Bukobawadau

WATATU WANASWA NA KILO 8 ZA ‘UNGA’

Dar es Salaam. Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, kimewakamata watu watatu katika matukio tofauti wakituhumiwa kukutwa na kilo 8.6 za dawa za kulevya zilizowekwa kwenye mabegi la nguo.
Watuhumiwa hao walikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam (JNIA).
Kati yao, wawili walikutwa na dawa kulevya aina ya cocaine na mmoja akiwa na malighafi ya kutengeneza dawa za kulevya aina ya Ephedrine.
Akizungumza jana, Kamanda wa kitengo hicho, Godfrey Nzowa alisema Machi 28, mwaka huu saa 5 asubuhi, Mkazi wa Mbezi Mwisho, Taric Barajashi (30) alikamatwa kwenye uwanja huo akiwa na kilo nne za malighafi hiyo.
Katika mahojiano, Nzowa alisema mtuhumiwa alikiri alikuwa anazisafirisha kwenda Afrika Kusini ambako kuna kiwanda cha kutengeneza dawa za kulevya.
“Alidai kuna kiwanda nchini Afrika Kusini kinachotengeneza dawa za kulevya. Malighafi hizi ni kama zile alizokamatwa nazo msanii, Agness Masogange,” alisema Nzowa. Kamanda Nzowa alisema pia kuwa, mtuhumiwa alikiri kufanya safari zaidi ya mara mbili nchini humo.
Alisema walifanikiwa kumtia nguvuni kijana huyo baada ya kupata taarifa za kitelijensia.
Katika tukio jingine, Mkazi wa Magomeni Mapipa, Agness Musa (22) alikamatwa JNIA Machi 30, mwaka huu saa 8:30 usiku akiwa kilo moja ya cocaine akitaka kwenda Uturuki kwa ndege ya shirika la ndege ya nchi hiyo.
Kamanda Nzowa alisema mtuhumiwa akiwa na hati ya kusafiria ya Tanzania, alitiliwa shaka na polisi wa JNIA na walipomhoji walibaini kuwa alificha dawa hizo kwenye begi lake la nguo.
Machi 31, 2014 saa 8:05 usiku, polisi hao walimkamata Mkazi wa Mbezi Mwisho, Pamela Kibaya akiwa na kilo 3.6 za Cocaine.
Januari 31 mwaka huu, raia wa Kenya anayeishi Mombasa, AbdulRahman Salim, alikamatwa JNIA akiwa na kete 141 za dawa za kulevya aina ya cocaine zenye thamani zaidi ya Sh119 milioni.
Februari 4 mwaka huu, watu 12 wanaodaiwa kuwa ni raia wa Iran na Pakistan walikamatwa na shehena kubwa ya dawa za kulevya, kilo 201 aina ya heroine katika Bahari ya Hindi wakiwa wanaelekea Zanzibar kwa jahazi.
MWANANCHI.
Next Post Previous Post
Bukobawadau