Bukobawadau

[ VIDEO]Hati za Muungano mvurugano, Kauli ya Nahodha yapingana na ya Katibu wa Bunge

Dodoma. Utata umezidi kuibuka katika Bunge Maalumu la Katiba kutokana na kutopatikana kwa hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ile ya Sheria ya Baraza la Mapinduzi ya kuridhia Mkataba wa Muungano.
Utata huo, umebainika katika Kamati kadhaa siku moja tangu wajumbe wa Bunge hilo waanze kujadili sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba, zinazohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wake.
Jana Kamati namba 2 ilimwalika, Spika Mstaafu wa Bunge la Muungano, Pius Msekwa kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo, lakini uhalali wa saini zake uliibua malumbano makali. Msekwa aliitwa kutokana na kwamba ndiye aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati huo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha, alithibitisha kutokea utata huo na kwamba walilazimika kumuita Msekwa ili kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa.
Nahodha alisema kwa maelezo ya Msekwa, inaonekana hati ya Muungano ipo Umoja wa Mataifa (UN), kwani kabla ya Muungano, Tanganyika ilikuwa na kiti chake UN na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar hali kadhalika.
Nahodha alisema baada ya UN kuomba uthibitisho wa Muungano, ndipo walipelekewa hati hiyo na kwamba haijawahi kurejeshwa.
Kauli hiyo ya Nahodha inapingana na kauli ya Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Hamis Hamad ambaye jana alisema hati hiyo ipo Dar es Salaam na ni moja tu, hivyo siyo rahisi kuipeleka bungeni Dodoma.
“Ile hati ya Muungano ipo Dar es Salaam, lakini tunahofia kuileta maana inaweza kupotea kwani ipo moja tu, sasa ambacho tutakifanya inaweza kutolewa nakala na kuthibitishwa na mawakili na ikaja nakala hapa Dodoma iwapo wajumbe wanahitaji,” alisema Hamad.
Nahodha alipoelezwa juu ya majibu ya Katibu wa Bunge kuwa hati hiyo ipo Dar es Salaam, alishikwa na mshangao na kusema wanamuomba Katibu huyo, aiwasilishe kama ipo.
Sheria za Muungano
Katika hatua nyingine, Sheria Namba 22 ya 1964 ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar kuridhia Muungano nayo haijulikani ilipo.
Baadhi ya wajumbe katika Kamati Namba 2 walidokeza kuwa, walipohoji kuhusu sheria hiyo walisomewa kitabu cha aliyewahi kuwa Mwanasheria wa Zanzibar, Abdul Jumbe na kuambiwa kwamba picha za ukumbusho zipo.
Nahodha ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, alikiri kuwa hata yeye hajawahi kuona sheria hiyo.
“Kwa Bunge la Tanganyika ushahidi tumeletewa hapa kuwa waliridhia Aprili 25, 1964 na waliosaini ni Julius Nyerere, Katibu wa Bunge hilo, Pius Msekwa na aliyekuwa Spika Adam Sapi Mkwawa, lakini kwa Zanzibar haupo,” alisema na kuongeza:
“Mimi nilikuwa mtendaji mkuu wa SMZ nilipaswa kujua, lakini nisingeweza tu kuanza kutafuta sheria, sheria ambazo zimetungwa Zanzibar ni nyingi, kwani ingeniwia kazi kubwa sana kuipata hati hii kwani msimamizi wake ni Ofisi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Ofisi ya Rais”.
Alisema Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman pia alisema hajawahi kuiona sheria hiyo.
Utata wa saini
Kuhusu utata wa saini za Nyerere na Msekwa kwenye hati hizo, Nahodha alisema yeye siyo mtaalamu wa maandishi kubaini kuwa hati hizo na saini zake ni halali au la.
Hata hivyo, alisema Msekwa alikiri kwenye kamati hiyo kuwa saini iliyopo kwenye hati ya makubaliano ya Muungano ni yake.
Utata wa saini za Msekwa uliibuliwa na baadhi ya wajumbe ambao walihoji tofauti baina saini iliyopo kwenye sheria hati ya muungano na saini zake katika nyaraka nyingine rasmi.
Wajumbe waliombana Msekwa wakiongozwa na Godbless Lema, pia walitilia shaka matumizi ya kompyuta katika sheria hizo zilizoandikwa mwaka 1964.
“Mwaka 1964 hakukuwa na kompyuta lakini hapa tunaona sheria zimeandikwa kwa kompyuta na hata sehemu ya saini ya Msekwa na Nyerere kuna herufi zimeandikwa kwa kompyuta,” alinukuliwa Lema.
Katika maelezo yake Msekwa licha ya kukiri upungufu, aliwakumbusha wajumbe kuwa siku ya kusainiwa hati hizo, picha zilipigwa na zipo hadi sasa.
Jana jioni kamati zilianza kupigia kura sura ya kwanza, na Mwenyekiti wa Kamati Namba 5, Hamad Rashid Mohamed alithibitisha kuwa asilimia 90 ya wajumbe wa kamati yake walipiga kura za wazi kupitisha ibara za sura ya kwanza.
Alisema ibara ya 1(1) ilikubaliwa na wajumbe wa kamati hiyo kwa kupata theluthi mbili ya kura kwa upande zote, lakini katika ibara hiyo sehemu ya pili (2), haikuungwa mkono baada ya kukosa theluthi mbili kwa pande zote za Muungano.
Kifungu hicho kinatamka kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi na shirikisho lenye mamlaka kamili ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya hati ya Makubaliano ya Muungano ya Mwaka 1964 zilikuwa nchi huru.
Hamad alisema ibara nyingine zilizokosa theluthi mbili kwa Tanzania Bara na Zanzibar ni pamoja na ibara ya 2, 5 na saba. Katika Sura ya kwanza yenye ibara tisa ni tano tu zilizokubaliwa na kamati yake.
Hamad alisema wanatarajia kukutana na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta kuangalia jinsi ya kutengua kanuni ili kuongeza muda wa majadiliano kwenye ibara ya sita ambayo wameanza kuifanyia kazi jana jioni.
Hali katika kamati nyingine tatu, ambazo wenyeviti wake hawajatoa taarifa rasmi bado, mabadiliko ya kifungu hicho yamekosa kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe Zanzibar, huku katika kamati moja kifungu hicho kikikosa kuungwa mkono na theluthi mbili ya pande mbili za Muungano.
MWANANCHI.

Next Post Previous Post
Bukobawadau