Baada ya vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) kukubaliana kumsimamisha mgombea mmoja wa
urais katika uchaguzi mkuu mwakani, baadhi ya wasomi na viongozi wa
asasi za kiraia wameunga mkono hatua hiyo.
Aliyekuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Prof.
Mwesiga Baregu, alisema lengo la kuundwa kwa Ukawa lilikuwa ni
kuunganisha nguvu kusaidia mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya ambayo
alidai kupinduliwa.
Prof. Baregu, alisema maazimio ya Ukawa
yatasaidia kuunganisa makundi mengine yaliyokuwa ndani ya Bunge Maalumu
la Katiba ambayo yalikuwa na nia moja na umoja huo, hivyo kutia nguvu
baadaye.
“Lengo ni zuri, wanahitaji kujipanga upya. Ni uamuzi
ambao utaimarisha vyama vya siasa hapo baadaye. Itasaidia katika
vuguvugu hilo la katiba mpya kwa kuunganisha asasi za kiraia na wale
ambao hawakuridhika na mchakato wa katiba mpya. Itasaidia kuwaunganisha
Ukawa na Watanzania kwa ujumla,” alisema.
Mwenyekiti wa Jukwaa
la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba, alisema: “Mimi ninaafiki,
wanaweza wakaleta ushindi mkubwa sana, kwani ninavyoamini umoja ni nguvu
na utengano ni udhaifu.
Kwa mujibu wa Kibamba, Ukawa
wakifanikisha kutekeleza malengo hayo, wapigakura katika chaguzi zijazo
watakuwa na hamasa kubwa na kutafanya vyama vingine vya siasa ambavyo
havikuungana na Ukawa kuweza kufutika kwa kutolea mfano kwa Marekani.
Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tangayika (TLS), Francis Stolla,
aliunga mkono hoja hiyo, kwa kusema: “Sasa hakutakuwa na kugawana kura.
Wakitekeleza kweli, litaweza kuleta mafanikio makubwa kwa chaguzi
zijazo.”
CHANZO: NIPASHE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Du,kazi tunayo 2015,Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Africa!
Post a Comment