TAMKO LA UKAWA KUHUSU; UCHAGUZI MKUU, KURA YA MAONI NA MWAFAKA WA MAJIMBO
UMOJA WA KATIBA YA
WANANCHI (UKAWA),
DAR ES SALAAM,
TANZANIA.
TAARIFA KWA UMMA,
DAR ES SALAAM, ALHAMIS, 30
APRIL 2015
UCHAGUZI
MKUU OKTOBA 2015 LAZIMA, KIKWETE ASIONGEZEWE MUDA, KURA YA MAONI BAADAE
Vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) leo vimetoa msimamo wao juu ya
njama za kuahirisha Uchaguzi Mkuu unaotakiwa kufanyika Oktoba mwaka huu. UKAWA
imesisitiza kwamba kuahirisha Uchaguzi Mkuu huo ni sawa na kumuongezea Rais
Jakaya Kikwete na Chama chake cha Mapinduzi muda wa kuendelea kutawala
Tanzania. UKAWA imesema jaribio lolote la kuahirisha Uchaguzi Mkuu kwa
kisingizio chochote kile litakuwa kinyume na Katiba ya sasa ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na litahesabika kuwa ni sawa na mapinduzi dhidi ya Katiba
(constitutional coup d’etat). Msimamo wa UKAWA unafuatia kumalizika kwa Kikao
cha Viongozi Wakuu wa Vyama vinavyounda UKAWA (UKAWA Summit) kilichofanyika
katika Makao Makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), jijini Dar es Salaam kati ya
tarehe 28 na 29 Aprili mwaka huu.
Akielezea
msimamo wa UKAWA juu ya suala hili, mwenyeji wa Kikao hicho na Mwenyekiti wa
CUF Profesa Ibrahim Lipumba alisema kwamba kuna dalili za kuonyesha kwamba zipo
njama za kuahirisha Uchaguzi Mkuu na kumuongezea Rais Kikwete na CCM muda wa
kutawala. “Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijaanza maandalizi yoyote kwa
ajili ya Uchaguzi Mkuu licha ya kwamba imebaki miezi sita tu Uchaguzi huo
ufanyike kwa mujibu wa Katiba. Shughuli zinazohusiana na maandalizi ya Uchaguzi
Mkuu na vifaa vinavyotumika kwa ajili yake ambavyo kwa taratibu za miaka yote
huanza kufanyika angalau mwaka mmoja na nusu kabla ya Siku ya Uchaguzi
hazijaanza kufanyika, vifaa vinavyohitajika havijanunuliwa na fedha kwa ajili
hiyo hazijatengwa hadi sasa.”
Profesa
Lipumba aliongeza kwamba jambo hili limefanyika kwa makusudi kwa sababu vyama
vya UKAWA vimekuwa vinapigia kelele suala la maandalizi ya Uchaguzi Mkuu tangu
mwaka 2012. “Licha ya madai ya muda mrefu ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
kwamba ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 imevurugwa kwa makusudi kwa kutokutenga
fedha kwa ajili hiyo katika bajeti ya Serikali tangu mwaka 2012, Serikali hii
ya CCM haijatoa fedha kwa NEC kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu. Badala yake, NEC
imeendelea kutangaza kwamba inafanya maandalizi kwa ajili ya Kura ya Maoni
kuhusu Katiba Inayopendekezwa ambayo imepitwa na muda kisheria na haiwezi
kufanyika tena bila kwanza kufanyika kwa marekebisho katika Sheria ya Kura ya
Maoni (the Referendum Act) ya mwaka 2013.”
Kwa
mujibu wa Profesa Lipumba, Kura ya Maoni ilitakiwa ifanyike ndani ya siku 124
kutoka tarehe Rais Kikwete alipotoa Tangazo la Kura ya Maoni na kutamka kuwa
Kura hiyo itafanyika tarehe 30 Aprili, 2015, yaani leo. Profesa Lipumba
alisema: “Kwa Sheria ya Kura ya Maoni ilivyo kwa sasa, hakuna uwezekano wa Kura
ya Maoni kufanyika tena bila kwanza kufanya marekebisho ya Sheria hiyo. Kila
hatua inayotakiwa kuchukuliwa chini ya Sheria hiyo imewekewa muda wake na muda
huo haubadiliki. Tangazo la Kura ya Maoni likishatolewa na tarehe kutangazwa
haibadilishwi kwa sababu yoyote ile. Hakuna namna yoyote ya kuahirisha Kura ya
Maoni na kuifanya tarehe nyingine yoyote.”
Profesa
Lipumba aliongeza: “Haya ndio masharti ya Sheria ya Kura ya Maoni. Yasipofuatwa
hakuna namna ya kuyarekebisha bila kwanza kurekebisha Sheria yenyewe. Na hadi
sasa Serikali hii ya CCM haijapeleka Muswada wa Sheria kuirekebisha Sheria hiyo
ili kuwezesha Kura ya Maoni kufanyika kwa tarehe nyingine. Tunashangazwa na
Tume inayoongozwa na aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ambayo ndio mahakama
ya juu kabisa katika nchi yetu, na Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye ni Mwanasheria
Mwandamizi wa Serikali, kuendelea kutangaza kwamba Kura ya Maoni itafanyika kwa
terehe itakayotangazwa baadae wakati Tume inafahamu kwamba jambo hilo
haliwezekani kisheria. Kama bado CCM na washirika wake wanataka Katiba
Inayopendekezwa ipigiwe Kura ya Maoni na Watanzania ni lazima wapeleke Muswada
wa Marekebisho ya Sheria ya Kura ya Maoni Bungeni. Vinginevyo itakuwa na
ubatilifu mtupu kama tuliouona wakati wa Bunge Maalum.”
Aidha,
UKAWA imesema haiko na haitakuwa tayari kuunga mkono jitihada zozote za
kumuongezea Rais Kikwete na CCM muda wa kutawala kwa kuahirisha Uchaguzi Mkuu
wa mwaka huu. Kwa mujibu wa Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA na Mwenyekiti wa Chama
cha NCCR-Mageuzi, Mheshimiwa James Mbatia, haijawahi kutokea Uchaguzi Mkuu
ukaahirishwa kwa sababu yoyote tangu mwaka 1960 tulipofanya Uchaguzi Mkuu
uliotupatia Serikali ya Madaraka ya Ndani hadi sasa.
Mheshimiwa
Mbatia alisema: “Watu hawa wanafahamu kuwa tumekuwa tukifanya Uchaguzi Mkuu
kila baada ya miaka mitano tangu mwaka 1960. Hata mwaka 1980, miezi michache
baada ya kutoka vitani dhidi ya nduli Iddi Amin wa Uganda na licha ya Baba wa
Taifa Mwalimu Nyerere kutangaza miezi 18 ya kujifunga mikanda kwa sababu ya
hali mbaya ya uchumi iliyosababishwa na Vita ya Uganda, hatukuahirisha Uchaguzi
Mkuu wa mwaka huo. Watu hawa wanafahamu kwamba Katiba yetu hairuhusu Uchaguzi
Mkuu kuahirishwa kwa sababu yoyote ile. Wanafahamu kwamba tangu mwaka 1985,
Rais anatakiwa atumikie vipindi viwili tu vya miaka mitano mitano. Wanafahamu
kwamba maisha ya Bunge ni miezi sitini au miaka mitano kuanzia tarehe ya
Uchaguzi Mkuu na haiwezekani kwa maisha hayo kuongezewa muda kikatiba bila ya
kufanyika Uchaguzi Mkuu. Na wanafahamu kwamba Rais Kikwete anakamilisha kipindi
chake cha pili mwezi Oktoba mwaka huu na maisha ya Bunge la Kumi yanamalizika
mwezi huo. Kuruhusu Uchaguzi Mkuu uahirishwe kwa kisingizio chochote kile ni
kuwazawadia wazembe na kuwaongezea mafisadi wanaolimaliza taifa letu kwa
ufisadi muda wa kuendelea na ufisadi huo. UKAWA haitakubali kuruhusu jambo hilo
litokee.”
Aidha,
UKAWA imesisitiza kwamba haitakubali na haitaunga mkono jaribio lolote la
kufanya marekebisho katika Katiba ya sasa kwa lengo la kumuongezea Kikwete,
chama chake na Serikali muda wa kutawala. Akielezea msimamo huo, Mwenyekiti
Mwenza wa UKAWA na Mwenyekiti wa chama cha National League for Democracy (NLD)
Dkt. Emmanuel Makaidi amesisitiza kwamba suala la vipindi viwili vya miaka
mitano mitano kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ni nguzo kuu muhimu ya Katiba ya
sasa na UKAWA haitakubali nguzo hiyo iguswe au kufumuliwa kwa sababu au
kisingizio chochote kile. Dkt. Makaidi alisema: “Kubadilisha Katiba ya sasa kwa
lengo la kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka sio tu kutaathiri misingi
muhimu ya Katiba ya sasa, bali pia kutahatarisha amani ya nchi yetu. Tumeona
kinachoendelea Burundi baada ya Rais Pierre Nkurunzinza na chama chake kuamua
kujiongezea muda wa kutawala nchi hiyo. Tumeona yanaoendelea Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC) baada ya Joseph Kabila kutaka kufanya hivyo hivyo.
Kikwete na wanaCCM wenzake wasitake kuiingiza nchi yetu katika majanga
yasiyokuwa na sababu.”
Kwa
upande mwingine, UKAWA imeitaka NEC kuhakikisha kwamba wananchi wote wenye sifa
ya kuandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanaandikishwa kwenye
Daftari hilo. Katika Mkutano wake na vyama vya siasa uliofanyika Dar es Salaam
tarehe 9 Julai mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume Jaji Damian Lubuva alisisitiza
kwamba NEC ilikuwa na uwezo na vifaa vya kuandikisha takriban wapiga kura milioni
24 katika vituo vya kuandikishia 40,000 nchi nzima kwa muda wa siku 14 katika
kila kituo cha kuandikishia. Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA na Mwenyekiti wa
CHADEMA Mheshimiwa Freeman Mbowe alieleza kushangazwa kwa UKAWA na matamko ya
Tume kwamba sasa Tume itaandikisha wapiga kura kwa muda wa siku saba katika
kila kituo.
Mwenyekiti
Mbowe alisema: “Tume iliwaahidi Watanzania kwamba watu wote wenye sifa
wataandikishwa katika Daftari la Wapiga Kura. Sisi wa UKAWA tulishauri muda wa
kuandikisha uongezwe hadi angalau siku 28 kama ilivyokuwa kwa Uchaguzi Mkuu
uliopita lakini Tume iling’ang’ania kwamba muda wa siku 14 unatosha. Leo Tume
inapunguza muda huo wakati tunafahamu kwamba Tume ina vifaa pungufu vya
kuandikishia wapiga kura kuliko ilivyoomba kupatiwa na Serikali hii ya CCM. Hii
ni njama ya Tume na ya Serikali hii ya CCM kuhakikisha wapiga kura wengi
hawaandikishwi. Sisi UKAWA hatutakubali jambo hilo litokee.”
Wakati
huo huo, Viongozi Wakuu wa UKAWA wameeleza kushangazwa na taarifa
zilizosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kwamba Chama cha
NCCR-Mageuzi kimejitoa au kimeandika barua ya kuomba kujitoa kwenye UKAWA.
Viongozi hao wamesema kwamba taarifa hizo ni uzushi mtupu unaosambazwa na
wapiga ramli na wanajimu wa kiama cha UKAWA kwa lengo la kuipatia CCM na vyama
vibaraka wake ahueni ya kisiasa. Akikanusha taarifa hizo, Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi Mheshimiwa Mbatia amesema kwamba yeye mwenyewe na Katibu Mkuu wake
Mosena Nyambabe pamoja na maafisa wa chama chake wamekuwa katika hatua zote za
vikao vya UKAWA kuanzia Kamati ya Ufundi na ile ya Wataalam hadi Kikao cha
Viongozi Wakuu kilichomalizika jana.
Mheshimiwa
Mbatia alisisitiza: “Tangu juzi tupo hapa tukijadiliana namna ya kupata
wagombea wa UKAWA wa ngazi zote kuanzia Urais, Ubunge hadi Udiwani. Kwa kiasi
kikubwa tumeshakamilisha kazi ya kupata wagombea Ubunge wa UKAWA. Tumeshapata
muafaka kwa zaidi ya asilimia 95 ya majimbo yote ya Uchaguzi Tanzania, na
majimbo 12 yaliyobakia tunaendelea kuyashughulikia na tutayapatia ufumbuzi muda
si mrefu. Tunaendelea na majadiliano juu kupata Mgombea Urais na Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano atakayepeperusha bendera ya UKAWA. Tumeshakamilisha kazi
hiyo kwa upande wa Zanzibar na tutaikamilisha kwa upande wa Jamhuri ya Muungano
katika muda muafaka. UKAWA iko imara sasa kuliko kipindi kingine chochote tangu
Bunge Maalum mwaka jana. Hao wanaosambaza uzushi kwamba tumefarakana na kwamba
sisi NCCR tumejitoa au tunataka kujitoa watafute hoja nyingine. Hii imebuma.”
Mungu Ibariki Tanzania!
Imetolewa na;
---------------------------------------
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba,
Mwenyekiti – CUF – Chama Cha Wananchi,
-----------------------------------
Mh.Freeman Mbowe (MB),
Mwenyekiti - CHADEMA
--------------------------------------
Mh.James Francis Mbatia(MB),
Mwenyekiti – NCCR MAGEUZI.
--------------------------------------
Mh.
Dkt. Emmanuel Makaidi
Mwenyekiti – NLD.