“EKA MBE” KANALI FABIAN MASSAWE
Na Prudence Karugendo
NIANZE makala hii kwa usemi wa lugha maarufu mkoani
Kagera, Kihaya, usemao kwamba “ebitagira mahyo tibyera”.
Usemi huo hauna tafsiri ya moja kwa moja katika Kiswahili isipokuwa kwa maelezo
yaliyozunguka ili kupata maana yake. Ni kwamba Wahaya wanaamini kwamba mtu
akiwa analima shambani asipopata mtu wa kumpa pole ya kazi mazao anayoyalima
hayawezi kusitawi vizuri. Lakini hatahivyo mantiki ya usemi huo ni kwamba
juhudi zozote zisizothaminiwa inakuwa ni kazi bure. “Ebitagira mahyo tibyera”.
Nimeanza na
maelezo hayo kusudi nipate kueleweka katika kusudio langu la makala hii ya
kumpongeza mkuu wa mkoa wa Kagera, Kanali Fabian Massawe, kwa juhudi zake
anazozionyesha za kuuinua tena mkoa huo
ambao kwa miaka ya karibuni uliporomoka sana kimaendeleo.
Itakumbukwa
kwamba tangu enzi za wakoloni kulikuwepo na jamii za makabila mawili katika
iliyokuwa Tanganyika zilizokuwa juu kimaendeleo; jamii za Wahaya na Wachagga.
Kuwepo juu kimaendeleo kwa jamii hizo
mbili kulileta aina ya ushindani kati ya
Wachagga na Wahaya, ushindani wa kimaendeleo wa kutaka kuonyesha nani zaidi
kati yao.
Ni katika
hali hiyo kulipojitokeza imani kwamba Mhaya asingeweza kuongea Kichagga wala
Mchagga kuongea Kihaya. Lakini kwa sasa hayo yamekwisha na kubaki kwenye
historia. Hiyo inatokana na ukweli kwamba hakuna tena ushindani wa kimaendeleo
kati ya Wachagga na Wahaya ambapo hali halisi kwa sasa inaonyesha kwamba
Wachagga wamewaacha mbali Wahaya kimaendeleo. Huo ni ukweli usio na ubishi.
Hilo
linajidhihirisha kwa njia mbalimbali. Nakumbuka siku moja nilimshukuru kiutani
rafiki yangu Mchagga kwa lugha yake kwa kumwambia “aika mbe” jamaa mmoja
aliyekuwa karibu akabaki mdomo wazi akisema kwamba kweli dunia sasa
imebadilika! Akaongeza kuwa zamani Mhaya kuongea Kichagga au Mchagga kuongea Kihaya
ilikuwa sawa na Mwislamu kula nyama ya nguruwe! Lakini kwa sasa Wachagga
wanaongea Kihaya na Wahaya wanaongea Kichagga. Hiyo ni kwa sababu upinzani
uliokuwepo wa kimaendeleo kati yao haupo tena. Tumekubali yaishe.
Lakini
hatahivyo nimegundua kwamba ukosefu wa ushindani wa kimaendeleo si jambo jema.
Unadumaza maendeleo kwa ujumla. Kunapokuwa hakuna changamoto kutoka upande
wowote ni vigumu jamii kupaona mahali ilipozembea ili ipafanyie kazi. Kwa maana
hiyo kutoweka kwa ushindani wa kimaendeleo uliokuwepo kati ya jamii ya Wachagga
na jamii ya Wahaya ni jambo ambalo haliwafurahishi Wachagga, pamoja na
kuonekana kwa sasa wako mbele ya Wahaya kimaendeleo. Kumbe Wachagga wangependa
ule ushindani wa karibu kati yao na Wahaya uendelee ili uzidi kuchochea kasi ya
maendeleo.
Ukweli wa
jambo hilo umedhihirishwa na uteuzi wa Kanali Fabian Massawe, Mchagga, kuwa
mkuu wa mkoa wa Kagera. Katika maneno yake, Kanali Massawe, anaonyesha kutoka
rohoni mwake jinsi anavyosononeshwa kuuona mkoa ambao ulikuwa ukitamba kwa maendeleo
ukiwa ni mfano kwa ajili ya mikoa mingine kuiga, ulivyorudi nyuma kwa kasi ya
kutisha. Ni kwa sababu hiyo Kanali Massawe ameamua kuupeleka mchakamchaka mkoa
huo ili kujaribu kuurudisha katika kiwango ulichokuwa nacho huko nyuma.
Moyo huo
alio nao Massawe wa kuuinua mkoa wa Kagera siwezi kusema kwamba unatokana na
bidii tu ya uchapa kazi, ni lazima kuna kitu cha ziada, kuna msukumo wa ziada.
Na msukumo huo ni historia niliyoiongelea kidogo hapo juu.
Sio kwamba
mkoa huo mpaka unadorora kiasi hicho haukuwa nao wakuu wa mkoa, maana kwa
kipindi cha karibu miaka 30 na zaidi mkoa huo umekuwa nao wakuu wa mkoa kadhaa
wakichapa kazi ila kwa namna tofauti na namna anavyofanya Massawe kwa wakati
huu. Waliomtangulia walichapa kazi lakini hatahivyo mkoa ukawa unarudi nyuma
badala ya kusonga mbele.
Pia wapo
waliokuwa wakienda Bukoba kwa vitisho wakisema kwamba mkoa huo muda wote
umekuwa juu kimaendeleo kwahiyo ingebidi ufunge breki na kuisubiri mikoa
mingine. Vilevile yupo aliyewahi kutamka kwamba mie nimekuja kiboko yenu
mtanitambua! Katika hali kama hiyo ni kitu gani kingeuzuia mkoa huo usidorore?
Kwa
kuyakumbuka hayo ndiyo maana nasema utendaji wa Massawe una kitu cha ziada
zaidi ya uchapa kazi. Massawe ni lazima anasukumwa na historia ya jamii ya mkoa
wake na ile ya jamii ya mkoa anaoutumikia kwa sasa. Bilashaka anashangazwa na
kusikitishwa na tofauti inayojionyesha kwa sasa kati ya jamii hizo mbili, jamii
zilizokuwa zimekabana kimaendeleo miaka ya nyuma.
Kwa
kuzitumia sifa alizo nazo Massawe ameanza kuonyesha matumaini ya kuuinua mkoa
wa Kagera na kutaka kuurudisha tena kwenye chati. Na kwa vile anaonyesha
dhamira inayotoka rohoni mwake, dhamira yenye msukumo wa kihistoria, sina shaka
atafanikiwa kutimiza lengo. Lengo la kuuona mkoa wa Kagera ukirudi katika
ushindani wa kutambiana kimaendeleo na mkoa wa Kilimanjaro pamoja na mikoa
mingine ambayo nayo kwa sasa imechomoza kimaendeleo.
Kama
ninavyoonyesha, Massawe ni kamanda msitaafu
wa jeshi. Hiyo ni sifa ya kwanza inayoonyesha kuwa mkuu huyo wa mkoa yuko
tayari kuongoza katika hali yoyote ngumu. Sababu kama alikuwa tayari kuongoza
katika hali ya vita, au katika vita, sioni ni ugumu gani utakaomfanya ajione
mnyonge katika hali ya amani na kushindwa kuwaongoza raia dhidi ya ufukara usio
na silaha wakati alizoea kuwaongoza wanajeshi katika mapambano ya silaha.
Sifa
nyingine ni kwamba yeye ni mwalimu kitaaluma. Mwalimu anazo mbinu na maarifa ya
kumwezesha mtu kukielewa kilichokusudiwa. Kwa sifa hiyo Massawe anayo nafasi ya
kuwafanya wana Kagera wauone ukweli wa kwamba wamerudi nyuma sana kutoka pale
walipokuwa miaka ya nyuma, na si kuuona ukweli huo tu bali kuuchukia na hivyo
kutamani kurudi kwenye nafasi yao waliyokuwepo na hata zaidi.
Fikiria
Wahaya, kabila moja maarufu mkoani
Kagera, lililokuwa linajivunia elimu kiasi cha kujulikana kiutani nchi nzima
kama “nshomile” kwa maana ya nimeelimika, sasa hivi shule zilizo katika maeneo
yao ndizo zinazofanya vibaya zaidi katika mitihani ya taifa! Neno “nshomile”
limebaki kutumika tu katika utani
uliojaa kebehi. Haiwezekani watu wa jamii hiyo wafanye madudu kielimu halafu neno
hilo liendelee kuwa na maana.
Lakini
kulingana na mikakati aliyonayo Kanali Massawe kwa upande wa elimu, na ikizingatiwa
kuwa yeye ni mwalimu kitaaluma, nina imani kwamba atawarudisha akina “nshomile”
kwenye majivuno yao hayo yakiwa ya kweli na siyo majivuno ya kubaki wameegemea
kwenye historia ya kwamba iliwahi kutokea eneo lao likatoa wasomi. Yeye anataka
Bukoba na Kagera kwa ujumla paendelee kutoa wasomi wa kweli kweli kama ilivyo
mkoani Kilimanjaro, kusudi wengine watakapokuwa wanasema wale ni akina “nshomile”
wawe ni nshomile kweli na siyo kebehi.
Kudorora kwa
mkoa wa Kagera kulikuwa kumeingilia tabia mpaka tamaduni za watu wa mkoa huo!
Mfano kabila la Wahaya ni moja ya makabila yenye utamaduni wa usafi hapa
nchini. Ni utamaduni huo uliowaepusha na milipuko ya ugonjwa wa kipindupindu
ambayo imeyasakama makabila karibu yote nchini isipokuwa Wahaya tu. Lakini kwa
miaka ya karibuni utamaduni huo ulianza kuingiliwa na kuonekana kama
unabadilika. Hali halisi ya mabadiliko hayo ilikuwa inajionyesha mara tu mtu
alipokuwa anaingia katika mji wa Bukoba, mji ambao umo katika eneo la Buhaya.
Uchafu ndio uliokuwa ukitangulia kumkaribisha mgeni aliyekuwa akiingia kwenye
mji huo na kuyaonyesha mabadiliko yaliyokuwa yanaukabili utamaduni wa Wahaya.
Kwa sasa
jambo hilo nalo linaonekana kushughulikiwa kiukamilifu na Kamanda Massawe. Kwa
mujibu wa mwandishi Joyce Lobozi aliyeongea na mkuu huyo wa mkoa hivi karibuni,
Kanali Massawe anasema mwitikio wa wananchi katika kuyaweka mazingira kwenye
hali ya usafi ni mzuri. Na yeye amejipangia kila siku ya Alhamisi kuwa siku ya
kukagua usafi katika maeneo mbalimbali mkoani humo. Kwa maana hiyo Bukoba bila
uchafu inawezekana, kama ilivyowezekana huko nyuma.
Pamoja na
hayo yote ningependa nimkumbushe Kamanda Massawe kitu kimoja . Ni kwamba mganga yeyote hawezi
kuutibu ugonjwa asiouelewa. Mtu anayeumwa tumbo lakini akienda kwa mganga
anadai anaumwa kichwa ni vigumu kupata msaada wa mganga.
Ni kwamba
tofauti na ilivyozoeleka kwamba Wahaya ni watu wanaojipendelea, ukweli ni
kwamba Wahaya ni watu wa ajabu sana. Tunaweza kujiuliza, iweje watu
wanaojipendelea maendeleo yao yarudi nyuma kwa kasi ya kutisha kiasi hiki? Hilo
ni tatizo la kuumwa tumbo lakini kwa mganga ukadai unaumwa kichwa, mganga
atatibu kichwa huku tumbo likiendelea kukusumbua.
Tatizo la
kweli linaloisumbua jamii ya Wahaya, jamii kubwa kuliko zote mkoani Kagera,
liko hivi. Wahaya hawana umoja wala mshikamano. Anapotokea mmoja akapatwa na
tatizo inakuwa shangwe kwa wengine, wataanza kusema, muache aipate…..kakoma
kuringa…..kaisha yule nakadhalika. Likimpata mwingine naye itakuwa hivyohivyo.
Hawana wazo la kuunganisha nguvu ili kulikabili tatizo linaloanzia kwa mmoja
kusudi lisisambae kwa wengine. Matokeo yake ndiyo haya, mkoa uliokuwa kinara
sasa unaburuza mkia!
Akitokea mtu
kwenye jamii ya Wahaya akatoa wazo lenye manufaa kwa jamii nzima ni nadra sana
wazo hilo kuungwa mkono wala kukubalika.
Imani iliyozoeleka ni ya kwamba mtoa wazo ataringa iwapo wazo lake litaleta
mafanikio. Kwahiyo ili kumkomoa, bila kuelewa kuwa wanajikomoa wenyewe,
watalipinga wazo hilo kwa nguvu zao zote. Mambo yatalala doro, watabaki kwenye
shida ileile ilmradi wasionekane wamemnufaisha aliyetoa wazo la kuimaliza shida
inayoleta usumbufu.
Jambo
lililotokea kuwa maarufu sana kwa akina “nshomile” ni kwamba pakitokea mtu
akapata nafasi ya juu atahakikisha chini yake anapajaza na watu wa jamii yake,
lengo si kuwainua, atahakikisha wanabaki hapo muda wote wa uhai wake, ili aweze
kuwapata watu wa kumsujudia kwa gharama raihisi. Wasiolielewa tatizo hilo
wanawachukulia watu hao kuwa wanajipendelea na wana ukabila!
Kwa ufupi ni
kwamba kwa kiasi kikubwa maendeleo ya mkoa wa Kagera yamerudishwa nyuma na
hulka hizo za ajabu za wakazi wa mkoa huo. Kwahiyo mtu wa kuusaidia mkoa huo ni
lazima kwanza atafute namna ya kuwashawishi wakazi wa mkoa huo wajaribu
kubadili tabia na mitazamo yao, hasa tabia ya “kantamuhira” neno lenye maana ya
sitaki niungue kwa ajili yake, neno
linaloleta maana ya kuwa na roho ya korosho.
Nimeyasema haya
kwa nia njema kabisa ili Kamanda Massawe aweze kulijua tatizo lililojificha na
kutafuta namna ya kulipatia tiba, kama kweli amedhamiria kuuona mkoa wa Kagera
unainuka tena na kurudi kwenye ushindani wa kimaendeleo na mkoa wa Kilimanjaro
kama ilivyokuwa tangu zamani. Maana Waswahili walisema kwamba mficha maradhi…..msomaji
utamalizia mwenyewe.
Tahadhari
yangu kwa Kamanda Massawe ni kwamba katika uchapaji kazi wake aiache demokrasia
ichukue mkondo wake. Historia inatuonyesha kwamba wote waliojaribu kutumia
uchapaji kazi wao kama kishawishi cha kuichokonoa demokrasia waliishia
kuangamia bila kupewa shukurani yoyote kwa mambo mazuri waliyokuwa wameyatenda.
Nimalizie
kwa kueleza kiini cha matumaini niliyonayo kwa Kamanda Massawe. Nimemfahamu Kanali Fabian
Massawe tangu akiwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee iliyo chini ya
Jeshi la Kujenga Taifa, Mgulani, Jijini Dar es salaam. Mafanikio aliyoyaonesha
katika shule hiyo, kutoka shule changa hadi
kufikia kuwa shule ya kuchuan na shule kongwe za Jijini Dar es salaam na katika taifa
kwa ujumla, ni mafanikio yasiyo ya kubeza. Ni mafanikio hayo yanayonipa imani
kuwa hata kule Kagera ataweza.
Wahaya
wanasema “ebitagira mahyo tibyera”, ndiyo maana hata mimi nataka nimshukuru
Kamanda Massawe kwa lugha yake, “Eka Massawe saa”. Najua kule Bukoba watakuwa
wanamuita Mangi kama tulivyozoea kuwaita wanaume wa Kichagga kote tunapowaona.
0784 989 512