MCHAKATO WA KATIBA MPYA:Ya Kaizari yanapochanganywa na ya Mungu!
Na Bernard Kazinduki
MCHAKATO wa Katiba Mpya unaonekana kuingiliwa kwa nguvu
na wasiopaswa kuuingilia. Tena wanauingilia kwa mtindo wa kuhatarisha
mustakabali wa nchi yetu. Maaskofu 32 wa
Kikristo wameuingilia mchakato huo kwa
kutumia mamlaka walio nayo ya uongozi wa kiroho na kutaka kuwafanya wananchi waamue kulingana na maelekezo
yao hao viongozi wa kiroho.
Maaskofu hao
wanafanya hivyo wakiwa wameyasahau maelekezo muhimu ya aliye muhimili wa imani
yao, aliyewafanya wakaabudu kwa jina lake, yaani kujiita Wakristo, Yesu Kristo
mwenyewe.
Katika
kuepusha mgongano wa mamlaka, mgongano wa mamlaka ya kidunia na ya Kimungu,
Kristo alishauri kwamba ya Kaizari mpeni Kaizari na ya Mungu mpeni Mungu. Kwa
kauli hiyo tayari Kristo alikuwa ametenganisha mambo ya Mungu, kiimani, na
masuala ya mamlaka ya kidunia. Alitenganisha dini na siasa.
Kristo
hakutaka watu wavunje sheria za kidunia kwa kisingizio cha imani ya kumtii
Mungu. Sababu hata Mungu anataka mamlaka halali ya kidunia yaheshimiwe, walio
na utiifu kwa mamlaka ya kidunia ndio walio katika mwelekeo wa kumtii yeye
Mungu.
Ipo mifano
mingi inavyoonyesha kwamba Mungu anawataka waja wake wayatii mamlaka ya kidunia.
Mfano mmojawapo ni wa mfalme wa Uganda, Kabaka Mwanga wa Pili. Kabaka huyo aliwakataza watu wake kufuata mafundisho ya
imani za kigeni, lakini baadhi ya watu walikaidi wakaendelea kufuata mafundisho
hayo ya imani za kigeni.
Alipowakamata
wasaliti hao wa amri yake, hasa wale 22 waliokuwa wahudumu wa Ikulu, akawachoma moto na wengine
kuwakaanga kwa mafuta ya kula kama “kiti moto” huku akisema kwamba kama Mungu
yupo wanayefundishwa na wazungu basi na aje auzime moto huo.
Mungu
hakuuzima moto huo, watu hao waliungua na kufa. Mimi naamini kwamba Mungu
hakushindwa kuuzima moto huo ila alitaka ya Kaizari apewe Kaizari na ya kwake
apewe yeye. Ni wazi kwamba Mungu hakufurahishwa na ukaidi wa watu hao kwa
kiongozi wao wa kimwili.
Nchi yetu ya
Tanzania muda wote imekuwa na amani tangu ilipopata Uhuru wake ikiwa Tanganyika
na baada ya kuungana na Zanzibar kuwa Tanzania. Kilichoifanya amani ikatamalaki
muda wote, zaidi ya miaka 50 sasa, pamoja na mambo mengine, ni hekima ya
viongozi wake ya kutochanganya mambo ya Mungu na ya kidunia. Kwahiyo sidhani
kama Kristo alikosea kutowataka watu kuchukua yaliyo ya Kaizari na kumpa Mungu.
Alijua kwamba kwa kufanya hivyo ni lazima kungetokea mtafaruku katika jamii.
Katika
mchakato huu wa kutafuta Katiba Mpya ya nchi yetu, yawezekana kweli maoni ya
wananchi walio wengi kuhusu muundo wa Muungano wetu yakawa ni kuwa na serikali
tatu. Lakini hiyo haitoshi kuufanya muundo wa muungano wetu uwe wa serikali
tatu, ni lazima iangaliwe pia hali hiyo ya wananchi kutamani kitu ambacho
kinaonekana si salama kwao inatokana na nini. Inawezekana watu walio wengi
wakawa wamepatwa na dhambi ya ubaguzi.
Dhambi ya
kwamba “wao Wazanzibari sisi Watanganyika”. Dhambi hiyo ni ya hatari kabisa, na
kama alivyosema Baba wa Taifa, dhambi hiyo inatafuna pale inapokumbatiwa. Kwa
nini maaskofu wetu hao wanashindwa kuliona hilo?
Kusema
kwamba maoni ya walio wengi yaheshimiwe bila kutumia hekima ya kuangalia ni
maoni ya aina gani ni uzembe mkubwa kiuongozi. Ikumbukwe jinsi Watanzania
asilimia 82 walivyotaka mfumo wa chama
kimoja cha siasa uendelee hapa nchini lakini hekima za Baba wa Taifa
zikaonyesha kwamba pamoja na mambo kuwa hivyo mfumo vyama vingi hakuwa na
sababu yoyote ya kuzuilika. Hivyo asilimia 18 ikaishinda asilimia 82!
Muundo wa
serikali tatu katika Muungano wetu utajenga ubaguzi wa kuwaona Wazanzibari kama
sio wenzetu. Ni tofauti na ilivyo kwa sasa, tunawaona Wazanzibari kama wenzetu wakati wao wanaendelea kuwa na
serikali yao ya Zanzibar. Hiyo ni kwa sababu kwa idadi yao ilivyo hakuna
uwezekano wowote wa kwamba wanaweza kuimeza idadi kubwa ya Watanganyika.
Lakini
tukisema tuwe na serikali moja, kwa maana ya kuwa na Tanzania tu bila serikali
ya Zanzibar, uwezekano wa Wanzibari kumezwa katika muungano wa aina hiyo ni
mkubwa sana, sababu idadi yao ni ndogo. Hicho ni kitu ambacho hakuna anayekitamani, awe Mzanzibari au
Mtanganyika. Sasa kama asilimia 18 iliishinda asilimia 82 katika mfumo wa vyama
vya siasa, kwa nini asilimia zaidi ya 40
ionekane imekufuru kwa kuishinda asilimia iliyo chini ya 60 katika muundo wa
muungano?
Lakini
kuiacha Zanzibar iwe na serikali yake huku Tanganyika nayo ikiwa na serikali
yake katika muundo wa serikali tatu uwezekano wa kutafunwa na dhambi ya
ubaguzi, wao Wazanzibari sisi Watanganyika, ni mkubwa sana. Na tusije tukasahau
kwamba Baba wa Taifa alishautolea radhi ubaguzi wa aina hiyo.
Viongozi hao
wa kidini kwa nini hawataki kujifunza kutoka kwa viongozi wenzao wa kidini
katika nchi ya Rwanda? Katika nchi hiyo ya Rwanda viongozi wa kidini, mapadri
na maaskofu, waliichochea dhambi ya ubaguzi wakionyesha kwamba wao Watutsi na
sisi Wahutu, matokeo yake ni mauaji ya kimbari yaliyoitetemesha dunia nzima.
Ni kwa
mantiki hiyo nashindwa kuyatilia maanani maoni ya maaskofu hao 32 ya kwamba
maoni ya wananchi ya serikali tatu yaheshimiwe. Sababu viongozi wenye hekima hawapaswi kufuata
tu idadi bali hekima vilevile. Sidhani kama wakija ibilisi watatu askofu
atalazimika kukubaliana nao kwa kuheshimu wingi wao na kumuacha malaika mmoja
kwa vile yuko peke yake.
Kwa maana
hiyo tunapaswa kuangalia mantiki ya kitu imekaaje bila kujali wingi wa watu
wanaokitaka. Tusikurupuke kukitamani kitu kinachoonyesha kitatupeleka kwenye
maangamizi kwa kuangalia tu wingi wa wanaokitamani.
Kwahiyo
katika hili ni vema tukaeleweshana uzuri na ubaya wa tunachokiongelea bila
kugombana wala kutukanana. Viongozi wetu wa kiroho inabidi nao tuwasahihishe
kiungwana pale tunapoona wamejisahau na kukifanya kitu kilicho kinyume na
mafundisho ya kiroho wanayopaswa kuyafuata.
Kristo
aliposema kwamba ya Kaizari apewe Kaizari na ya Mungu apewe Mungu, alikuwa na
maana kubwa. Kikubwa alichokilenga ni kutogonganisha mambo ya kiroho na yale ya kimwili. Kwahiyo maaskofu wetu hao wanapaswa
kuuzingatia ushauri huo wa Kristo.
MUNGU
IBARIKI TANZANIA