Bukobawadau

WANANCHI WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO KWA WATAALAM WA UTAFITI WA HALI YA UMASIKINI WA KAYA TANZANIA.

Naibu Waziri wa Fedha –Sera, Mhe. Mwigulu Nchemba akifungua mafunzo ya wiki tatu ya wakufunzi, wasimamizi na wadadisi kutoka Tanzania Bara  na  Zanzibar  watakaoendesha utafiti wa kufuatilia hali ya umasikini katika kaya mwaka 2014/15.
 Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Joel Bendera akiwakaribisha washiriki wa mafunzo ya wiki 3 ya utafiti wa kufuatilia hali ya umasikini katika kaya mwaka 2014/15 mkoani Morogoro.
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumzia  umuhimu wa matumizi ya takwimu sahihi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakufunzi, wasimamizi na wadadisi kutoka Tanzania Bara  na  Zanzibar  watakaoendesha utafiti wa kufuatilia hali ya umasikini katika kaya nchini mwaka 2014/15
 Naibu Waziri wa Fedha –Sera, Mhe. Mwigulu Nchemba akisalimiana na Mkuu wa mkoa wa Morogoro Mhe. Joel Bendera wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wiki tatu ya wakufunzi, wasimamizi na wadadisi kutoka Tanzania Bara  na  Zanzibar  watakaoendesha utafiti wa kufuatilia hali ya umasikini katika kaya mwaka 2014/15 mkoani Morogoro.
Washiriki wa mafunzo ya wiki tatu ya wakufunzi, wasimamizi na wadadisi kutoka Tanzania Bara  na  Zanzibar  watakaoendesha utafiti wa kufuatilia hali ya umasikini katika kaya nchini mwaka 2014/15 yanayofanyika mkoani Morogoro wakifuatilia masuala mbalimbali 
 Washiriki wa mafunzo ya wiki tatu ya wakufunzi, wasimamizi na wadadisi kutoka Tanzania Bara  na  Zanzibar  watakaoendesha utafiti wa kufuatilia hali ya umasikini katika kaya nchini mwaka 2014/15 yanayofanyika mkoani Morogoro wakifuatilia masuala mbalimbali .
Serikali imewataka wananchi na viongozi wa maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha kuwa wanatoa ushirikiano kwa wadadisi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu watakaoendesha  zoezi la utafiti wa ukusanyaji  wa takwimu za kufuatilia hali ya umasikini katika  kaya kwa mwaka 2014/2015, utaokaofanyika  kuanzia Oktoba mwaka huu.


Kauli hiyo imetolewa jana mkoani Morogoro na Naibu Waziri wa Fedha –Sera, Mhe. Mwigulu Nchemba wakati akifungua mafunzo ya wiki tatu ya wakufunzi, Wasimamizi na wadadisi watakaoendesha utafiti huo kutoka Tanzania Bara  na  Zanzibar.


Amesema serikali  kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa upande wa Bara na ile ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar  imeamua  kufanya utafiti huo ili kupata takwimu bora na sahihi zitakazoiwezesha kujitathmini na kupima juhudi zake katika kuwaletea wananchi maendeleo, kukuza uchumi na kupunguza umasikini wa kipato.


Amesema utafiti huo  pamoja na tafiti zilizopita utaiwezesha serikali kuchambua kiundani sababu zinazofanya kaya nyingi nchini kuendelea kubaki kwenye umasikini,  baadhi kutoka kwenye  umasikini na nyingine kuingia kwenye umasikini.


“Kufanyika kwa utafiti huu kutatuwezesha kufahamu namna na sababu zinazofanya kaya kuendelea kubakia kwenye umasikini , baadhi ya kaya kutoka kwenye umasikini na nyingine  kuingia kwenye umasikini” Amesema.


Ameongeza kuwa kukamilika kwa utafiti huo kutaiwezesha serikali kuelewa kwa kina changamoto zinazoikabili katika utekelezaji wa Sera, mikakati na programu mbalimbali za maendeleo kwa wananchi.


Mhe. Mwigulu amefafanua kuwa Serikali itaendelea kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuijengea uwezo ili iweze kukamilisha tafiti mbalimbali zinazoendelea kufanyika nchini kwa kufikisha matokeo ya tafiti hizo katika ngazi zote za utawala.


“Nia yetu ni kuhakikisha kuwa mipango ya maendeleo ya wananchi inapangwa kwa kutumia takwimu rasmi, kwa upande wetu serikali takwimu rasmi ni masikio  na macho katika utendaji wa kazi za kilia siku” Amesisitiza Mh. Mwigulu.


Aidha, amewataka wakufunzi, wasimamizi na wadadisi watakaoendesha zoezi hilo walio kwenye mafunzo hayo kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yote watakayopita kuhusiana na umuhimu wa zoezi hilo kwa taifa  na kusisitiza kuwa serikali haitawavumilia wadadisi watakaokiuka maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo amesema  kuwa washiriki wa mafunzo hayo watakaofaulu wataruhusiwa kushiriki katika utafiti huo.


Amesema kuwa utafiti huo hufanyika  kila baada ya miaka 2  kwa kuzipitia kaya binafsi ambazo huhojiwa kwa vipindi tofafuti ili kupata ufahamu wa namna ambavyo kaya zinaingia na kutoka kwenye hali ya umasikini wa kipato na sababu zinazochangia hali hiyo.


Ameeleza kuwa kwa mwaka huu utafiti huo utakuwa wa nne  kufanyika hapa nchini ukitanguliwa na zile zilizofanyika mwaka 2008/09, 2010/11 na 2012/13.


Amefafanua kuwa madodoso ya utafiti huo yatafuatilia na kukusanya taarifa muhimu za sekta nyingine muhimu ambazo zinaweza kuchambuliwa kwa  kuhusishwa  na hali ya umasikini zikiwemo kilimo, uvuvi, mifugo, Afya, Ajira na Upatikanaji wa huduma za maji, umeme, afya na elimu.


Amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu itahakikisha  takwimu hizo zinasambazwa katika ngazi zote za utawala kwa ajili ya kutumika  kupanga mipango ya maendeleo ya wananchi. 


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera awali akizungumza wakati wa kuwakaribisha washiriki wa mafunzo hayo mkoani Morogoro amesema kuwa bila takwimu sahihi hakuna mipango ya maendeleo inayoweza kufanyika.


Amesema kuwa kukamilika kwa utafiti huo  kutatoa picha halisi ya nini kifanyike katika kuwaletea maendeleo wananchi.


MWISHO.
Next Post Previous Post
Bukobawadau