Bukobawadau

BARUA KWAKO MZEE JOSEPH SINDE WARIOBA!

Na Nova Kambota, Jumatatu Novemba 3, 2014
Shikamoo mzee wangu Warioba na pole sana kwa masaibu yaliyokukuta jana .
Mimi mjukuu wako pasi na shaka ukiangalia kwenye diary yako
utanikumbuka kwani niliwahi “kukutupia” swali moja pale chuo kikuu
Mzumbe siku ya tarehe 16 mwezi Novemba 2011.
Tangu hapo hatujapata kuonana tena ingawaje nimekuwa nikifatilia
harakati zako zote tangu hapo? Kwanini nimekuwa nikifatilia? Jibu ni
moja tu, kwa namna ulivyonijibu siku ile sikutia shaka uelewa wako
mkubwa sambamba na uzalendo wako usio na doa kwa taifa hili.
Ulizidi kunifurahisha zaidi kwa namna ulivyoratibu mchakato wa
kukusanya maoni ya katiba mpya na uandaaji wa rasimu. Najua wapo
baadhi ya “wakubwa” hawafurahishwi na namna unavyotetea kile
unachoamini ni chema kwa vizazi vijavyo vya Tanzania, Mungu akubariki
sana.
Vitimbi ulivyofanyiwa na maneno ya kejeli uliyojibiwa yanaonyesha kuwa
hayajakuvunja moyo hata kidogo, kwani jana nilikuona ukiongea kwa uso
uliojaa bashasha huku ukidhihirisha kuwa ungali na ari ileile ya
kupigania katiba ya wananchi.
Sitaki kukuchosha kwa maneno mengi mzee wangu lakini nina uhakika
Mungu yuko upande wako katika hili, tuliotega sikio na kukusikiliza
tunajua unaongea ukweli mtupu na MSEMA KWELI NI MPENZI WA MUNGU.
    Hata manabii walipingwa na kudhihakiwa hivyohivyo lakini leo
tunawasoma na kuwaheshimu kama mashujaa wa imani, ni ukweli kuwa
katiba lazima iwe mwafaka wa kitaifa na siyo mpasuko wa kitaifa,
wanaokupinga wanalijua hili?
                    Wasalam,
                               Ni mimi  Mjukuu wako mtiifu,
                                                    Nova Kambota
0712-544237, novakambota@gmail.com , http://novakambota.wordpress.com
Next Post Previous Post
Bukobawadau