Bukobawadau

ADHA YA MICHANGO NA UGUMU WA MAISHA WA KUJITAKIA

Na Prudence Karugendo
 NIPO kazini, mfanyakazi mwenzangu ananiletea kadi ya kuomba mchango wa harusi ya mdogo wake. Papo hapo nakumbuka kwamba siku hiyo ndiyo siku ya mwisho ya kuwasilisha michango kwa ajili ya sherehe ya kumuaga binti ya jirani yangu (send-off) anayeolewa juma lijalo. Kwenye mkoba wangu kuna kadi nyingine tano zote zikidai michango kwa ajili ya sherehe mbalimbali.  Naona kuna ya kipa imara, komunio, “birthday”, ubatizo, na nyingine ni kwa ajili ya “graduation”.  Zote hizi zinatoka kwa ndugu, jamaa na marafiki,  ambao kila mmoja, kutokana na ukaribu tulio nao, ana imani ya kupata mchango wangu usiopungua shilingi elfu 50!
Baada ya kufika nyumbani nikitokea kazini nakuta mama (mke wangu) ameshika kadi inayomuarifu juu ya shughuli ya kumfunda binti ya shoga yake (kitchen party). Unatakiwa vilevile mchango usiopungua shilingi elfu 50 pamoja na doti moja ya khanga kwa ajili ya sare! Haraka haraka kadi hiyo ananipatia mimi huku akiwa amenikazia macho yanayoonyesha jinsi shughuli hiyo ilivyo muhimu kwake! Kwa hiyo kadi hiyo nayo inaongezwa kwenye idadi ya kadi za michango nilizotoka nazo kazini!
 
 Kabla sijakaa sawa rafiki yangu ananipigia simu kunijulisha uzinduzi wa nyumba yake, anatumia lugha ya masihara kama tulivyozoeshana, kwamba “nimpige tafu” japo kwa vikosi vitano  vya Wanamsimbazi. Maana yake ni kwamba ananialika kwenye tafrija ya uzinduzi wa nyumba yake pamoja na kuniomba mchango wa elfu 50. Wekundu wa Msimbazi ni neno  linalotumika kumaanisha noti ya shilingi elfu kumi.
 
Kesho yake niko kazini napata barua tatu kwa mpigo, zote kumbe ni kadi za kuomba michango! Kadi ya kwanza ni ya kanisa. Kanisa la Parokia ya kijijini kwetu linatimiza miaka hamsini toka lijengwe, kwahiyo wanaparokia popote walipo ulimwenguni wanaombwa kutoa michango yao kwa ajili ya kulifanyia sherehe ya jubilii ya dhahabu kanisa hilo!
 
Barua nyingine(kadi) inatoka kwa mjomba wake mama. Yeye anaomba mchango kwa ajili ya sherehe ya kumkaribisha nyumbani kwake rafiki yake wa kuchanjia, sherehe inayoitwa kwa Kihaya “okutaya omukago”. Anaomba tusimtupe mkono sababu anadumisha mila. Barua(kadi) ya tatu, ambayo ndiyo kiboko ya zote, inatoka kwa Baba mkubwa. Anasema anatimiza miaka tisini ya kuzaliwa, kwahiyo anataka kila mtoto amchangie elfu themanini na zawadi juu, anatishia kumwaga radhi kwa yeyote atakaye kaidi maelekezo yake!
 
Haya ndiyo maisha ya kawaida ya siku hizi. Michango michango kila kukicha. Michango ambayo inaendeshwa kwa mtindo wa mashindano bila ya wachangishaji kuzingatia ugumu wa kipato unaoikabili jamii yetu wala kufikiria jinsi ambavyo michango hiyo inavyoweza kutumiwa katika mambo ya maendeleo zaidi ya kuonyeshana  ufahari wa muda.
 
Jambo la kushangaza ni kwamba jamii yetu imeukubali mtindo huu wa maisha,  ambapo sasa kiwango cha chini cha kuchangia kimepandishwa mpaka sh. 100,000 bila kujali kipato kimepanda kwa kiasi gani!
 
Ingetokea mtu akaitisha mchango kwa ajili ya kumpeleka mtoto wake kidato cha kwanza lazima maneno ya kejeli yangejitokeza….mtu huyu kama hana hela ya kumpeleka mtoto wake shule si bora amuache akauze madafu, kila mtu anayo majukumu yake, basi ilmradi maneno ya kukatisha tamaa ili pasitokee watu,  katika jamii tuliyomo,  wenye mawazo ya kuwashirikisha wenzao kufanya mambo  yenye faida endelevu.
Wanajamii hawako tayari kumchangia mtoto wa mwenzao ili aende shule kwa sababu wanaamini faida ya kufanya hivyo wanaijua wazazi wa mtoto husika peke yao. Lakini mtoto huyo huyo angekuwa anaoa na watu wale wale wakapelekewa kadi za kuombea michango ya harusi wako tayari kuchanga kwa moyo mkunjufu! Hiyo ni pamoja na kuelewa mtindo wa ndoa za ziku hizi ambazo nyingi hazidumu kwa zaidi ya mwezi mmoja!
 
Ni wazi kwamba watu hawachangii ili kumwezesha kijana wa jamaa yao apate jiko, sababu kwa kijana huyo kupata jiko ni sawa na ambavyo angepata elimu, vyote viwili havionyeshi kurudisha faida ya moja kwa moja kwa wachangiaji, ila kinachoangaliwa ni namna mchangiaji atakavyo nufaika na mchango anaoutoa. Mtu anayechangia harusi anategemea kualikwa siku yasiku, na hii maana yake ni kula kunywa na kuserebuka.
Wakati anayejitosa kuchangia elimu ni kama anaona ametupa pesa yake kwa vile hajui ni  lini itatokea naye aalikwe kuserebukia mafanikio ya elimu aliyoichangia.
 
Kukosekana kwa fikira za kubuni, kupanga na kufanya mambo yenye manufaa endelevu ni tatizo kubwa linalochangia ukomavu wa ufukara katika jamii yetu. Pamoja na hilo, kitendo cha watu, kwenye jamii yetu, kupendelea kuonyeshana ufahari hata kwa wale wasio na uwezo endelevu wa kuhimili ufahari huo ni tatizo lingine. Na ni tatizo hili linalosababisha mfumuko wa michango ninayoiongelea hapa. Michango ambayo, kwa vile faida yake ni vigumu kuonekana, sioni sababu ya watu kuendelea kuchangiana.
 
Moja ya makabila yaliyokuwa na dira ya maendeleo toka zama za wahenga hapa nchini ni kabila la Wahaya. Wahaya walifanikiwa kupata maendeleo kutokana na,  pamoja na mambo mengine, kuwa na malengo mazuri katika kukabiliana na kila kilichoonekana kuwa kikwazo katika njia yao ya kutafuta maendeleo. Walifanikiwa kufanya mambo kadhaa yaliyoonekana kuwa msingi thabiti wa maendeleo yakiongozwa na elimu kiasi cha makabila mengine kuwabatiza jina la utani la “Nshomile”. Maana ya nshomile ni nimeelimika.
Siri moja ya mafanikio ya Wahaya kimaendeleo ilikuwa ni kushirikishana kwa lengo la kutafuta maendeleo hayo. Mfano, kijana alipokuwa anakaribia kuoa alikuwa anawaomba mchango vijana wenzake. Mchango wenyewe ulikuwa ni kumsaidia kijana mwenzao kutafuta miti, fito na nyasi kwa ajili ya kujengea na kuezekea ili siku ya kuoa awe  amepata kibanda chake. Hili ni jambo lililo katika mtizamo wa maendeleo. Wazazi wa kijana kwa upande wao, siku ya kuoa kijana wao ilipokuwa inakaribia, walikuwa wakipita kwa wazee wenzao wakiomba ndizi kwa ajili ya chakula cha sherehe ya harusi na ndizi kali kwa ajili ya kutengenezea pombe(olubisi) ya harusi. Michango hiyo inajulikana kwa Kihaya kama “omutwelo gw’ekitoke n’enkundi”,  basi kijana anaoa mambo yanaendelea.
 
Siku hizi mambo yamebadilika. Wahaya nao, kama jamii nyingine, wameathiriwa na hali hii ya sasa, inayojieleza kuwa ndiyo maendeleo ya wakati tulio nao. Hali ya kufanya mambo bila malengo ya baadaye, ilmradi kufurahisha watu na kutafuta sifa ya wakati huo tu! Kwa maana hiyo hutamsikia mtu, hata huku mjini,  anakwambia kwamba anaomba ndizi kali kijana wake anaoa, ilhali akijua kwamba mashamba ya ndizi kali tumeyaacha Bukoba! Kumbe maana yake anaomba mchango wa hela kiujanja ili atimize malengo yake ya kutangaza ufahari!
 
Hata wale walio kijijini wanaposema ndizi na ndizi kali siku hizi wanakuwa wanamaanisha mchango wa pesa. Mtu atakushangaa akija kwako kuomba ndizi na ndizi kali kwa ajili ya sherehe  halafu wewe humuongoze kwenda shambani kumuonyesha mikungu ya ndizi na ndizi kali yenye thamani isiyozidi sh. 20, 000,  wakati kichwani mwake alikuwa amepiga mahesabu ya kupata mchango wa sh. 100,000!
 
Hii inadhihirisha kwamba kinachotiliwa maanani siku hizi ni kiwango cha ufahari wa harusi bila kujali hao wanaooana wataishi maisha ya kiwango gani, hata kama ni kuoana leo na kesho yake wakaachana hiyo wazazi haiwahusu. Wao wanachojali ni kulinda heshima yao kwa kumfanyia mtoto wao harusi ya kifahari. Na kibaya zaidi hawategemei ufahari huo utoke mifukoni mwao, bali mifukoni mwa wenzao!
 
Kipindi fulani jirani zetu Kenya walikuwa wanaonekana wako mbele yetu kimaendeleo. Kielimu walikuwa mbele yetu, kiafya walikuwa mbele yetu, miundombinu yao ilikuwa imeboreshwa kuliko yetu. Hakuna miujiza yoyote tunayoweza kudai kwamba walikuwa nayo hawa jirani zetu iliyokuwa ikiwafanya wawe mbele yetu kwa karibu kila kitu.
 
Kitu pekee walichokuwa nacho ni ule moyo wa kutaka maendeleo. Kwa kuzingatia hali ya ufukara waliyokuwa nayo, ufukara ambao kiwango chake hakikupishana na kiwango cha ufukara wetu, waliamua kuikumbatia sawa sawa kaulimbiu iliyoanzishwa na Babawa Taifa lao,  Mzee Jommo Kenyatta, “harambee twende pamoja.” Ni kaulimbiu iliyokuwa ikiwatia hamasa ya kuunganisha nguvu zao ili kuyakabili mambo yaliyokuwa yanaonyesha kwamba vinginevyo yangewazidi nguvu katika harakati zao za kusaka maendeleo.
  
Kwa mtindo wa harambee waliweza kujenga mashule, mahospitali, barabara n.k. Pia waliweza kusomesha watoto wao kwa mtindo uleule wa harambee mpaka kufikia vyuo vikuu na wakati mwingine kuwapeleka baadhi ya vijana wao  kusomea ng’ambo. Wenzetu kule ni kawaida yao kuitisha mikutano ya harambee, na mtu akishapewa habari ya mkutano wa harambee moja kwa moja anakuwa ameishaelewa kuwa anaenda kushirikishwa katika jambo la maendeleo.
 Tofauti na kwa wenzetu, huku kwetu mtu akiitiwa kikao kitu cha kwanza atakachokifikiria ni sherehe! Na kwa vile sio kawaida watu kulipa michango katika kikao cha kwanza, mara nyingi  kikao cha kwanza kinapata watu wengi. Sababu ya watu kuwa wengi katika kikao cha kwanza ni kwamba watu wanakuwa wanaelewa  mtayarishaji wa kikao hicho,  haikosekani atakuwa ameandaa vitu vya kuwatia hamasa wanakikao,  ili waweze kutoa ahadi za michango iliyonona. Kwa hiyo atakuwa ameandaa vivywaji pamoja na vitafunwa.
  
Wanakikao wakishafika na kuelezwa matilaba ya kikao pamoja na kuhudumiwa kwa vinywaji na vyote vilivyoandaliwa, huwa hakuna anayeona tatizo la kutoa ahadi anayoona mdomo wake unaweza kuitamka. Kutamka ahadi siyo tatizo, mbinde ipo katika kulipa ahadi hiyo. Kawaida baada ya kikao, siku hizi, kuna kitu kinachoitwa “kichefuchefu” yaani kuchangia vinywaji kwa ajili ya kikao kinachofuatia. Hapo ndipo watu huanza kuteleza kwa kujifanya wengine wanaenda chooni kumbe ndiyo moja kwa moja wakiuwahi mzunguko wa bakuli la kichefuchefu kabla haujawafikia! Wale wanaokosa nafasi ya kuteleza bahati mbaya wakabambwa na bakuli la kichefuchefu, huku wakijua kwamba wameishatoa ahadi zinazolingana na uwezo wao wa kutamka, siyo uwezo wa kulipa, hutawasikia wakisema, tena kwa kujiamini, kuwa kwa leo hela sina ila naahidi sanduku moja la bia kwa kikao kijacho, mwingine ataahidi sanduku mbili za soda, kumbe watu hao tayari wamejifukuza,  ndio hawaonekani tena katika vikao hivyo!
 
 
Kama nilivyosema hapo juu vikao na michango ya aina hii ni kwa ajili ya kufanikisha umaarufu wa kuonyesha ufahari wa muda tu.
Haitokei vikao hivi vikawa kwa ajili ya kupanga kitu cha maendeleo endelevu. Mathalani,  katika baadhi ya sehemu hapa nchini,  utakuta mtu anao vijana kama wanne wote wakiwa hawana la kufanya, wawili wakitishiwa na janga la uvutaji wa bangi na kutumbukia kwenye magenge ya vibaka wakati wawili waliobaki wananyemelewa na umalaya wa reja reja (uchangudoa). Ukimuuliza kwanini vijana hao hakuwatafutia angalau vyuo vya ufundi ambavyo vingeweza kumgharimu kama shilingi milioni mbili kwa wote wanne, jibu unakuta liko tayari. Pesa sina, ninayo akiba yangu shilingi laki tatu ambayo nataka nijazie kutoka kwa watakaonichangia ili zifikie japo milioni tano, mwisho wa mwezi nataka niwacheze ngoma mabinti zangu wawili. Halafu atasisitiza kwa kutamba, unajua si mchezo kuwatoa wali wawili kwa pamoja, nataka wanitambue mtaa huu mimi ni nani!
 
Wakati mwingine mtu anatishiwa na mauti kwa kukosa shilingi laki moja tu za kulipa hospitali ili akapasuliwe busha! Lakini mtu huyo huyo mwezi uliopita alichangiwa hadi shilingi milioni 7 wakati anamtoa mwali!
 
Kama hatukujitahidi kubadilisha mtindo huu wa maisha ieleweke kwamba tunajimaliza sisi wenyewe. Tuchangie kwa kipimo, kwa maana ya kujali tunachokichangia tukiwa tumelinganisha na kipato tunachokipata, vinginevyo ugumu wa maisha unaojitokeza tunaulazimisha sisi wenyewe.
 
 
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau