Bukobawadau

KUFUATILIA UDHAIFU WA UTEKELEZAJI/UTENDAJI WA WIZARA YA MAJI, DAWASA, DAWASCO NA EWURA

Kumb: OMU/MJ/19/01                                                           17/01/2015


Spika
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi Ndogo
Dar Es Salaam:

Mheshimiwa,

YAH: KUFUATILIA UDHAIFU WA UTEKELEZAJI/UTENDAJI WA WIZARA YA MAJI, DAWASA, DAWASCO NA EWURA KUHUSU HATUA ZA HARAKA ZA KUBORESHA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA USHUGHULIKIAJI WA MAJI TAKA KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM

Utakumbuka kwamba tarehe 4 Februari 2013 niliwasilisha Hoja Binafsi ya kutaka hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar Es Salaam.

Baada ya kuwasilisha hoja hiyo Waziri wa Maji badala ya kuchangia kwa kujibu hoja kama kanuni ya 53 (6) (c) aliwasilisha hoja tofauti kwa kutumia kanuni ya 57 (1) (c) ya kuiondoa hoja yangu isiendelee kujadiliwa kwa maelezo kwamba “tayari kuna mpango maalum uliotengewa fedha nyingi na Serikali ya CCM na kwa kuzingatia kuwa utekelezaji wa mpango huo unaendelea vizuri sana”.

Waziri alikiuka kanuni za Bunge kwa kuwasilisha hoja hiyo kwa kuwa kanuni ya 57 (4) badiliko hilo lilikuwa linapingana na hoja kwa kuwa linaiondoa hoja yenyewe na kanuni ya 58 (5) ambayo inaelekeza kwamba hoja ikishawasilishwa anayeweza kuondoa hoja ni mtoa hoja mwenyewe tu tena kwa idhini ya Bunge.

Aidha, Waziri wa Maji alitoa maelezo yenye kulidanganya bunge, kujenga matumaini hewa fedha za kutosha zimetengwa na utekelezaji unakwenda vizuri sana. Hiyo ilikuwa kinyume kabisa na maelezo yake mwenyewe bungeni tarehe 10 Julai 2012, 7 Novemba 2012 na nyaraka nilizonazo za ndani ya Serikali za Januari 2013.

Pia, Waziri wa Maji hakutoa maelezo kuhusu mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha (Dar es salaam Water Supply and Sanitation Project-DWSSP) uliotumia dola milioni 164.6 hata hivyo mpaka sasa katika maeneo mengi mtandao wake maarufu kama mabomba ya Wachina, hautoi maji huku kukiwa na upungufu katika uzalishaji, upotevu wakati wa usafirishaji, udhaifu katika usambazaji na tuhuma za ufisadi katika matumizi.

Hakujibu pia iwapo Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) atafanya ukaguzi  maalum wa matumizi ya fedha matumizi ya bilioni 96.4 za mradi wa maji safi na mazingira vijijini katika Jiji la Dar es salaam na Halmashauri zingine na kuwezesha hatua za ziada kuchukuliwa kutokana na matumizi mabaya ya fedha pamoja na kasoro zingine katika utekelezi wa Programu ya Maji Safi na Mazingira Vijijini (RWSSP) ikiwemo katika Manispaa za Jiji la Dar es Salaam ilipaswa kutekelezwa kuanzia mwaka 2005/2006 na kukamilika mwaka 2010/2011.

Kwa ujumla, hakueleza hatua zozote ambazo Serikali ingetarajia kuchukua kutokana na hatua tisa za haraka nilizopendekeza kwenye hoja yangu na masuala niliyotaka yazingatiwe kutoka katika maelezo yangu ili kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es salaam. (Nakala ya Hoja nimeiambatanisha).

Ikumbukwe kwamba mnamo tarehe 23 Machi, 2012 nilishiriki ziara ya kikazi kukagua shughuli za DAWASA na DAWASCO ambapo wakati wa ziara hiyo nilipatiwa maelezo kuhusu mpango maalum wa kulipatia maji Jiji la Dar es Salaam, ambao utekelezaji wake ulianza mwaka 2011.

Katika ziara hiyo nilitembelea Mtambo wa Maji wa Ruvu Juu, na baadaye chanzo cha maji cha Ruvu Chini kuona kazi ya upanuzi ya mtambo wa maji wa Ruvu Chini inavyoendelea.

Hata hivyo, nilibaini kwamba kasi ya utekelezaji wa mradi haikuwa inaridhisha hivyo mwezi Oktoba 2012 niliwasilisha taarifa ya hoja binafsi kutaka Bunge lipitishe maazimio ya hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar Es Salaam.

Uamuzi wangu uliifanya Wizara ya Maji itoe kauli ya Serikali Bungeni tarehe 7 Novemba 2012 kuhusu Mpango wa Haraka wa Maji katika Jiji la Dar Es Salaam na kutoa ratiba ya utekelezaji.

Lakini, baada ya kufuatilia kwa miezi miwili na kubaini kwamba hatua hizo za haraka hazichukuliwi kikamilifu tarehe 4 Februari 2013 niliwasilisha hoja binafsi bungeni kuhusu hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar Es Salaam.

Uamuzi huo uliifanya Wizara ya Maji, DAWASA na DAWASCO kuchukua hatua nyingine za ziada kabla, wakati na baada ya hoja hiyo ambazo nashukuru zimeboresha upatikanaji wa maji safi katika baadhi ya maeneo na kuongeza jitihada za kutekeleza miradi mbalimbali ya maji pamoja  na kuwa Waziri wa Maji alisema uongo bungeni na kupendekeza hoja hiyo iondolewe.

Hata hivyo, yapo maeneo mengine ambayo bado matatizo yanaendelea na kwa ujumla Wizara imekuwa haitekelezi kikamilifu ahadi zake ilizotoa bungeni kwa nyakati mbalimbali miaka ya 2011, 2012, 2013 na 2014.

Aidha, kumekuwa na udhaifu wa utendaji katika Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA), Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) na hivyo kupunguza ufanisi ambao ungewezesha hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar Es Salaam.

Hivyo, kwa kuzingatia Kanuni ya 5 (1) na Nyongeza ya Nane Kanuni ndogo ya 7 (1) (c) (e) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Aprili 2013 naomba uelekeze Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji katika vikao vinavyoendelea kabla ya Mkutano ujao wa Bunge ifuatilie utekelezaji wa Wizara, DAWASA, DAWASCO, EWURA kwa kurejea hoja binafsi niliyowasilisha bungeni, udhaifu unaoendelea mpaka sasa na malalamiko ya wananchi.

Izingatiwe kuwa mradi wa upanuzi wa Ruvu Chini ulipaswa kukamilika kabla ya mwezi Machi 2013; hata hivyo kutokana na udhaifu mbalimbali mradi huo haujakamilika mpaka sasa.

Aidha, kumekuwepo na udhaifu katika utekelezaji wa mradi wa ulazaji wa Bomba Kuu la kipenyo cha milimeta 1,800 kutoka mtambo wa Ruvu Chini hadi Jijini Dar Es Salaam ambapo ilipaswa maji yawe yamefika jijini ikiwemo katika Jimbo la Ubungo Januari 2014 kwa gharama za Shilingi bilioni 192.68.

Kwa upande mwingine, pamoja na Serikali ya Tanzania kupata fedha kutoka Serikali ya India dola za Kimarekani milioni 178.125 sawa na Shilingi bilioni 289.45 kwa ajili ya  upanuzi wa chanzo cha maji Ruvu Juu kumekuwepo na udhaifu wa utekelezaji ambao Wizara ya Maji na DAWASA wanapaswa kutoa maelezo kwa Kamati tajwa ya Bunge.

Mradi huo unahusisha ulazaji wa bomba kuu kutoka Mlandizi hadi Kimara; na Ujenzi wa tanki kubwa katika eneo la Kibamba; usanifu na ujenzi wa mabomba ya usambazaji katika maeneo ambayo hayana mtandao wa maji.

Ujenzi wa mradi huo ulipaswa kuanza toka Agosti 2013, hata hivyo mwezi huo ulipita bila ujenzi kuanza hali ambayo ilichelewesha hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi.

Hata baada ya kusainiwa Januari 2014 kwa mikataba ya ujenzi wa Bomba kati ya Serikali na kampuni ya Megha Engineering and Infrastructural Ltd na wa upanuzi wa mtambo wa kusafisha maji Septemba 2014 kati ya Serikali na Kampuni ya VA-TECH WABAG kuna udhaifu wa utekelezaji. 

Kadhalika usanifu na utayarishaji wa vitabu vya zabuni kwa ajili wa ujenzi wa bwawa la Kidunda Mkoani Morogoro ambalo litachangia kuboresha upatikanaji wa maji katika mkoa huo na mikoa ya Pwani na Dar Es Salaam haukukamilika mapema 2013 kama ambavyo Wizara ya Maji iliahidi.

Serikali imekuwa ikisuasua kutenga kwa ukamilifu fedha za ujenzi wa bwawa tajwa zinazokadiriwa kufikia Shilingi bilioni 179.7 hali inayohitaji Bunge kushauri na kuisimamia Serikali ipasavyo.

Wakati huo huo, kwa miaka mingi kumekuwepo pia udhaifu katika kuchukua hatua za kupunguza uvujaji wa maji na maji yasiyolipiwa (non-revenue water) ambapo ilipaswa toka mwaka 2010 kupunguzwa kutoka katika ya 50-60 mpaka asilimilia 25 lakini mpaka sasa utekelezaji ni hafifu.

Tafsiri ya hali hii ni kwamba kwa kuondoa tu upotevu wa maji unaohusisha pia ufisadi na biashara haramu, bila hata kuongeza kiwango cha uzalishaji nusu ya tatizo la maji katika Jiji la Dar Es Salaam ingeweza kupungua au walau hata robo. Hatua hii inahitaji shilingi bilioni 17 tu ambazo Wizara ya Maji, DAWASA na DAWASCO wamekuwa wakisuasua kuzitenga na kutekeleza mipango kwa wakati.

Iwapo hatua zote hizo za haraka na zingine zingechukuliwa maeneo ambayo mabomba yalilazwa na kukarabatiwa ambayo hayapati maji na maeneo yote ambayo hayana mtandao wa maji kwa sasa yangepata maji ya kutosha.

Hatua hiyo ingeambatana na kuhakikisha maeneo mengine yanajengewa mtandao mpya wa mabomba ya majisafi hususani Kiluvya, Kibamba, Mbezi Luisi, Mbezi Msumi, Msakuzi, Makabe, Mpiji Magohe, Saranga, Malambamawili, King’ong’o, Matosa, Bonyokwa, Kibangu, Kinzudi na Goba katika Jimbo la Ubungo.

Hatua hizo zingenufaisha pia wananchi wa majimbo mengine katika Jiji la Dar Es Salaam na Mkoa wa Pwani ikiwemo wa  Kinyerezi, Kipawa, Kiwalani, Vinguguti, Uwanja wa Ndege, Ukonga, Gongolamboto, Pugu, Chanika, Tegeta, Bahari Beach, Boko, Bunju, Salasala, Mbezi Juu, Madale, Kisota, Mabwepande, Mpiji, Vikawe, Mapinga, Zinga, Kilombo, Bagamoyo, Kibaha na Mlandizi ambayo hayakufikiwa na miradi ya awali.

Hivyo, kikao na Kamati ya Bunge kitawezesha hatua za haraka za kutolewa kwa kiasi cha Shilingi bilioni 138.85 zinazohitajika kufanikisha kazi hiyo.

Yapo masuala mengi mengine ambayo ni muhimu yakazingatiwa na Bunge kuhusu hatua za haraka za uboreshaji wa upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar Es Salaam ambayo nitayawasilisha kwa Kamati husika ya Bunge ikiwaita viongozi na watendaji wakuu wa Wizara ya Maji, DAWASA, DAWASCO na EWURA.

Wako katika uwakilishi wa wananchi,

John Mnyika (Mb)
Next Post Previous Post
Bukobawadau