Bukobawadau

WANAUSHIRIKA KAMACHUMU WAFANYIWA VITENDO VYA KIHUNI

Na Prudence Karugendo
CHAMA  cha Msingi Kamachumu ambacho ni kati ya vyama vya msingi vinavyounda Chama Kikuu cha Ushirika cha KCU (1990) Ltd., mkoani Kagera, kimefanyiwa uhuni mbaya sana ambao umemuacha kila mwanaushirika wa sehemu hiyo akijiuliza kama huo ni ushirika au kikundi cha watumwa waliokusanywa na kupewa maagizo ya nini cha kufanya na mamlaka iliyo juu yao bila wao kuhoji lolote!
Tofauti na hali halisi ilivyo, kwamba ushirika ni chombo cha hiari ambacho wananchi wanaamua wenyewe kukianzisha bila kushurutishwa ili kupata nguvu ya pamoja katika kukifanikisha walichokilenga, wananchi wa Kamachumu wamejikuta wanageuka wafungwa ndani ya ushirika wao wakiamriwa kumsikiliza mtu mmoja tu aliyejipachika ubwana jela na kuwataka wanaushirika hao wafanye namna anavyotaka yeye na si vinginevyo.
Kisa chenyewe, kama wanavyosimulia wanaushirika wa Kamachumu, kiko hivi; Kutokana na Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera, KCU (1990) Ltd., kufanya mambo mengi yaliyo na picha ya ufisadi huku wakulima wa kahawa, ambao ndio wadau pekee wa chama hicho, wakitaabika kwa ukata pasipo kuyaona manufaa yoyote ya zao la kahawa wala kuiona faida ya kuwa na ushirika, ndipo chama hicho cha msingi Kamachumu kwa kumtumia mwakilishi wake mmoja,  kikaanza kupaza sauti kuhoji mambo mbalimbali ambayo uongozi wa  KCU (1990) Ltd. hautaki yaulizwe wala kujadiliwa.
Baada ya hapo uongozi wa KCU (1990) Ltd. ukaanza kuwaangaza wale unaodai wanaleta kidomodomo ili washughulikiwe. Ndipo ikabainika kwamba mwakilishi mmoja wa Kamachumu, Archard F. Muhandiki, ndiye mwenye kuleta hoja zisizotakiwa na uongozi wa chama kikuu na hivyo kuamua afukuzwe kwenye mikutano ya chama hicho kikuu.
Kilichofuatia ni wanaushirika wa Kamachumu kuhoji uhalali na usahihi wa mwakilishi wao kuvuliwa kinyemela jukumu lake la uwakilishi alilopewa na wanaushirika wenzake katika chama chake cha msingi.
Wanaushirika hao wakasema kwamba kuzuiwa kwa mwakilishi wao kuhudhuria mikutano ya chama kikuu ni sawa na chama chao cha msingi  kutengwa na chama hicho kikuu au kuondolewa kabisa kwenye ushirika huo wa KCU (1990) Ltd.. Maana wanasema kwamba chama chao cha msingi hakiwezi kushiriki bila kushirikishwa kwa maana ya kuwakilishwa.
Kufuatia mtafaruku huo kati ya Chama Cha Msingi Kamachumu na KCU (1990) Ltd., wanaushirika wa chama hicho wakalazimisha uitishwe mkutano wa dharura ili, pamoja na mambo mengine, wakaliongelee hilo la mwakilishi wao kufanyiwa hujuma na KCU (1990) Ltd. akiwa anatimiza majukumu yake kwa mujibu wa taratibu za ushirika.
Kutokana na tuhuma ambazo wanaushirika wa Kamachumu walizielekeza kwa mwenyekiti wao, Super Karugaba, zinazodai kwamba anashirikiana na uongozi wa chama kikuu kukihujumu chama chao, wanaushirika hao wakapiga kura ya kutokuwa na imani na mwenyekiti huyo. Karugaba akaondolewa marakani pamoja na makamu wake kwa nguvu za wanaushirika. Kwahiyo Kamachumu wakabaki hawana uongozi.
Wanaushirika hao walihakikisha hayo yote yanawasilishwa kwa Afisa Ushirika wa wilaya ya Muleba kama utaratibu unavyoagiza. Pia wakamtaka afisa huyo kupanga tarehe ya kuitisha uchaguzi wa kuupata uongozi mpya wa chama hicho cha msingi. Lakini wanasema bahati mbaya au kwa makusudi Afisa Ushirika huyo aliamua kukaa kimya bila kuwajibu lolote!
Kamachumu ni eneo linalozalisha kahawa kwa wingi katika mkoa wa Kagera; kwahiyo ndilo tegemeo kuu la kahawa la KCU (1990) Ltd., na ndiyo maana chama hicho kinawekeza sana nguvu zake katika eneo hilo huku kikiwa hakitaki pawepo na uongozi imara na uwakilishi unaojisimamia.
KCU (1990) Ltd. iliendelea kumtambua Super Karugaba kama mwenyekiti wa Kamachumu pamoja na ukweli kwamba mwenyekiti huyo alikuwa hatambuliwi tena na wanaushirika wa chama hicho kwa vile walishamuondoa kwenye uongozi.
Swali linaloonekana kuwasumbua sana wanaushirika hao ni la kwamba uongozi wa chama cha msingi unapaswa utambuliwe na nani kwanza? Wanaushirika wanaouchagua au chama kikuu kinachoundwa na vyama vya msingi? Wanauliza kama chama kikuu ndicho kinavimiliki vyama vya msingi au vyenyewe kwa umoja wake ndivyo vinakimiliki chama kikuu?
Sababu eti bila chama kikuu vyama vya msingi vinaweza vikaendelea kuwepo, lakini bila vyama vya msingi vya ushirika hapawezi pakawepo chama kikuu cha ushirika!
Kwahiyo kutokana na chama kikuu, KCU (1990) Ltd. kutopenda kumpoteza Karugaba, mwenyekiti aliyeondolewa madarakani Kamachumu, kwa faida inayojulikana kwa KCU peke yake, chama hicho kikuu kikamkingia kifua kwa njia za kustaajabisha. Kwa kutumia mabavu, njama na vitisho dhidi ya wanaushirika wa chama cha msingi Kamachumu.
Ulipofika wakati wa uchaguzi uliofanyika ndani ya ushirika kwa mwaka huu, uliofanyika  kwa kuanzia na vyama vya msingi tarehe 5 Septemba, fomu za wagombea zikatolewa kinyemela bila matangazo yoyote kusudi wanaushirika wanaohofiwa na uongozi wa chama kikuu wasiweze kuziona na kupata nafasi ya kugombea.
Baada ya hapo kilichofanyika katika uchaguzi wa Chama Cha Msingi Kamachumu ndicho kimegeuka simulizi, sababu kimewaacha wananchi wakijiuliza wao ni wanaushirika au ni wafungwa?
Uchaguzi huo ulipaswa kusimamiwa na Afisa Ushirika wa wilaya ya Muleba kutokana na eneo la Kamachumu kuwa katika wilaya hiyo. Lakini sivyo ilivyokuwa.
Kwa hisia za kwamba Afisa Ushirika wa Muleba alikuwa na deni kwa wanaushirika hao wa Kamachumu la kutowajibu barua yao iliyomtaka aitishe uchaguzi kuziba pengo lililoachwa na uongozi uliondolewa madarakani, ikafanyika mipango yeye asiende kule na badala yake akaombwa Afisa Ushirika wa wilaya ya mbali,  Misenyi, iliyo mpakani mwa Tanzania na Uganda,  Amphrey Kachelele, ndiye akasafiri kwenda kusimamia uchaguzi huo.
Afisa Ushirika huyo, bilashaka baada ya kuelezwa kinachoendelea Kamachumu, akajiandaa kivita. Eti hakuthamini hata kidogo kama aliokutana nao ni watu wazima wenye heshima zao na waliokuwa wanafanya kitu kilicho chao na kwa manufaa yao!
Wanaushirika hao wa Kamachumu wanasema msimamizi huyo wa kuazimwa alipofika kwenye mkutano wao wa uchaguzi akaanza kumwaga vitisho na majigambo, akisema kwamba yeye ni msomi wa hali ya juu na kwamba mkutano ule ni wa kwake. Eti akaongeza kwa kujigamba kwamba hata kama angekuwepo Rais Kikwete ingembidi rais akae kule! Eti akasema kwahiyo hataki mtu yeyote kufanya “vyoko” hata kama angekuwa rais!
Na kwa vile fomu za kuombea nafasi za kugombea zilifichwa kiasi kwamba wanaushirika walio wengi hawakuziona, wajumbe, wanaushirika wa Kamachumu, hawakujua ni nani aliyekuwa anagombea uenyekiti wa chama chao cha msingi, kabla ya kuelezwa na msimamizi kuwa anayegombea uenyekiti ni mtu mmoja tu, Super Karugaba, mwenyekiti aliyeondolewa madarakani na wanaushirika kutokana na kukihujumu chama chao.
Kwahiyo msimamizi, kama alivyoelekezwa na waliompeleka kule, akaamuru kura zipigwe za ndiyo au hapana! Hiyo yote ni katika kumlinda Karugaba asiondoke kwenye uenyekiti ambao ameukalia kwa zaidi ya miaka 30 kinyume na kanuni za vyama vya ushirika.
Pia inasemwa kwamba msimamizi huyo toka Misenyi alishasema kwamba mkutano huo, aliouita wa kwake, ni lazima ungefanyika hata kama wanaushirika wote wa Kamachumu wangeususa akabaki yeye peke yake!
Hilo ndilo jambo lililowashtua wanaushirika hao wa Kamachumu na kumuona msimamizi huyo kuwa kaenda kwao kishari na wala sio kusimamia uchaguzi.
Kibaya zaidi ni kwamba msimamizi huyo alidiriki kuchukua karatasi ya kupigia kura toka kwa mmoja wa wapiga kura na kuichanachana mbele ya wajumbe wote wa mkutano huo akidai kwamba mjumbe  huyo kaichelewesha kura hiyo!
Swali kuu walilobaki nalo wanaushirika hao wa Kamachumu ni la kwamba kweli huo ndio ushirika au ni ufungwa? Swali hilo wanalielekeza kwa Rais Jakaya Kikwete ili aweze kuwafikiria akiwa ameufikiria ushirika kwa ujumla. Sababu wanasema kwamba maji yamewafika shingoni na hawana pengine pa kukimbilia.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau