Bukobawadau

SERIKALI KUPELEKA MSAADA KIJIJINI BULEMBO-KAMACHUMU

 HATIMAYE serikali imesikia kilio cha wanakijiji wa Bulembo, Tarafa ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera na kuahidi kutoa msaada wa sh milioni 170 ili kunusuru wananchi waliopigwa na upepo ulioezua nyumba zaidi ya 200 na kuharibu mazao ya kaya zipatazo 305 takriban mwezi mmoja uliopita.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa msaada huo utatolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa baada ya kelele zilizopigwa na wadau mbalimbali, likiwamo gazeti hili kwa nyakati mbalimbali.
Miongoni mwa wadau walioguswa na kupigania wanakijiji hao ni Mhariri Mtendaji wa gazeti hili, ambaye pia ni mkazi wa Bulembo, Ansbert Ngurumo.

Kwa wiki mbili mfululizo, Ngurumo ametumia vyombo vya habari – Tanzania Daima, Nipashe, ITV, RFA, Kasibante Redio, Radio Vision na mitandao kadhaa ya mawasiliano – kuomba serikali iende Bulembo kunusuru uhai wa wananchi hao.
Vilevile amekuwa anahamasisha wafanyabiashara, wanasiasa na watu wenye moyo wa kusaidia, kuelekeza misaada Bulembo.

 Akizungumza na wanakijiji hao juzi, Ngurumo alisema serikali inatarajia kutoa tani 160.8 za mahindi, sh milioni 60.3 kwa ajili ya kununulia maharage, sh milioni 7.7 kwa ajili ya kuezeka Shule ya Msingi Rugongo na sh milioni 26.5 kwa ajili ya kusafirisha chakula hicho.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Anterius Sosthenes, bajeti ya ukarabati wa shule hiyo ni sh milioni 18.5.
Ngurumo alitumia fursa hiyo kushukuru wadau wote waliosaidia kusukuma serikali itoe mchango huo, akiwamo mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage, ambaye hajafika Bulembo tangu walipopigwa na kimbunga japo amekuwa akipiga simu huku na kule kuomba misaada.

Wananchi wa Bulembo na vijiji jirani wamekuwa wanamlalamikia mbunge wao kutofika kwa wakati au kutoa msaada kwao, lakini watu wake wa karibu wanamtetea kuwa amesaidia kwa kutumia njia nyingine.


Mwijage aliueleza mtandao wa Friend of Bukoba (FoB) mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba amekuwa anapambana na serikali kwa ajili ya wanavijiji wa Bulembo na Mafumbo, akasema serikali imeshakubali kutoa msaada huo.
Mmoja wa wadau waliofika Bulembo juzi, Salehe Mashaka, alisema ni vema viongozi na wawakilishi wa wananchi wawe mfano wa kuigwa kwa kuguswa na matatizo ya wananchi, hata ikibidi waahirishe shughuli zao maafa yanapotokea ili kuwafariji wananchi wao.

“Juzi juzi tulisikia Waziri Mkuu, Waziri wa Ujenzi na viongozi wengine wakiongozana kukagua maeneo na kufariji waathirika wa mafuriko ya Dar es Salaam. Waliondoka bungeni Dodoma wakaenda Dar es Salaam, wabunge wengine wameshafika hapa Bulembo. Mbunge wetu yuko wapi? Yeye ana kazi nzito kuliko wenzake?” alihoji.

Ngurumo aliwashukuru wabunge wawili waliofika Bulembo kwa nyakati tofauti na kutoa msaada. Mbunge wa Muleba Kusini, Prof. Anna Tibaijuka, ambaye alitoa tani moja na kilo 125 za maharage na Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamulaza (CHADEMA) aliyetoa tani moja na kilo 100 za mchele, sawa na kiwango alichotoa Ngurumo wiki moja na nusu iliyopita.

Alishukuru pia mashirika kadhaa yakiwamo, Msalaba Mwekundu, Kolping, makanisa na makundi kadhaa ambayo yameshafika Bulembo kusaidia wananchi hao. Aliomba wengine wajitokeze kuunga mkono wananchi wenzao hadi serikali itakapokuwa imefikisha msaada huo kijijini hapo.
Hata hivyo, Ngurumo alitoa tahadhari kwamba wananchi wanapaswa kuwa macho ili msaada huo usichakachuliwe na wajanja, maana hata katika misaada iliyotangulia, zimekuwapo lawama kwamba viongozi wa serikali wamekuwa wakichakachua.

Alisema alishangaa pia kusikia kwamba wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba wasio wana UKAWA walichanga sh milioni 40 kusaidia wananchi wa Dar es Salaam walioathirika kwa mafuriko wiki mbili baada ya maafa ya Bulembo, huku wakiwasahau kabisa wanakijiji hao walioathirika mapema.

Akizungumzia msaada aliotoa juzi, Rwamlaza alisema anajua kuwa chakula hicho hakiwezi kutimiza mahitaji ya wananchi wote, lakini ameguswa na taarifa za maafa hayo, na kutoa kidogo alichonacho.

“Nimesikitika sana kuona serikali imekaa kimya, imeweza kutoa msaada Dar es Salaam na kujenga madaraja haraka; huu ni ubaguzi kwa watu wa Muleba,” alisema Rwamlaza.
Alisema inawezekana viongozi wa wilaya na mkoa hawajapeleka taarifa sahihi za maafa hayo kwenye ngazi za juu zinazohusika na maafa, ndiyo maana serikali imechelewa kutoa msaada.
Alionya pia kwamba msaada unaotoka Ofisi ya Waziri Mkuu si hisani bali ni wajibu wa serikali, kwani ni fedha zinazotokana na kodi zao, hivyo wasitokee wanasiasa na kujipiga kifua kwa malengo ya kujinadi kwamba ndio wametoa msaada huo.

Rwamulaza alitoa kauli hiyo baada ya taarifa kuzagaa kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanafanya jitihada kugeuza msaada wa serikali kuwa ni mchango wa chama chao kwa wananchi wa Bulembo na Mafumbo.
Next Post Previous Post
Bukobawadau