Bukobawadau

NJIA KUU 6 ZA KUKUTOA KWENYE UMASIKINI

 Kila wakati ninapopata nafasi ya kuzungumza na watu juu ya maisha nimekuwa nikilisema hili mara kwa mara kuwa maisha tunayoishi yanaongozwa na kanuni. Kanuni hizi ndizo zinazoleta
matokeo ya aina fulani katika maisha yetu kila siku uwe unajua au hujui.

Kiuhalisia kutokana na kanuni hizi au njia hizi wale wanaofanikiwa hujikuta ndio wanaomudu kutumia kanuni hizi vizuri katika maisha yao na wale wasiofanikiwa na kuishia kwenye umaskini hujikuta wao ndio wanaoshindwa kutumia kanuni au njia hizi ndogo ndogo katika maisha yao.

 Ni kweli kama unataka kufanikiwa na kutoka kwenye umaskini ulionao ni lazima utumie njia hizi ambazo zitakusaidia sana katika mchakato mzima wa kupata utajiri katika maisha yako. Hizi ni njia ambazo zimetumiwa na watu mbalimbali waliofanikiwa kuwatoa kwenye umaskini na hatimaye kuwa matajiri.

Kwa kadri utakavyomudu kutumia njia hizi za mafanikio utakuwa unajitengenezea uwezo mkubwa wa kufanikiwa kwa kile unachofanya. Njia hizi ni zipi ambazo zinaweza kukutoa kwenye umaskini na hatimaye kukufanya kuwa tajiri? Hizi ndizo njia zinazoweza kukutoa kwenye umaskini:-

1. Amua kuwa tajiri.
Ili uweze kutoka kwenye umaskini ulionao hatua ya kwanza unayotakiwa kuchukua ni kuhakikisha unaamua kuwa tajiri. Maamuzi ya kuwa tajiri ni muhimu sana kwako kwani chochote utakachopania katika maisha yako utakipata, hii ikiwa na maana kuwa mtu ana uwezo wa kufanikisha kile anachoamini anaweza na si zaidi.

 Kama kwenye maisha yako umeamua kuwa tajiri, utakuwa tajiri kweli kikubwa maamuzi yako tu umeamua maisha yako yawe vipi. Kama upo kwenye safari ya kuelekea kwenye utajiri ambayo hata mimi ninayo ni lazima ufanye kile unachotafuta, kionekane kinawezekana kwako, weka malengo yatakayokufanya uendelee mbele zaidi kila siku.
2. Kuwa na mipango ya uhakika.
Kama una nia kweli ya kutoka kweli kwenye umaskini ulionao, hakikisha pia una mipango ya uhakika ya kukutoa pale ulipo. Kama unataka kufanya kitu fulani, tafuta njia itakayokutoa na hasa tafuta mtu mwingine aliyewahi kufanikisha jambo hilo unalotaka kulifanya.

Weka mipango ya uhakika na inayowezekana kwako kuifikia. Jifunze haya yote kwa wale waliofanikiwa zaidi yako. Unapokuwa na mipango ya uhakika inakuwa ni rahisi sana kwako kuifatilia na kiutekeleza. Acha kupanga mipango yako bila ya kuifatilia, ipange mipango yako kisha uifatile. Ikiwa huwezi kufatilia mipango yako nani ataifatilia?

3. Jifunze kutokukata tamaa mapema.
Hii ni njia muhimu sana kwako ya kukufanya wewe kuwa tajiri na kukutoa kwenye umaskini ulionao. Ukiwa na uwezo wa kupambana na vikwazo, ndicho kitu kitakachokufanya ufanikiwe zaidi, na si kukata tamaa na kuacha. Kila safari ya mafanikio ina changamoto zake na vikwazo vyake, hivyo inabidi kukabiliana navyo.

Utaweza kufika kule unakotaka , ikiwa utakuwa uko tayari kupambana na vikwazo vitakavyotokea njiani. Vikwazo vyote ni nafasi ya kufanikiwa kama utajifunza kitu kwenye hivyo vikwazo au matatizo yanayokuzunguka.

4. Jifunze kufanyia kazi ndoto zako kila siku.
Hii iko wazi kabisa ikiwa utaendelea kufikiria tu, unalofikiria litaendelea milele kubaki kwenye fikra zako na si zaidi. Ni lazima ufanye mambo kwa vitendo ili uweze kujikwamua na umaskini. Unatakiwa kuanzia mahali fulani hasa pale ulipo.
Mpaka utakapoanza ndipo utakapopata matokeo yatakayokusaidia kuweka misingi bora na mwelekeo wako. Ndege ni lazima ianze kwa kuruka inapofika hewani huanza kujiweka sawa ili upate mwelekeo mzuri wa kule inakokwenda.

Ni lazima uanze na mahala fulani popote, si lazima iwe mahala maalumu kama unavyofikiri, wewe anza tu kufanyia kazi ndoto zako mambo mengine yatajipanga mbele ya safari. Acha kusita sita fanyia kazi ndoto zako ili ufanikishe kile unacholenga.

5. Jifunze kuwa na bajeti maalumu katika maisha yako.
Unapokuwa na bajeti hii itakusaidia wewe kuwa na taarifa nyingi za matumizi na mapato ya pesa zako binafsi na za biashara zako. Ikiwa kila siku unaishi maisha ya kutoweka kumbukumbu hiyo itakusababishia kutojua wakati unapopotezaq fedha bila ya sababu hadi hali yako itakapokuwa mbaya zaidi.

Jijengee utaratibu wa kujiwekea bajeti hii itakufanya hautatumia pesa hovyo na hizo pesa utakazozotunza zitakusaidia sana katika kuwekeza pale zitakapokuwa nyingi na hatimaye zitakuoa kwenye umaskini.

6. Jijengee tabia ya kijiendeleza zaidi.
Ni watu wachache sana ambao huwa na tabia ya kujiendeleza kwa kujisomea mara baada ya kumaliza masomo. Kama unataka kuondokana na umaskini hakikisha unasoma mambo mengi na mapya ili kukabiliana na changamoto zaidi za dunia ya sasa.

Bahati mbaya sana mfumo wetu wa elimu tulionao sasa hautusaidii sana kuhusiana na hali halisi ya maisha yetu, hivyo usifikirie kwamba kwa vile umefika chuoni, basi una kila nyenzo ya kukufanya ufanikiwe. Unatakiwa kuendelea kujifunza, watu wenye mafanikio ni watu wakujifunza sana katika maisha yao yote.

CREDIT; AMKA MTANZANIA
Next Post Previous Post
Bukobawadau