MKUU WA MKOA WA KAGERA AKITEMBELEA KIWANDA CHA KAGERA SUKARI KUJIONEA UTEKELEZAJI WA MATOKEO MAKUBWA SASA KATIKA KILIMO
Katika mpango wa Matokeo Makubwa
Sasa (Big Results Now) kitaifa unaolenga kuinua uchumi wa nchi kupitia sekta
mbalimbali za kilimo, Maji, Elimu na Miundombinu mkoa wa Kagera nao umelenga kuinua uchumi wake kupitia sekta hizo kwa kuweka mikakati mbalimbali za
kuutekeleza mpango huo.
Katika kutekeleza mpango wa Matokeo Makubwa Sasa mkoa wa Kagera ulichagua
zao la biashara la miwa linalozalisha sukari kama zao litakalolimwa na kutoa
matokeo makubwa kwa haraka kwa kuinua uchumi wa mkoa na wananchi mmoja mmoja.
Zao la miwa siyo geni katika mkoa
wa Kagera kwani linalimwa zaidi Wilayani Missenyi ambako kuna kiwanda cha
wawekezaji wanaoendesha kilimo hicho kwa teknolojia ya kisasa na kuzalisha
sukari. Kwa sasa kiwanda hicho kimeweza kulima hekta 12,000 katika udongo wenye rutuba.
Pamoja na kiwanda cha Kagera
Sukari kuwekeza katika kilimo cha miwa
Wilayani Missenyi mkoani Kagera lakini pia wakulima mbalimbali
(Outgrowers) katika Wilaya hiyo nao wanaendelea kulima miwa na kukiuzia kiwanda
hicho ili kuongeza uzalishaji wa sukari.
Katika kuchochea uwekezaji na
kuwahimiza wananchi na kiwanda cha Kagera Sukari kulima miwa kwa mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa Mkuu wa mkoa wa Kagera Mhe. John mongella alitembelea
kiwanda hicho ili kujionea uwekezaji na mikakati ya kiwanda hicho kikishirikiana
na wakulima wa nje katika kutekeleza kilimo cha miwa.
Katika ziara hiyo aliyoifanya
Mhe. Mongella katika kiwanda cha Kagera Sukari tarehe 30 Marchi, 2015 alijionea
jinsi sukari inavyozalishwa kiwandani hapo kuanzia hatua ya kwanza mpaka mwisho
aidha alitembelea mashamba na kujionea jinsi uongozi wa kiwanda hicho
unavyolima kisasa mbegu na aina mbalimbali
za miwa.
Aidha katika taarifa yake Meneja
Mkuu wa Kiwanda cha Kagera Sukari Bwana Ranna alisema kiwanda hicho mpaka sasa
kimeweza kuwekeza katika kilimo cha kisasa cha miwa katika hekta 12,000 na
kutoa ajira zaidi ya 4,000 kwa wananchi wa mkoa wa Kagera na kutoka nje ya mkoa
wa Kagera.
Katika kutekeleza mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa Bw. Ranna alisema tayari wameanza maandalizi upanuzi wa mashamba katika eneo la Kitengule
ng’ambo ya mto Kagera kwa kuanza na utafiti wa kina kuhusu udongo wa eneo hilo
kuona kama unafaa katika kilimo cha miwa.
Vilevile Meneja mkuu wa Kagera
Sukari aliiomba serikali kutengeneza miundombinu ya barabara katika mashamba ya
wakulima wa nje ili kurahisisha uvunaji na usafirishaji wa miwa kutoka katika
mashamba hayo hadi kiwandani.