Bukobawadau

BODI MPYA YA KCU (1990) LTD INAWEZA KUUFUFUA AU KUUZIKA USHIRIKA

NA PRUDENCE KARUGENDO
PAMOJA  na wakulima wa kahawa mkoani Kagera kuufurahia uamuzi wa kuisimamisha kazi Bodi ya Wakurugenzi ya zamani ya chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd., bado yapo mambo yanayowatia wasiwasi wakulima hao wa kahawa na kuwafanya wahisi kwamba Bodi mpya iliyochaguliwa siku chache zilizopita inaweza isifanye kazi zake kwa usahihi kutokana na kuathiriwa na kinachoonekana kama vidudu nyemelezi toka kwenye Bodi iliyotangulia.
Wakulima hao wanakuwa na mtazamo huo katika sehemu mbili tofauti. Sehemu ya kwanza inaonyesha kwamba uamuzi wa kuisimamisha Bodi ya zamani, pamoja na kuonekana ni uamuzi mzuri, lakini eti ulicheleweshwa sana kiasi cha kuifanya Bodi hiyo kusambaza virusi vyake ambavyo vimeleta madhara makubwa na kuifanya kazi ya kuyasafisha madhara hayo iwe ngumu.
Inasemwa kwamba ugumu wa kuyasafisha madhara yaliyoachwa na Bodi iliyotangulia uko namna hii; Bodi hiyo ilisimamia uchaguzi wa vyama vya msingi vinavyounda chama kikuu cha KCU (1990) Ltd.. Usimamizi huo ulikuwa wa mizengwe mitupu ambapo Bodi hiyo ya zamani ya chama kikuu ilikuwa inahakikisha wanapatikana wawakilishi na wajumbe wa Bodi za vyama vya msingi ambao walikuwa wanaelewana na wajumbe wa Bodi ya chama kikuu ambao wangeweza kushirikiana kukihujumu chama hicho bila ya kupigiwa makelele yoyote.
Inasemekana hayo yalifanyika kwa imani kwamba wakurugenzi wa Bodi ya chama kikuu pengine wangeendelea kuwa walewale waliokuwa wakilalamikiwa na wanaushirika muda wote. Kwahiyo mizengwe iliyofanyika mpaka wakapatikana wawakilishi hao wa  vyama vya msingi ilikuwa imelenga kujihami dhidi ya wanaushirika waliokuwa wakihoji juu ya mwenendo usioeleweka wa wakurugenzi wa Bodi ya chama kikuu.
Kwahiyo kusimamishwa, au niseme kuzuiwa kugombea tena, kwa wakurugenzi wa zamani, ni kitu kilichojitokeza bila kutegemewa na yeyote. Hivyo Bodi mpya ya wakurugenzi wa KCU (1990) Ltd., ambayo bilashaka haikutegemewa, haiwezi kufanya kazi zake kiusahihi kwa kushirikiana na wakurugenzi wa Bodi za vyama vya msingi ambao walikuwa tayari kufanya kazi na Bodi iliyosimamishwa. Pia wawakilishi wa vyama vya msingi ambao walichaguliwa kwa malengo ya kuibeba Bodi iliyopita watajikuta wanashindwa kufanya kazi barabara na Bodi mpya.
Bodi mpya, hata kama itakuwa imekusudia kufanya mambo mazuri ya kuusimamia uongozi wa KCU (1990) Ltd. inaweza ikatatizwa na uwepo wa Bodi za vyama vya msingi ambazo zimewekwa kwa manufaa ya Bodi iliyosimamishwa. Kwa mantiki hiyo ingefaa Bodi zote za vyama vya msingi nazo zifumuliwe na kuundwa upya, na ikiwezekana wajumbe wake wote waliokuwemo nao wazuiwe kugombea tena,  kwa mtazamo uleule uliowafanya wajumbe wa Bodi ya chama kikuu kuzuiwa kugombea tena.
Hiyo ndiyo ingeonekana ni kuusafisha uchafu uliokuwa kwenye ushirika huo kwa maana halisi. Sababu haiwezekani kuustawisha mmea kwa kuuangalia tu juu kwenye majani yake bila kuuangalia kuanzia chini kwenye shina lake. Ushirika unaanzia kwenye vyama vya msingi, hayo ndiyo mashina ya ushirika,  sababu kule ndiko wanaushirika waliko wanaolima mazao yanayoshughulikiwa na ushirika husika.
La pili wanalolisema wanaushirika kuhusu Bodi mpya ni la uongozi wa chama hicho kikuu cha ushirika. Wanasema kwamba tatizo lililokuwa kwenye Bodi iliyopita ni la kutokuelewa majukumu yake. Wanasema kwamba Bodi ya wakurugenzi kazi yake kuu ni kuusimamia uongozi na kuutolea maelekezo. Lakini eti kinyume chake uongozi wa KCU (1990) Ltd. ndio uliokuwa ukiisimamia Bodi na kuielekeza ifanye nini!
Kwamba maamuzi mengi yaliyoenda kinyume na kuufanya ushirika huo uonekane umeanza kutetereka yalikuwa yanatolewa na uongozi na kuilazimisha Bodi kuyabariki. Kwa muonekano huo Bodi haikuwa na maana yoyote, sababu yenyewe ipo kuusimamia uongozi, “management”, na si kinyume chake.
Kwahiyo wanaushirika wanasema kwamba ili Bodi mpya ionekane inaleta matumaini ingeanza kwa kuuondoa uongozi uliokuwepo tangu wakati wa Bodi iliyondolewa kwa kushindwa kazi. Hiyo ingeleta maana ya kwamba Bodi iliyoondolewa haikuonewa, na zaidi kuonyesha kwamba hii iliyowekwa sasa imeingia kuboresha kwa kuparekebisha pale ambapo paliishinda Bodi iliyoondolewa.
Taarifa zinazotoka kwenye uongozi wa chama hicho cha ushirika zinaonyesha kwamba kwa sasa chama hicho kinaendeshwa na kitengo chake kimoja cha Moshi Export. Mishahara na mambo mengine yote yanategemewa kupatikana toka Moshi Export.
Kitengo cha Moshi Export kilianzishwa kama idara inayojitegemea kwa lengo la kuitafutia soko, hasa soko la nje,  kahawa inayolimwa Bukoba na maeneo jirani. Lakini hakikuanzishwa kwa ajili ya kuuendesha ushirika kama kinavyofanya kwa sasa.
Kwa mantiki hiyo, baadhi ya wafanyakazi ndani ya uongozi wa KCU (1990) Ltd. wanauliza kwamba kama chama kinajiendesha kwa kukitegemea kitengo chake kimoja tu kilichoko Moshi, inawezekanaje meneja mkuu abaki yuleyule aliyeko Bukoba wakati ikionekana hana lolote la kufanya zaidi ya kumtegemea mkuu wa kitengo cha Moshi Export amalize kila kitu?
Wanasema kwamba kwa sasa kitengo hicho cha Moshi karibu kinafilisika kutokana na kuwa na majukumu yaliyokizi uwezo kwa vile hayakuwa malengo yake tangu kilipoanzishwa.
Hapohapo ndipo linajitokeza swali la kwa nini watumishi wakuu wa KCU (1990) Ltd. kama meneja mkuu, meneja wa fedha, mhasibu mkuu na wengineo waendelee kunufaika na vyeo vyao pasipokufanya lolote lenye tija kwa ushirika lililowafanya wakapewa utumishi huo? Eti kwa nini kisiachwe kitengo cha Moshi tu ndicho kikabaki kinauendesha ushirika huo kuliko kuendelea kupata maelekezo toka Bukoba ambako kumebaki mahali pa matumizi tu pasipozalisha kitu?
Hiyo ndiyo changamoto inayoikabili Bodi mpya ya wakurugenzi ya KCU (1990) Ltd., inatakiwa iliangalie hilo na kujipambanua na Bodi iliyoondolewa kwa kushindwa kazi. Kwahiyo kwa kutaka kuonyesha kuwa kazi iliyopewa inaiweza Bodi mpya inapaswa iyafanye yaliyoishinda Bodi iliyopita.
Kama alivyosema mmoja wa wajumbe wa Bodi mpya, Bodi hii ina mawili, ama kuufufua ushirika wa KCU (1990) Ltd. au kuuzika moja kwa moja. Kila la heri Bodi mpya.
Next Post Previous Post
Bukobawadau