MKOA WA KAGERA WAADHIMISHA SIKU YA KUPANDA MITI KITAIFA WILAYANI ‘MISSENYI MISITU NI MALI PANDA MITI'
Aprili Mosi kila mwaka huwa ni
siku ya kupanda miti kitaifa na mwaka huu 2015 mkoa wa Kagera ulipewa heshima
ya kuadhimisha siku hiyo ambapo iliadhimishwa katika Halmashauri ya Wilaya ya
Missenyi na kushirikisha wadau mbalimbali pamoja na wananchi wanaojihusisha na
kupanda miti na kutunza misitu.
Maadhimisho hayo yaliyoongozwa na mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Celestine
Gesimba kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo maadhimisho hayo yalianzia
katika Kijiji cha Bugolola eneo la Omukajunguti kwa kupanda miti 2100 kwa kushirikisha washiriki wote na wananchi wa kijiji hicho.
Kauli mbiu ya siku hiyo ilikuwa
ni “Misitu
ni Mali Panda Miti.” Katika Hotuba yake Naibu Katibu Mkuu Bw. Gesimba
alisema wizara yake siyo kwamba inahamasisha wananchi kupanda miti ili kulinda
mazingira tu bali wananchi wapande miti ili kunufaika nayo kwani ni mali
inayoingiza kipato kikubwa kwa mwananchi mmoja mmoja.
Bw. Gesimba alisema wananchi
wanatakiwa kupanda miti kwa wingi kwani miti isipopandwa itasababisha maafa
makubwa hapo mbeleni kama inavyoanza kuonekana kwa sasa mfano, ukosefu wa mvua
au mvua kutonyesha kwa wakati, joto jingi, kuyeyuka kwa theruji mlima Kilimanjaro.
Bw. Gesimba alimalizia hotuba
yake kwa kusema kuwa kutotunza misitu kumesababisha baadhi ya sehemu kuwa
jangwa au kusababisha ugonjwa wa malaria
mfano Lushoto mkoani Tanga ambako
hakukuwa na ugojwa huo miaka ya 1970 na 1990. Aidha alitahadhalisha misitu
kutoweka kabisa kwani kila baada ya dakika sita (6) nusu kiolmeta ya misitu
hutoweka duniani.
Bwana Jaffari Omary Afisa Misitu
katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa akitoa salaamu za mkoa wa Kagera alisema mkoa wa
Kagera una jumla ya misitu 17 yenye hekta 341,756.35 pia eneo la misitu na
vichaka ni kilometa za mraba 10,148 sawa na asilimia 35 ya nchi kavu ya mkoa
mzima.
Mkoa wa Kagera una misimu miwili
ya upandaji miti, msimu wa vuli ambapo wananchi hupanda miti kwa wingi kutokana
na msimu huo kuwa na mvua za kutosha pia na msimu wa masika ambapo nao hutumika
kupanda miti kwa wingi, alifafanua Bw. Jaffari Omary .
Meneja wa Wakala wa Huduma za
Misitu Kanda ya ziwa Bw. Haji Khatibu akitoa salaam za Kanda ya Ziwa alisema
kuwa kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 2003 Kanda ya Ziwa ilionekana kuwa misitu imebakia mapori
tu kutokana na uchomaji moto ovyo,
mifugo mingi na wananchi kutoshiriki kuitunza misitu, uchomaji mkaa, kilimo na
uvunaji wa mbao usiozingatia kanuni na taratibu.
Aidha Bw. Khatibu alisema uharibifu wa miti
unachangiwa pia na sera mbalimbali kuingiliana na alitoa mfano katika
halmashauri za Wilaya kutoa maeneo ya hifadhi za misitu kwa wananchi kama
viwanja vya kuishi na kuendesha kilimo jambo ambalo linapelekea uharibifu
mkubwa katika maeneo hayo ya hifadhi.
Ili kukabiliana na changamoto
hizo na kuzipatia ufumbuzi Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kuwahasisha
wananchi kushiriki katika kuilinda na kuitunza misitu kupita serikali zao za
vijiji na vitongoji pamoja na mwananchi mmoja mmoja kutoshiriki katika vitendo
ovu vya kuharibu misitu.
Aidha serikali imekuwa ikiendesha
doria katika maeneo ya hafadhi za taifa ili kukabiliana na uvamizi wa maeneo
hayo pia kukamata mazao ya misitu ambayo yanavunwa bila kuzingatia sheria,
taratibu na kanuni za uvunaji na
kuwachukulia hatua kali wahusika wanaokamatwa.
Mwenyekiti wa halmashauri ya
Wilaya ya Missenyi William Katunzi akitoa shukrani zake kwa Wizara ya Maliasili
na Utalii kwa kuadhimisha siku ya kupanda miti kitaifa Wilayani missenyi
alisema tayari kwa mkoa wa Kagera wananchi wanajua nini maana ya kupanda miti
kwa sasa, wapanda miti kibiashara ili kujipatia kipato pia kulinda mazingira.
Takwimu za upandaji na utunzaji
wa miti katika mkoa wa Kagera kwa miaka minne
mfululizo; mwaka 2011/2012 lengo la kupanda lilikuwa miti 12,500,000 Miti
iliyopandwa ni 13,100,875 sawa na asilimia 105, Miti iliyopona ni 11,220,328
sawa na asilimia 89.7. Mwaka 2012/2013
lengo la kupanda lilikuwa miti 12,500,000 Miti iliyopandwa ni 12,755,042 sawa
na asilimia 102, Miti iliyopona ni 11,081,519 sawa na asilimia 88.
Aidha mwaka 2013/2014 lengo la kupanda lilikuwa miti 13,000,000
Miti iliyopandwa ni 13,767,022 sawa na asilimia 85, Miti iliyopona ni
11,248,933 sawa na asilimia 88.4. Na mwaka
2014/2015 lengo la kupanda lilikuwa miti 13,000,000 Miti iliyopandwa ni
12,278,125 sawa na asilimia 98.4, Miti iliyopona ni 11,153,627 sawa na asilimia
90.8