MKOA WA KAGERA WAZINDUA RASMI USAMBAZAJI WA KATIBA PENDEKEZWA LEO FEBRUARI 20, 2015
Katika uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa
wa Kagera Mhe. John Mongella
aliwasistiza viongozi na wadau waliohudhuria katika uzinduzi huo kuwahamasisha
wananchi kusoma Katiba pendekezwa na kuielewa ili wakati ukifika waweze
kuipigia kura ya ndiyo au hapana bila kupotoshwa.
Mhe. Mongella aliwaomba wananchi kuilewa
Katiba pendekezwa bila kushawishiwa na miemuko ya vyama, dini, watu binafsi kwa
mitazamo yao au makundi mbalimbali ili wakati ukifika waweze kutoa maamuzi yao
wenyewe katika kupiga kura ya ndiyo au hapana.
Akisistiza kuhusu kupiga kura
Mhe. Mongella amewaomba viongozi wa dini Wakuu wa Wilaya, Viongozi wa Taasisi
na Mashirika ya serikali na na yasiyokuwa ya serikali kuhakikisha wanawahamasisha wananchi
kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ili kupata haki ya kupiga kura ya
ndiyo au hapana kwa katiba pendekezwa na
Uchaguzi Mkuu ujao mwezi Oktoba mwaka huu 2015.
Aidha, Mhe. Mongella aliwaomba
wadau kuwafikiria kundi la tatu ambalo pengine wao hawataki kusema chochote
kuhusu katiba pendekezwa kuwa nao waheshimiwe na kusikilizwa ukiacha makundi yatakayopita kwa wananchi kuhamasisha wananchi
kupiga kura ya ndiyo na kura ya hapana.
Pia alisema kuwa Katiba
Pendekezwa imeweza kuzingatia maoni ya
wananchi kwa asilimia 80 na kuwa haiwezekani hata siku moja katiba kuwa au
kusema kila kitu anachokihitaji mwananchi mmoja mmoja mfano watoto, wanawake,
vijana, wanaume au kusema kila jambo ambalo lipo nchini.
Katika hatua nyingine Katibu
Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Nassor Mnambila alisema kuwa tayari zimesambazwa
nakala za Katiba pendekezwa 54,300 katika mkoa wa Kagera kwa mchanganuo ufutao,
Halmashauri ya Wilaya Missenyi nakala 6,000 Karagwe nakala 6600, Kyerwa nakala 5400,
Manispaa ya Bukoba nakala 4200, Bukoba Vijijini nakala 8700.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya
Ngara nakala 6000, Muleba nakala 12900, na Biharamulo nakala 4500. Pia katika
kikao cha uzinduzi ziligawiwa nakala 132 ambazo zinakamilisha nakala 54,432 jumla
katika mkoa wa Kagera. Alisema pia nakala nyingine nyingi zaidi zitawasili hapo
baadae ili wananchi walio wengi waweze
kupata nakala hizo na kuzisoma.