Bukobawadau

WIZARA YA AFYA YAKABIDHI MABASI 6 KWA VYUO VYA AFYA NCHINI.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kabla ya kukabidhi mabasi 6 kwa wakuu wa vyuo vya Afya kutoka katika maeneo mbalimbali .Mabasi hayo yatasaidia kuaondoa upotevu wa muda na adha ya usafiri waliyokuwa wakiipata wanafunzi,watumishi na wakufunzi  wa vyuo hivyo  kufika kwenye maeneo ya mafunzo kwa vitendo.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo akikata utepe kwenye basi moja kati ya sita yaliyonunuliwa kwa ufadhili wa Mradi wa Mfuko wa Dunia mzunguko wa 9 ambayo yamekabidhiwa kwa wakuu wa vyuo vya afya leo jijini Dar es salaam.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo akikagua mabasi hayo yaliyonunuliwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia mzunguko wa 9 ambayo yamekabidhiwa kwa wakuu wa vyuo  6 vya afya leo jijini Dar es salaam.
 Sehemu ya ndani ya mabasi hayo yaliyotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Mradi wa Mfuko wa Dunia.
  
Na. Aron Msigwa – MAELEZO

25/9/2014. Dar es salaam.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii  imekabidhi mabasi 6 kwa  vyuo vya elimu ya Afya kwa lengo la kurahisisha huduma ya usafiri kwa wanafunzi na wakufunzi wanaokwenda kwenye mafunzo kwa vitendo katika maeneo mbalimbali nchini.

Vyuo vilivyokabidhiwa mabasi hayo ni Chuo Kikuu cha Hurbert Kairuki Memorial (HKMU) kilichopo jijini Dar es salaam, Chuo cha Uuuguzi Bagamoyo,Chuo cha Uuguzi Mirembe mkoani Dodoma, Chuo cha Uuguzi Tanga na Chuo cha Tabibu kilichopo mkoani Mtwara.

Akikabidhi mabasi hayo kwa wakuu wa vyuo hivyo leo jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo amesema mabasi hayo yatasaidia kuaondoa upotevu wa muda na adha ya usafiri waliyokuwa wakiipata wanafunzi,watumishi na wakufunzi  wa vyuo hivyo  kufika kwenye  maeneo ya mafunzo kwa vitendo.

“Ninakabidhi magari haya kwenu leo hii yakafanye kazi za kuwahudumia watumishi na wakufunzi wa maeneo yenu ya kazi, Ni wajibu wenu kuhakikisha mnayatunza na kuyafanyia matengenezo kulingana na miongozo iliyopo ili yaweze kudumu” Amesisitiza.

Amesema mabasi hayo 6 yamenunuliwa  kwa gharama ya shilingi milioni 344 kupitia ufadhili wa Mradi wa Mfuko wa Dunia mzunguko wa 9 ambao pamoja na mambo mengine unaisaidia Wizara katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya uzalishaji wa rasilimali watu wa kutoa huduma za afya nchini.

Bw.Pallangyo ameeleza kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeendelea kujenga uwezo kwa wataalam wa sekta ya afya hapa nchini  na kuongeza udahili kwa wanafunzi kwa lengo kuzalisha rasilimali watu wa kutoa huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini .

Amesema kutokana na kuongezeka kwa kasi ya udahili wa wanafunzi wa kada za afya, Serikali imeendelea kuvijengea uwezo vyuo hivyo kwa kujenga majengo mapya na kupanua yaliyopo ili yaweze kutumiwa na wanafunzi wengi zaidi wa fani za afya.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafuzo wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Otilia Gowelle akizungumza kabla ya makabidhiano ya magari hayo amesema kuwa Serikali imekuwa ikifanya juhudi ya kuhakikisha kuwa wanafunzi walio katika mafunzo ya kada mbalimbali za afya wanajengewa uwezo kwa kuboreshewa miundombinu, majengo, vifaa vya mafunzo vya maabara ili kurahisha mafunzo yao kwa vitendo.

Amesema kupatikana kwa mabasi hayo 6 ni sehemu ya mpango wa Wizara wa kuwawezesha wanafunzi wa vyuo hivyo kwenda kwenye maeneo ya mafunzo kwa vitendo nje ya vyuo wanavyosoma kwa  urahisi zaidi.
Nao baadhi ya wakuu wa vyuo hivyo vilivyopokea mabasi hayo Prof. Boniface Msamati wa Chuo Kikuu cha Hubert Kairuki cha jijini Dar es salaam na Mkuu wa Chuo cha Uuguzi Tanga ,Thomas Marato wakizungumza kwa niaba ya wenzao mara baada ya kupokea mabasi hayo wameishukuru serikali kwa kuwaondolea kero ya usafiri wanafunzi katika vyuo vyao.

Wamesema mabasi hayo yatatumika kuwasafirisha wanafunzi na wakufunzi kwenda katika maeneo mbalimbali nchini na kuwaondolea adha ya kukodi magari kwa fedha nyingi  kwa lengo la kuwapeleka wanafunzi wao kwenye mafunzo kwa vitendo katika maeneo yaliyo nje ya vyuo hivyo.
MWISHO.
Next Post Previous Post
Bukobawadau