Bukobawadau

UHAMIAJI:TULIMKAMATA NDAMBILE KIMAKOSA

IDARA ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam imesema mmiliki wa Kampuni ya Ulinzi ya Advance Security, Juma Ndambile alikamatwa kimakosa kwa tuhuma za kuwaingiza nchini na kuwahifadhi makomandoo wa kijeshi raia wa Nepal.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi, Naibu Kamishna wa Uhamiaji, Grace Hokororo, alisema hivi sasa wanamshikilia Ally Ally (25), kwa tuhuma hizo.
“Baada ya kufanya uchunguzi tulibaini Ally ndiyo mhusika mkuu wa kuwaingiza na kuwahifadhi makomandoo hao huku akiwatoza dola 3,000 za Marekani kila mmoja kwa madai ya kuwatafutia ajira hapa nchini…
“Mtuhumiwa huyo amekiri kutumia kampuni hiyo bila mmiliki kujua,” alisema Hokororo na kuongeza kwamba sheria za idara yake zitatumika kukomesha aina hiyo ya uhalifu hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Ally alisema kutokana na hali ngumu ya maisha alijiingiza kwenye ujasiriamali wa aina hiyo kwa kuwa walimuahidi fedha nyingi.
“Niliwaingiza kupitia wakala wao anaitwa Amit, kwamba niwatafutie kazi ili nipate kamisheni, nilikubali nikawapokea na kuwahifadhi…lakini walivyozidi kuja niliwakimbia kwa sababu nilishindwa kuwahudumia kutokana na uwingi wao hadi wanakamatwa walikuwa 12,” alisema Ally.
Agosti 25, 2014 idara ya Uhamiaji iliwakamata raia hao katika nyumba ya kulala wageni iliyopo Kijitonyama jijini hapa wakiishi nchini bila kibali.
TANZANIA DAIMA.
Next Post Previous Post
Bukobawadau