Bukobawadau

SHIRIKA LA ICAP LAZINDUA MASHUA MPYA ZIWA VICTORIA KWA AJILI YA HUDUMA ZA UKIMWI

 Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera akikata utepe katika Uzinduzi wa Mashua mpya katika Ziwa Victoria iliyotolewa na shirika la ICAP kwa ajili ya huduma za UKIMWI kwa Wananchi waishio Visiwani.
Bukoba, Tanzania, (4 Februari 2015)  Shirika la Kimataifa la ICAP lililobobea katika huduma za Afya ya jamii, leo limezindua mashua mpya ya kitabibu ambayo itatumika kusaidia huduma za kinga, tiba na huduma za UKIMWI kwa jamii ya Watu wanaoishi katika Visiwa vya ziwa Victoria.
 Chombo hiki kimefadhiliwa na ICAP, kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Uongozi wa Afya Mkoa (RHMT), kama zawadi kwa Wananchi wa Mkoa wa Kagera, kwa hisani ya Watu wa marekani kupitia mfuko wa dharura wa Rais wa Kupambana na UKIMWI ulimwenguni (PEPFAR)
 Tangu mwaka 2004, ICAP imeshirikiana na Serikali ya Tanzania katika kusaidia mwitikio wa Taifa wa kupambana na UKIMWI; kama Mshirika wa Wizara ya Afya, na mpango wa Marekani wa kudhibiti magonjwa yaani Centers for Disease Control (CDC); ICAP hutoa ushauri wa kitaaluma katika ngazi zote za mfumo wa huduma za afya nchini ukiwemo utafiti, mafunzo na kuendeleza mpango wa huduma za UKIMWI na Kifua Kifuu. Katika ngazi ya Mkoa, ICAP hushirikiana na Uongozi wa Afya wa Mkoa (RHMT) na Hospitali zote, Maabara na Vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika mkoa wa Kagera, Kigoma, Pwani, Mtwara, Lindi na Zanzibar kwa ajili ya kupanua na kuboresha huduma za Kinga, Tiba na Huduma ya UKIMWI kwa ustawi wa Familia, Jamii na Makundi yote maalumu katika hatari ya maambukizi (Key populations).
 “Katika maeneo ya visiwa vya ziwa Victoria, kiwango cha maambukizi ya VVU na UKIMWI kiko juu zaidi kuliko katika maeneo ya nchi kavu, jambo linalochangiwa na uhaba wa huduma za VVU na UKIMWI” Hayo yamesemwa na Dr. Fernando Morales, Mkurugenzi mkazi wa ICAP Tanzania. “Mashua hii mpya, itasaidia kupanua huduma za kinga na tiba ya VVU na UKIMWI kwa Jamii yote ya visiwa vilivyomo katika Ziwa Victoria na kuisaidia Serikali kupiga hatua ili kufikia lengo la kuwa na kizazi kisicho na maambukizi ya VVU na UKIMWI”
Tanzania inakabiliwa na maambukizi ya ujumla, ambapo watu wapatao milioni 1.5 wanaishi na maambukizi ya VVU na UKIMWI (UNAIDS 2012). Inakadiriwa kuwa watu wapatao 150,000 huambukizwa VVU kila mwaka nchini (UNAIDS 2012). Katika mkoa wa Kagera, maambukizi ya VVU kati ya watu wazima ni asilimia 4.8, na Visiwa vya ziwa Victoria maambukizi yako juu zaidi.  
 Juhudi za serikali ya Tanzania pamoja na Wadau na Washirika wake, katika kupunguza maambukizi na vifo vitokanavyo na UKIMWI zimeonyesha matokeo yenye kutia moyo kwani maambukizi haya kwa sasa kitaifa yameshuka kutoka asilimia saba (7%) mwaka 2003/04 hadi kufikia asilimia tano (5%) katika mwaka 2011/12.
 Kuhusu ICAP
ICAP ni shirika la Kimataifa lenye wigo mpana katika utoaji huduma za afya ya Jamii, na lililobobea kwenye nyanja za Utafiti, mafunzo na program za utoaji huduma katika nchi takribani 21  ulimwenguni. Lilianzishwa mwaka 2004 na lenye makao yake katika Chuo Kikuu cha Columbia huko Marekani, ICAP imejizatiti kwa ajili ya kupambana na changamoto mbalimbali za kiafya kwa kuhakikisha ustawi wa afya za Familia na Jamii kupitia uboreshwaji wa mifumo ya huduma za afya kote ulimwenguni. Kwa kushirikianana Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali, ICAP hivi sasa inavisaidia vituo vya kutolea huduma za afya zaidi ya 3,380 pote ulimwenguni. Zaidi ya watu milioni 2 wamesaidiwa kupitia huduma hizi za ICAP ulimwenguni na watu wapatao milioni 1.2 wamepokea huduma za tiba ya UKIMWI.
 Kwa maelezo zaidi, tembelea www.icap.columbia.edu
 Mkurugenzi wa ICAP Mkoani Kagera Dr. Julius Zelithe akitoa utambulisho wa meza kuu kabla ya Ufunguzi rasmi wa shughuli ya Uzinduzi wa mashua mpya ya kitabibu ambayo itatumika kusaidia huduma za kinga, tiba na huduma za UKIMWI kwa jamii ya Watu wanaoishi katika Visiwa vya ziwa Victoria.
 Mkurugunzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Joseph Mkude akitoa salaam wakati wa utambulisho.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Mawasiliano na Ushauri wa ICAP nchini Tanzania Kate Raum akitoa neno
Hotuba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
 Msanii wa Kikundi cha Kakau band akiwajibika.
 Wadau mbalimbali wakifuatilia burudani
 Sehemu ya mashuhuda
 Wasanii wa ngoma ya asili ya Kabila la Wahaya 'Kakau Band', wakitoa burudani jukwaani wakati wa sherehe za Uzinduzi wa Mashua mpya
 Burudani ikiendelea
 Kakau band wakiendelea kushusha burudani
Matukio mbalimbali wakati wa burudani
Mashua hiyo inakabidhi Mkuu wa Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, Lembris Kipuyo anakabidhiwa rasmi mashua hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba akiongelea changamoto zilizopo katika Wilaya yake.
 Wilaya ya Muleba ina eneo la kilomita za mraba 10,739 na kati ya hizo kilomita za mraba 3,444 ni nchi kavu na kilomita za mraba 7,295 ni eneo la maji hususani Ziwa Victoria . Eneo la nchi kavu linahusisha pia zaidi ya visiwa ishirini vilivyomo katika Ziwa Victoria .
 Mshereheshaji wa Shughuli hii Mc Jane wa 88.5 Kasibante Fm Radio akiwajibika mbele ya DC
Dr. Julius Zelithe akiongea na wanahabari
 MWISHO KWA MATUKIO YA PICHA ZAIDI INGIA HAPA>>ICAP Yazindua Mashua mpya katika Ziwa Victoria
Next Post Previous Post
Bukobawadau