Bukobawadau

HUKO BRAZIL KIPENGA KOMBE LA DUNIA KUPULIZWA KESHO!

IMESALIA SIKU MOJA KABLA YA KOMBE LA DUNIA
Kila Kombe la Dunia lina taswira yake ya kipekee. Tarswira hiyo huoneshwa kupitia nembo maalum. Nembo hiyo rasmi ya Kombe la Dunia huwakilisha michuano yenyewe na nchi inayoandaa michuano hiyo kwa dunia.
Nembo rasmi ya Kombe la Dunia Brazil 2014 inajulikana kama "Kuhamasisha". Nembo hiyo ina picha ya mikono mitatu inayounda mfano wa Kombe la Dunia. Mikono hiyo mitatu ina rangi za manjano na kijani. Rangi hizi zinatoa ishara kuwa Brazil inakaribisha Ulimwengu mzima nchini humo.
Nembo hiyo imechaguliwa na jopo la wataalam, ambao walipitia nembo nyingine zipatazo 25 zilizopendekezwa na taasisi mbalimbali nchini Brazil

 Je wafahamu kuwa...
Brazil ni nchi ya tano duniani kuandaa Kombe la Dunia kwa mara ya pili -- baada ya miaka 64. Brazil iliandaa michuano ya nne ya Kombe la Dunia mwaka 1950. Uwanja wa MaracanĂ£ Rio de Janeiro ulijengwa mahsusi kwa ajili ya michuano hiyo, na utatumika pia mwaka huu.
Nchi nyingine ambazo zimeandaa Kombe la Dunia mara mbili ni: Mexico (1970, 1982), Italy (1934, 1990), Ufaransa (1938, 1998), na Ujerumani (1974, 2006)

 Je wajua kwamba...
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kombe la Dunia, rangi itatumika na waamuzi kuweka alama uwanjani wakati wa free kick. Rangi hiyo ambayo hutengenzwa kwa kutumia zaidi maji, itatumika kuweka alama mahala hasa kosa au 'foul' ilipotokea ili mpira uwekwe hapo bila kusogezwa. Pia rangi hiyo itatumika kuchora mstari ambao timu inatakiwa "kujenga ukuta". Hii itaepusha wachezaji kuusogelea mpira kabla free kick haijapigwa. Rangi hiyo ni nyeupe na hufutika baada ya kama dakika moja. FIFA iliidhinisha matumizi ya rangi hiyo katika Kombe la Dunia 2014, baada ya kutumiwa na kupata mafanikio katika Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 20, mwaka 2013, Kombe la Dunia chini ya miaka 17, mwaka 2013, na katika Kombe la Dunia la vilabu mwaka 2013.

 SIKU MOJA KABLA YA KOMBE LA DUNIA
Je wafahamu kuwa....Ronaldo de Lima, mchezaji wa zamani wa Brazil, huenda akapoteza rekodi yake ya kufunga magoli 15 katika michuano ya Kombe la Dunia.
Ronaldo alifunga bao lake la kwanza katika mechi dhidi ya Morocco mwaka 1998, ngazi ya makundi. Goli lake la mwisho na lililovunja rekodi alifunga mwaka 2006 dhidi ya Ghana.
Kwa kuwa Ronaldo amestaafu, rekodi yake sasa huenda ikachukuliwa na Miroslav Klose wa Ujerumani ambaye amefunga magoli 14 katika Kombe la Dunia.
Klose alifunga goli lake la kwanza katika Kombe la Dunia mwaka 2002 dhidi ya Saudi Arabia katika ngazi ya makundi.
Iwapo Klose atafunga angalau mabao mawili ataweka rekodi mpya.
Katika picha, Ronaldo de Lima alipotembelea jengo la utangazaji London Novemba 5 2013.
Next Post Previous Post
Bukobawadau