WANAOPINGA RASIMU YA KATIBA MPYA WANAMKANA JK
Na Prudence Karugendo
MWANZONI kabisa alipoingia madarakani, Rais Jakaya
Kikwete, alisema wazi kwamba jambo moja kubwa lililokuwa likisumbua kichwa
chake ni kero zilizokuwa zikijitokeza kwenye Muungano wa Tanzania. Na kwa vile
alikuwa amechaguliwa kuiongoza Tanzania ni wazi kwamba asingependa kuiongoza
nchi yenye ugonjwa unaotishia uhai wake, uhai wa nchi aliyopewa kuiongoza.
Kwahiyo
akaahidi kwamba kutokana na nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa nchi aliyopewa
na wananchi angejitahidi kadiri ya uwezo wake kuzitatua na kuzimaliza kero hizo
zilizokuwa zikijitokeza kwenye Muungano. Hiyo ilikuwa ahadi ya kwanza na muhimu
ya rais aliyekuwa ameingia madarakani.
Sasa rais
anataka kukitimiza alichokiahidi chama chake kinamshika shati! Ni maajabu na
kweli!
Kwa sasa
kuna mchakato wa kuipata Katiba mpya ya nchi. Lakini ikumbukwe kuwa chama
tawala, Chama Cha Mapinduzi, ambacho rais wetu ni mwenyekiti wake, hakikuwa
kabisa na wazo la Katiba mpya. Hilo ni wazo la wapinzani ambao walipojaribu
kulieleza Bungeni walichezewa mduara na wabunge wa CCM walio karibu robo tatu
ya wabunge wote, ingawa wingi wao hauwiani kabisa na manufaa yao kwa wananchi.
Kuona hivyo
wapinzani wakalichomoa wazo lao Bungeni na kulipeleka Ikulu kwa rais. Rais
akaona mantiki yao, wazo la wapinzani likamkumbusha kero alizoahidi kuzishughulikia.
Na kwa vile yeye ni rais wa watu wote, wakiwemo wapinzani, kinyume na mawazo ya
wachache wanaomchukulia kama rais wa chama chake, akawaahidi wapinzani
kuanzisha mchakato wa kuipata Katiba mpya.
Mpaka hapo
tutaona kwamba rais alikuwa nalo wazo la Katiba mpya tofauti na fikira za
wasaidizi wake na wapambe wa chama chake. Sababu bila hivyo ni vigumu mtu
kukiridhia kitu ambacho haoni mantiki yake, na ikizingatiwa mtu mwenyewe ni
rais aliye na mamlaka yasiyopimika wala kupingika katika jamii yake.
Kwahiyo JK
akaunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akamteua Jaji Joseph Sinde Warioba pamoja
na wajumbe wake, akawaapisha na kuwakabidhi kazi hiyo ya kuanzisha mchakato wa
kuitafuta Katiba mpya.
Msisitizo ni
kwamba kitendo cha rais kuwaapisha mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kinaleta maana ya kwamba watu hao wanaenda kufanya kazi kwa niaba
yake. Yoyote yanayokuwemo kwenye kazi wanayoenda kuifanya, yawe mazuri au
mabaya, wa kuwajibika ni rais mwenyewe.
Kazi hiyo ya
Tume ya Warioba ikafanyika kiungwana, kiumakini na kitaalamu mpaka ikakamilika.
Ikaletwa na kukabidhiwa kwa Rais Kikwete. Rais akaipitia na kuridhika nayo.
Tarehe 22 / 1 / 2014, akaitia mkono, sahihi, ili iwe Rasimu, akaunda Bunge
Maalumu la Katiba ili Rasimu hiyo ikawasilishwe kwenye Bunge hilo kusudi
likaichambue na kutengeneza Katiba mpya kabla ya Katiba hiyo kuletwa kwa
wananchi wakaipigie kura ya kuikataa au kuikubali.
Kwa ufupi ni
kwamba JK asingekubali kuisaini Ripoti ya Warioba iwe Rasimu kama
asingekubaliana nayo au kuyaona mapungufu makubwa ndani yake. Ni lazima
angemueleza Warioba ayarekebishe mapungufu kwanza, au kwa mamlaka yake,
kuivunja Tume hiyo na kuunda nyingine. Izingatiwe kwamba ile ni Tume yake Rais
iliyokuwa ikifanya kazi kwa niaba yake.
Kwa maana
hiyo siamini kabisa kwamba hotuba aliyoitoa JK Bungeni, iliyopaswa kuwa ya
uzinduzi wa Bunge Maalumu la Katiba, lakini ikageuka kuwa ya kuichambua Rasimu,
ilitokana na dhamira ya kweli ya rais. Dukuduku langu hilo linatokana na
mlolongo mzima nilioueleza hapo juu kuhusiana na mchakato huu wa kuipata Katiba
mpya.
Baada ya
hapo wajumbe wa Bunge Maalumu wa upande wa CCM wakaanza kuonyesha wasiwasi wao
kuhusu Rasimu hiyo kabla ya hata kuanza kuichambua! Ikaonekana Rasimu hiyo
haionyeshi mustakabali mwema kwa chama chao!
Hivyo
wakaanza kuandaa mikakati ya kuishughulikia Rasimu hiyo huku wakionekana
kumshambulia waziwazi Jaji Warioba kwamba ni kama ameileta makusudi Rasimu hiyo
kama mbinu ya kukiangamiza chama chao!
Wanaosema hivyo
hawayatilii kabisa maanani mambo kama haya; kwamba baadhi yao hawaijui CCM wala
kuipenda kufikia hata robo ya Jaji Warioba, kwamba alichokiwasilisha Warioba
sio mawazo yake bali ya wananchi kama
alivyoelekezwa na rais, kwamba anachokitaka Warioba ni kuiona CCM iliyokomaa na
kuacha kutegemea kubebwa na nguvu za dola na badala yake chama hicho
kijitegemee chenyewe kama vinavyofanya vyama vingine.
Mwisho
kabisa Warioba anaupenda Muungano, ni kwa vile anauelewa kuliko wajumbe wengi
wa CCM wanaomshambulia kiushabiki wakiwa wameyaweka mbele maslahi yao binafsi
ndani ya muungano huo wakikitegemea chama chao kuyapata wanayoyataka, wakiwa wameyatelekeza maslahi ya nchi hasa ya
Muungano.
Tatizo
ambalo hata mimi naliona kwa hapa ni la baadhi ya wananchi kuupenda Muungano
kwa vile unalinda maslahi yao binafsi bila ya kujali ni namna gani Muungano huo
unalinda maslahi yake wenyewe.
Ikumbukwe
Muungano ndio unaozaa jina la Tanzania, kwa maana hiyo ukishaondoa neno Zanzibar
unachobaki nacho sio Tanzania Bara kama ilivyozoeleka kwa sasa, bali
kinachobaki ni Tanganyika. Sababu neno TanZania ni muunganisho wa majina mawili
ya Tanganyika na Zanzibar.
Haiwezekani
ukaicha Zanzibar ikajitambua kwa rais wake, Katiba yake, bendera yake, Wimbo wake wa Taifa,
Bunge lake, Baraza lake la mawaziri nakadhalika, halafu Muungano wenyewe
ukabaki imara, ni lazima utayumba na baadaye kutoweka.
Hicho ndicho
alichokisisitiza Jaji Warioba, kwamba ili Muungano usiyumbe hapanabudi
ukaitambua pia Tanganyika katika kujiwekea uwiano wake. Vinginevyo ukiendelea
kuelemea upande mmoja matokeo yake utapinduka na kuzama kama MV Bukoba. Na
katika kuzama hakuna heri yoyote.
Hizo ni kero
zilizomo kwenye Muungano alizoziona Rais Kikwete na kusema jinsi zinavyomsumbua
kichwa chake, hivyo akaahidi kuzishughulikia.
Kwahiyo
wajumbe wanaodhani wanamshambulia Warioba waelewe wazi kuwa wanamshambulia na
kumkana JK. Sababu kazi ya Warioba haikutokana na dhamira yake mwenyewe, hiyo
ni kazi iliyokuwa kwenye dhamira ya Rais Kikwete, Warioba ni msaidizi tu.
Muungano wa
Tanzania unapaswa usimame kwenye umakini huku zikijengwa hoja murua za
kuulinda, hauwezi kulindwa na viroja.
Viroja ni
kama hivi; wapo wanaosema kwamba
muungano wa miaka 50 utavunjikaje leo? Huku wengine wakisema kwamba asilimia
kubwa ya Watanzania wa leo wamezaliwa baada ya Muungano kwahiyo eti hawaijui
Tanganyika!
Kusema
ukweli hapo sioni hoja yoyote ya kuulinda Muungano zaidi ya kuuchimbia kaburi.
Scotland na
Uingereza ziliungana mwaka 1707, zaidi ya miaka 300 iliyopita, lakini leo hii
nchi hizo zinaongelea kutengana kiustaarabu. Mbona umri wa muungano wa nchi hizo
haujawa kikwazo kwa mazungumzo hayo ya kutengana? Ila umri wa muungano wetu,
ambao ni zaidi ya mara 6 ya muungano wa Scotland na Uingereza, ndio uonekane
mhimili wa kuulinda muungano wetu!
Kitu kingine
ni kwamba Mwalimu Nyerere kazaliwa enzi za wakoloni, hakuwahi kusoma wala
kufundishwa kokote juu ya nchi iliyoitwa Tanganyika huru na baadaye ikatawaliwa
na wakoloni, lakini mbona hiyo haikumzuia kuongoza harakati za kuudai uhuru wa
Tanganyika?
Sasa iweje
wananchi wa Tanzania waliozaliwa baada ya Muungano wakasoma historia ya
Muungano huo na Tanganyika iliyokuwa huru, wakose kuielewa Tanganyika? Na
watashindwaje kuyahoji mambo ambayo wanaoona hayakwenda sawa wakati wa kuziunganisha
hizi nchi mbili?
Mwisho ni
kwamba kuna hadithi ya Waingereza inayosema juu ya mtu anayeliwa na dubu, eti
mtu akiliwa na dubu na huyo mnyama akaendelea kuishi mzuka wa marehemu
aliyeliwa utabaki ukiwasumbua jamaa zake mpaka dubu huyo atakapokufa.
Ndivyo
ilivyo kwa mzuka wa Tanganyika. Mzuka huo unasababishwa na uwepo wa Zanzibar.
Mzuka huo hauwezi kupotea hata baada ya miaka milioni moja kama Zanzibar
inaendelea kujitambua.
Tukiangalia
miaka ya 1960 mwishoni mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1970, tutaona kwamba mzuka
wa Tanganyika ulikuwa umetulia pamoja na kwamba ulikuwa muda mfupi tangu nchi
hizi ziungane, sababu ni kwamba kilichokuwa kikitumika sana ni Tanzania
Visiwani na Tanzania Bara. Neno Zanzibar lilibaki kutumika kama jina la mji tu
basi.
Kwahiyo
inapoandikwa Katiba mpya mambo hayo hayanabudi kuwekwa maanani, kama kweli
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wamekidhamiria wanachokifanya. Kumsuta Jaji
Warioba hakufai, sababu wanaofanya hivyo watajikuta wanajisuta wenyewe au
wakimsuta wanayedhani wanamfurahisha.
0784 989 512