Bukobawadau

WENYEVITI WA VIJIJI BUKOBA WAPIGWA 'STOP'

 WENYEVITI wa vijiji na vitongoji katika Halmashauri ya Bukoba wamezuiwa kugawa au kuuza ardhi kwa wananchi kinyume na sheria.
Amri hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba, Kapteni mstaafu Dauda Kateme kwenye kikao cha madiwani wa halmashauri hiyo.
 Kateme alisema kumekuwa na taarifa nyingi za baadhi ya wenyeviti hao kuuza ardhi kiholela, huku madiwani wakiwa hawana habari.
 Alisema mara nyingi wenyeviti hao hawafuati sheria, badala yake wanauza ardhi kinyume na sheria jambo ambalo limesababisha migogoro ya kila siku kati ya wakulima na wafugaji au wananchi wenyewe kwa wenyewe.
Mbali na agizo hilo, kiongozi huyo aliwataka madiwani kuwahimiza na kuwasimamia watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha kuwa wanawasomea wananchi taarifa za mapato na matumizi ya kila mwezi ili kupunguza malamiko na kudumisha utawala bora.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe wa kikao hicho walidai kuwa kinachowasukuma wenyeviti wa vijiji na vitongoji kujiingiza katika uuzaji wa viwanja, ni kutopewa malipo yoyote na serikali kutokana na kazi zao.
Hata hivyo, hoja hiyo imepingwa na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Bukoba, Acheni Maulid, ambaye alisema kutopata posho kwa wenyeviti wa serikali za mitaa isiwe sababu ya wao kuvunja sheria na taratibu za nchi.
Badala yake aliwataka viongozi hao kupeleka malalamiko ama maoni yao ngazi za juu serikalini ili yapatiwe ufumbuzi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau