Bukobawadau

CHADEMA YAIBUKA KIDEDEA KESI YAO MAHAKAMA YA NJOMBE DHIDI YA MBUNGE WA CCM

MAHAKAMA ya Wilaya ya Njombe imetupia mbali kesi iliyokuwa ikiwakabili viongozi wa CHADEMA mkoani hapa, ya kutishia kummwagia tindikali Mbunge wa Njombe Kaskazini, Deo Sanga (CCM) maarufu kama Jah People.
 
Sanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Njombe, alidai kukumbana na tishio hilo wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Njombe mjini.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Malya, alisema kesi hiyo iliyokuwa chini ya Hakimu Augustino Rwizele, ilitupiliwa mbali kwa kutumia kifungu cha 91 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.

Alisema kuwa shitaka la kwanza lililokuwa likiwakabili viongozi hao ni lile lililotokea Februari 3, mwaka huu, ambapo washitakiwa Ali Mhagama, Robert Shejamabu na Award Kalonga walidaiwa kuvamia kikao cha CCM na kutishia kummwagia tindikali mbunge huyo.

Shitaka la pili lilimhusu Emmanuel Mwasongwe ambaye ni msaidizi wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, la kutoa lugha ya matusi dhidi ya Jeshi la Polisi mkoani Njombe.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa, viongozi wa CHADEMA waliviomba vyombo vya dola pamoja na mahakama kuendelea kufanya kazi kwa kufuata maadili ya kazi zao ili kila mwananchi apate haki yake.
Katibu wa CHADEMA Kata ya Njombe Mjini, Ali Mhagama aliwataka wananchi kuwa makini katika chaguzi mbalimbali zijazo kwa kuchagua viongozi ambao watajali maslahi ya umma.

“Tunamshukuru Mungu kwa kushinda kesi hii, na endapo tungepatikana na hatia leo hii, bila shaka kungekuwa na pengo kubwa katika utendaji wa kazi za chama,” alisema Mhagama.

Kalonga, alisema pamoja na kupigwa katika tukio hilo kiasi cha kuvunjwa taya, alishangaa kupelekwa polisi na kufunguliwa mashitaka huku akiwa ana maumivu makali.

“Siku hiyo nilivunjwa taya, baada ya hapo tulikimbia na kujifungia, lakini jambo la kushangaza ni kwamba tulipelekwa polisi na wakatufungulia mashitaka,” alisema Kalonga.
Akizungumza mara baada ya hukumu hiyo, Katibu wa CCM Wilaya ya Njombe, Clemence Mponzi, alikiri kuwa chama chake kilishindwa kwenda kutoa ushahidi na hivyo kuifanya mahakama itoe uamuzi wake.


Katika uchaguzi huo mdogo uliofanyika Februari 9, mwaka huu, CHADEMA ilishinda kupitia mgombea wake Joseph Mtambo, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na marehemu Lupyana Fute.
Next Post Previous Post
Bukobawadau