Bukobawadau

KDCU Ltd. Kagera nao walia na ufisadi

Na Prudence Karugendo
WANA ushirika wa Chama kikuu cha Ushirika cha Karagwe District Co-operative Union (KDCU LTD.) cha wilaya za Karagwe na Kyerwa,  mkoani Kagera, nao wameanza kulia na hujuma za kifisadi zinazofanywa na uongozi wa chama chao hicho cha ushirika dhidi ya wanaushirika wake, wakulima wa zao la kahawa katika wilaya hizo mbili.
Ufisadi unaofanyika katika chama hicho unawafanya wakulima hao wa kahawa wafikirie jambo moja kati ya mawaili, ama kuachana na ukulima wa kahawa na kutafuta zao mbadala la biashara au kuachana kabisa na mfumo wa ushirika ili waanze kuuza mazao yao ya biashara kwa makampuni binafsi yanayowalipa pesa nzuri kwa muda muafaka bila kuwakopa.
Wanasema makampuni binafsi yanayoshughulika na ununuzi wa mazao yamedhihirisha ubora wake kutokana na kutokuwa na urasimu uliojaa ufisadi kama unavyojionyesha   kwenye ushirika.
Eti mpangilio wa ushirika, kuanzia kwa mwenyekiti, meneja, Bodi mpaka kwa wawakilishi wa vyama vya msingi,  ni urasimu mtupu unaokifanya chama kikuu cha ushirika kitumie karibu mapato yake yote, na hata pesa ya kukopa, kwa ajili ya uendeshaji wa mpangilio huo mbovu usiojali maana ya uwepo wake kwa wakulima. Kwahiyo eti kinachofanywa na ushirika ni kumfanya mkulima, ambaye ndiye uti wa mgongo wa chama cha ushirika, aambulie patupu!
Baada ya wanaushirika hao wa Karagwe na Kyerwa kutoa madai hayo, wanayosema wameishayafikisha hata kwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, na kuyapa kichwa cha habari “Okoa jahazi la wakulima unusuru KDCU Ltd. kabla ya kufilisika” bila kuona mafanikio yoyote, ndipo nikawaomba wanionyeshe ushahidi wa hicho wanachokisema.
Bila kwenda mbali wakanitolea ripoti ya makisio (Bajeti) ya KDCU Ltd. ya mwaka 2014 – 15.
Wanasema pamoja na KDCU kupata hasara ya sh. 1, 321, 679, 652/= katika msimu uliotangulia wa 2013 – 14, bado uongozi wa chama hicho, bila kujali hasara hiyo ambayo ni pamoja na deni la sh.1,237,000,000 la benki ya CRDB, unapanga bajeti ya kukiendesha chama hicho iliyo na mambo mengi yasiyokuwa na umuhimu wowote kwa chama chenyewe na kwa wakulima, isipokuwa kwa kuongeza gharama inayounufaisha uongozi tu pamoja na wanaoutetea na kuulinda ufisadi ndani ya ushirika huo.
Eti chama chao, kwa mujibu wa makisio ya mwaka 2014 – 15, ambayo nakala yake ninayo, KDCU Ltd. inafikia  kuwaweka kwenye bajeti hata watu wa nje, ambao sio wanaushirika, ila wakiwa na maslahi binafsi kwa uongozi wanaoukingia kifua ili usiwajibishwe na wanaushirika au mamlaka ya juu kinchi. Watu hao ni kama Mrajis Msaidizi wa Mkoa, maafisa ushirika wa wilaya na wanaoitwa wageni rasmi.
Wakati hayo yakifanyika kipato cha mkulima, mwanaushirika, kinazidi kufifia,  kisingizio kikubwa kikiwa ni kwamba bei ya kahawa inateremka kwenye soko la dunia!
Gharama hizo zilizo kwenye makisio ya mwaka huu ni pamoja na kumpangia mwakilishi wa chama cha msingi nauli ya sh. 60, 000/= kwenda na kurudi kwenye mkutano mkuu, ambayo kwa basi ni sawa na nauli ya kutoka Karagwe kwenda Dar es salaam, wakati mazingira ya wilaya za Karagwe na Kyerwa hayana umbali wa aina hiyo na hivyo kuyafanya makisio hayo yasionyeshe uhalali wowote kwa nauli hiyo.
Maafisa ushirika, ambao ni waajiriwa wa serikali, wakiwa wanalipiwa kila kitu na mwajiri wao wanapofanya kazi zao, nao eti wanaingizwa katika mahesabu ya chama cha ushirika ambapo nao kinawapangia bajeti kana kwamba kimewaajiri chenyewe! Tena eti kwenye bajeti hii, kama inavyoonekana kwenye ripoti ya makisio, wamepigiwa hesabu ya watu wawiliwawili!
Vilevile Mrajis Msaidizi wa Mkoa amepangiwa bajeti ya kwake inayoonyesha kwamba safari peke yake, Bukoba hadi Kayanga, Karagwe, kwenda na kurudi ni sh. 400, 000/=, ambayo ni zaidi ya nauli ya ndege kati ya Bukoba na Mwanza! Na ikumbukwe kwamba hakuna usafiri wa ndege kati ya Bukoba na Kayanga, na hata kama ungekuwepo nauli yake haiwezi kuwa hiyo, sawa na ya kwenda Mwanza, kutokana na tofauti ya umbali.
Mbali na usafiri huo wa kutisha, Mrajis Msaidizi pamoja na maafisa ushirika, nao wanapangiwa posho za vikao sh. 50, 000 x 2 x 4, posho za kujikimu sh. 50, 000 x 3 x 4 na kuongezewa asilimia 20 ambazo hazijulikani ni kwa ajili ya nini!
Wanaushirika wa Karagwe na Kyerwa wanajiuliza ni kwa nini gharama hizo zibebwe na chama chao wakati watu hao wanatimiza majukumu yao ambayo ndiyo yaliyowafanya wakaajiriwa na  serikali? Pia wanaushirika wanauliza, watu hao ni waajiriwa wa serikali kweli au wanafanya kazi ya kujitolea?
Eti kama wameajiriwa na serikali inakuwaje sasa wanalipwa na chama cha ushirika kwa kazi ambayo serikali inawalipa pia mishahara na posho kwa kutumia kodi za wanaushirika ikiamini kwamba inawawezesha wananchi kuendesha kilimo chao? Na kama watu hao wanafanya kazi ya kujitolea kwa nini ushirika uingie kwenye gharama kana kwamba umewakodi?
“Na vile vile, kama KDCU kilipata hasara kubwa katika misimu miwili iliopita na kuwa na madeni makubwa ya benki, kwa nini uongozi umepanga kutumia Sh. 110,000,000 kila mwaka kwa mikutano mikuu ya kifahari ambapo kila mjumbe analipwa Sh.180,000 kwa siku?  Aidha, inawezekanaje leo chama hicho kipange kuwalipa wajumbe wake 8 wa Bodi kiasi cha sh. 16,000,000 kama “bonus” bakshishi? Kitapata fedha hizo kutoka wapi kama sio kutumia vibaya fedha za mkopo kutoka benki za kununulia kahawa?”, wanauliza wanaushirika hao.
 
Kwa kadri mambo yalivyo, kumejengeka hisia kwa wanaushirika hao wa Karagwe na Kyerwa za kwamba madai ya kushuka kwa bei ya kahawa katika soko la dunia si ya kweli. Wao wanaona hicho ni kiinimacho tu, eti kiuhalisia  bei ya kahawa inashushwa na chama chao kikuu cha ushirika kutokana na chama hicho, kwa njia za kifisadi,  kujiingiza kwenye gharama zisizo na manufaa yoyote kwa wakulima wala kwa chama chenyewe.
Wanatoa mfano huo wa maafisa ushirika pamoja na Mrajisi Msaidizi wa mkoa kuonekana kwenye orodha ya wanaopaswa kulipwa na chama chao (payroll), kama kitu kimojawapo kinachowafanya wapate bei ya chini katika zao lao la kawaha huku wakidanganwa kuwa bei inashuka kwenye soko la dunia.
Jambo wanalojiuliza ni kwamba kama kweli bei ya kawaha inashuka kwenye soko la dunia, kwa nini kushuka uko kumuathiri mkulima peke yake bila kuugusa mfumo mzima wa chama cha ushirika? Wanasema haiwezekani chama cha ushirika kikawapangia nauli wajumbe wake  ya sh. 60, 000/= kwa umbali siozidi km. 50, wakati nauli hiyo inatosha kumsafirisha mtu kwa umbali usiopungua km. 1500, sawa na kutoka Karagwe kwenda Dar es salaam , wakati hakina mapato ya uhakika.
Eti kwa nini KDCU inaangalia kushuka kwa bei ya kahawa kwenye soko la dunia wakati wa kumlipa mkulima  tu, na hailizingatii hilo wakati wa kupanga “matanuzi” yake? Eti kwa nini wakati wa kupanga gharama za matumizi  chama hicho kinajiona kinao utajiri mkubwa kupindukia na hivyo kuamua kupandisha gharama  ya kila kitu kwa zaidi ya mara 10 wakati hali hiyo haimnufaishi mkulima?
Wanachoshindwa kukielewa wanaushirika wa KDCU Ltd. ni kwamba katika hali hiyo inayoonyesha wazi kuwa chama hicho kinawahonga wahusika wanaopaswa kukisimamia, kuanzia wawakilishi wa vyama vya msingi mpaka kwa maafisa ushirika na Mrajisi Msaidizi, watu hao wanawezaje kukisimamia na kuhakikisha kinawatendea haki wakulima?
Maana eti kama tayari chama kikuu kimeisha wafumba macho na kuwafunga midomo watu hao ili wasiangalie wala kusema chochote, kusudi wanaushirika waendelee kuteseka na umasikini ndani ya utajiri wao huku viongozi wa ushirika wakineemeka, inaonyesha nini kama sio kuwakaanga wanaushirika kwa mafuta yao?
Jambo hilo ndilo linalowaleta kwenye mawazo ya kwa nini ushirika uendelee kuwepo? Kwamba kama hali ndiyo hiyo, kuhenyeka kwa ajili ya watu fulani walio wachache, wasio na uadilifu, kwa nini wakulima wasiuze kahawa yao kwa makampuni binafsi yanayoiona na kuijali thamani ya zao la kahawa huku wakiwathamini pia wanaolizalisha zao hilo?
Pamoja na malalamiko hayo ya wanaushirika wa Karagwe na Kyerwa, bado wanakisifu chama chao hicho kwa kitendo cha kuonyesha uwazi na ukweli, japo ukweli huo unauma. Wanasema KDCU inakubali kuonyesha kwamba Mrajis Msaidizi, pamoja na maafisaushirika wa wilaya, wapo kwenye orodha ya wanaolipwa na chama hicho.
Hiyo ni kwamba waajiriwa hao wa serikali wanalipwa mara mbili kwa kazi ileile moja waliyoajiriwa kuifanya,  kitu ambacho kinapingana na sera ya utumishi wa umma.
Kwahiyo eti kama ushirika unakufa pasitafutwe mchawi kwingine, eti mchawi ni watumishi hao wa serikali walioajiriwa kuusimamia na kuulinda ushirika ili kuhakikisha unashamiri na kuimarika. Eti sasa watu hao ndio wanaogeuka na kuuelekeza kuzimu. Swali ni  kwa nini serikali inawakubalia wafanikishe uovu wao huo?
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau