia lini.
Sudan Kusini, nchi changa kuliko zote katika Afrika, sasahivi nayo imegeuka jahanamu! Tamaa ya madaraka na ubabe wa viongozi wa nchi hiyo vinavy ochochewa na ukosefu wa uwezo wa kujenga hoja vimegeuka kiama kwa wananchi. Maisha ya watu yanateketea, wale ambao bado wamenusurika wako katika shida isiyosemekana!
Kule Afrika ya Kati tunaona jinsi ubinadamu ulivyopotea kabisa. Binadamu wanaendesha maisha ya kutisha kuliko hata ya wanyamapori! Fikiria mtu anamuua mwenzake, anamkata mguu na kuanza kuutafuna hadharani! Hayo yote yanasababishwa na uongozi au utawala mbovu, utawala ulioishiwa hekima na uwezo wa kujenga hoja zinazokubalika kwa watu.
Syria nako kumegeuka jahanamu! Utu umepotea, watawala wanawaza kutawala tu bila kujali maisha na uhai wa wananchi ukoje. Watu wanakufa kama sisimizi, watawala wanaona cha muhimu ni kulinda tu utawala wao, acha watu wateketee, kinacholindwa ni utawala, sio watu!
Tunapoyaangalia yote hayo bado sisi Tanzania tunaamini kwamba tuko hivi tulivyo, amani na utulivu, kutokana na Mungu kutupendelea! Mpaka viongozi wetu wanafikia kutoa kauli za ajabu bila kujali ni madhara gani yanaweza kutokana na kauli hizo! “……mimi nasema wapigwe tu maana tumechoka…..”! Hakuna kujiuliza kwamba wanaoamriwa wapigwe wakiamua kusema hapana, nasi tumechoka, kinachoweza kufuatia ni nini!
Sababu wananchi wakishasema hapana, hatukubali kupigwa tu, elewa kwamba kauli hiyo ya umma tayari iko kwa Mungu. Yanayoweza kufuatia waziri mkuu anakuwa hayawezi tena. Anachoweza kufanya ni kukaa akijutia kauli yake ya wapigwe tu.
Wahaya wanasema “ekiruga kanwa tikishubamu” wakimaanisha kwamba kitokacho kinywani hakirudi tena kinywani, kwa maana ya kwamba hakifutiki.
Mara hii mwenyekiti wa chama tawala, rais na Amiri Jeshi Mkuu, anawambia wanachama wake kwamba wasiwe wanyonge, eti wajibu mapigo ya wapinzani! Anatoa mifano ambayo naamini kwamba kapewa maelezo ya kuchongwa na wasaidizi  wake. Eti ndiyo iliyomfanya akafikia kutoa kauli hiyo.
Mwenyekiti wa CCM anasema kwa uhakika kana kwamba aliwaona waliotenda anayoyatolea mifano. Ila hasemi yeye akiwa rais, kwa nini hakuamuru waliohusika na matukio anayoyataja, kama ya kutobolewa macho kwa bisibisi pamoja na kumwagiwa tindikali, wakamatwe mara moja, kama walionekana na kujulikana kuwa ni wapinzani, ili wakafikishwe kwenye vyombo vya sheria. Kama hilo halikufanyika kwa nini aendelee kuwa na uhakika kwamba waliohusika ni wapinzani?
Lakini hatahivyo mwenyekiti wa chama tawala, CCM, hasemi  lolote kuhusu mashambulizi ya wazi yanayofanyika dhidi ya wapinzani! Mbali na anayesemekana kutobolewa macho na mwingine kumwagiwa tindikali, mwenyekiti wa CCM haonekani kukumbuka kuwa Chadema walishambuliwa kwa bomu la kivita wakiwa kwenye mkutano wa hadhara, bomu lililoua baadhi ya watu na kujeruhi wengine kadhaa Mjini Arusha!
Hakumbuki jinsi Polisi wanavyotumia nguvu ya ziada kusambaratisha mikusanyiko halali ya vyama vya upinzani, mfano kule Morogoro ambako risasi za moto zilitumika moja ikimuua kijana muuza magazeti aliyekuwa hahusiki na mkusanyiko halali wa Chadema!
Mwenyekiti wa CCM haongelei chochote kuhusu fujo zilizodhamiriwa na aliyekuwa Mkuu wa Polisi (RPC) mkoani Iringa, Michael Kamuhanda, na fujo hizo kuishia kwa mauti ya mwanahabari, Daud Mwangosi, kijijini Nyololo, Mfindi, Iringa.
Swali la muhimu kujiuliza ni kwamba, kama kweli wapinzani wanafanya fujo inakuwaje Amiri Jeshi Mkuu awambie CCM wajilinde na kujibu mashambulizi? Ina maana kalifuta Jeshi la Polisi? Au anayoyaona yakifanywa na vikundi vya Seleka na Ati-balaka kule Afrika ya Kati anaona  kuwa ndiyo yanayofaa?
Je, Jumuiya ya kimataifa, ambayo muda wote inahangaika kwa hali na mali kupatanisha penye machafuko, hasa haya ya kujitakia, inapomsikia JK akitoa amri ya aina hiyo kweli itaendelea kumuona kama mtu aliyedhamiria kukomesha machafuko na kuleta upatanishi katika nchi nyingine wakati kwake akiyaandaa machafuko ya aina ileile?
Nimalizie kwa kusema, vyovyote iwavyo tuelewe kwamba hoja na hekima ndio mhimili wa amani na utulivu wetu. Tunapoviacha vitu hivyo vitoweke kinyemela basi hatunabudi kuelewa kuwa tumejiweka njiapanda ya kuelekea kuzimu.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau