Bukobawadau

MKUU WA POLISI KANYIGO AFA AJALINI

MKUU wa Kituo cha Polisi cha Kanyigo, Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera, D 6192 SGT Rajabu (47), amefariki dunia baada ya gari alilokuwa akiendesha kugongana  gari la abiria, maeneo ya Kyakailabwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga, alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea Mei 12, saa 3 asubuhi katika barabara ya Uganda, maeneo ya Kyakailabwa.
Alisema askari huyo akitokea maeneo ya Katoma kuelekea Bukoba Mjini akiwa anaendesha gari T 954 AVV Toyota Mark II, aligongana na gari la abiria T 660 CEM Toyota Hiace lililokuwa likiendeshwa na Wilsson Ishengoma (40), mkazi wa Nyakanyasi, Bukoba mjini.
Alisema katika ajali hiyo SGT Rajabu aliumia sehemu za tumboni, hivyo madaktari walimfanyia upasuaji na kugundua bandama yake ilikuwa imepasuka na damu nyingi zilikuwa zimevujia tumboni.
Alisema kuwa askari huyo alifariki dunia saa nane usiku baada ya kufanyiwa upasuaji huo.
“Chanzo cha ajali ni hali ya hewa baada ya  kioo cha gari la marehemu kupata ukungu, aliamua kufuta kioo wakati  akiendelea  ndipo gari lilihama  na kwenda kugonga  Hiace ya abiria na usukani wa gari yake ulimbana kifuani,” alisema. Mwili wa marehemu umesafirishwa Singida kwa mazishi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau