Bukobawadau

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:Chama cha Wazalendo (ACT - Tanzania )


Chama cha Wazalendo (ACT - Tanzania )
Kama mnavyo fahamu, Chama cha Wazalendo ACT-Tanzania kitafanya mkutano wake mkuu na uzinduzi wa chama mnamo tarehe 28 na 29 Machi 2015. Katika mkutano Mkuu chama kitapitisha katiba mpya ya chama na kufanya uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo Kiongozi wa chama, Mwenyekiti wa Chama, Makamu wenyeviti, Katibu Mkuu na Manaibu makatibu wakuu. Pia chama kitachagua wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.

Katika Uzinduzi wa chama tarehe 29 Machi 2015 kuanzia saa tisa alasiri, viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wamealikwa. ACT – Tanzania imemwalika Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, Mwenyekiti wa Taifa wa CUF kuzungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani nchini kuhusu ‘ kwanini Tanzania bado ni nchi masikini na nini cha kufanya kuondoa umasikini’. Pia viongozi wote wa vyama vya siasa nchini, mabalozi wa nchi mbalimbali na wakuu wa asasi zisizo za kiserikali wamealikwa. Uzinduzi utaonyeshwa moja kwa moja na vituo vya televisheni na radio kadhaa hapa nchini.

Mheshimiwa Samia Nkrumah, Kiongozi wa Chama cha CPP cha Ghana na mtoto wa Rais wa kwanza wa Ghana Osagyefo Kwame Nkrumah amealikwa pamoja na Mheshimiwa Ababu Namwamba, Katibu Mkuu wa chama cha ODM cha Kenya na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Kenya. Vile vile ACT – Tanzania inatarajiwa kupata wageni kutoka vyama rafiki vya Ujerumani Die Linke na Umoja wa vyama vya mrengo wa kushoto Progressive Alliance.

Baada ya Uzinduzi ACT Tanzania itafanya mikutano ya hadhara nchi nzima kwa kuanzia na mikoa ya Arusha, Shinyanga, Tabora, Kigoma na Mbeya. Jijini Arusha ACT – Tanzania itahuisha Azimio la Arusha na kuelezea mwelekeo wa kisera wa chama katika kujenga Tanzania mpya yenye kufuata misingi Usawa, Uzalendo, Uwazi, Uwajibikaji, Demokrasia na Uadilifu.

Abdallah Khamis,
Next Post Previous Post
Bukobawadau