Bukobawadau

HALMASHAURI ZOTE NCHINI KUJENGEWA UWEZO WA KUKABILIANA NA MAAFA


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Florens Turuka akiongea na wajumbe wa wa Baraza la Wafanyakazi  Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa mkutano huo, Jijini Dar es Salaam, tarehe 4 Mei, 2015.
 Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi   Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia mkutano huo Jijini Dar es Salaam, tarehe 4 Mei, 2015. (wa kwanza) ni Naibu Katibu  Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Regina Kikuli.
 Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi  la Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia mkutano huo Jijini Dar es Salaam, tarehe 4 Mei, 2015. 
 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Florens Turuka (mwenye tai nyeupe ) akiwa na wajumbe wa  Baraza la Wafanyakazi  wa Ofisi ya Waziri Mkuu mara baada ya kufungua mkutano huo , Jijini Dar es Salaam, tarehe 4 Mei, 2015.

Na Mwandishi Maalum
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imesema kuwa katika jitihada za kukabiliana na athari za maafa nchini,  imejipanga katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2015/2016 kujenga uwezo wa kukabiliana na maafa kwa Halmashauri zote nchini kupitia mafunzo ya kukabiliana na maafa pamoja na kuandaa Mipango ya Kujiandaa Kukabili Maafa katika Halmashauri  zote nchini.
Ofisi ya Waziri Mkuu imeshazijengea uwezo wa kukabiliana na maafa  Halmashauri za mikoa mitano nchini kwa  kuandaa Mipango ya kukabiliana na maafa pamoja na kufanya zoezi la mezani la utekelezaji wa mipango hiyo kwa Halmashauri zake; Mikoa hiyo ni;  Dodoma, Shinyanga, Simiyu, Kilimanjaro na Mtwara.
Akiongea mara baada ya kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Jijini Dar es Salaam, tarehe 4, Mei 2015, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Florens Turuka alisema  kila Halmashauri inayo majanga ambayo huisumbua mara kwa mara lakini kwa kutumia mafunzo na Mipango ya kukabiliana na maafa zinaweza kuyakabili maafa zenyewe.

“Mafunzo ya maafa yanaweza kuiwezesha jamii kupata  elimu kuhusu athari za ujenzi na kuendesha shughuli za uchumi katika maeneo hatarishi, umuhimu wa usafi wa mazingira matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame pamoja na kuzuia ujenzi katika maeneo hatarishi hivyo Majanga ya mafuriko, Ukame, na mlipuko wa kipindupindu  ambayo yamekuwa yakizisumbua Halmashauri zetu mara kwa mara yanaweza kukabiliwa kwa uwezo wa Halmashauri husika” alisema Turuka.
Turuka aliongeza kuwa pamoja na kuwa na mafunzo ya namna ya kukabiliana na maafa, aidha halmashauri hazinabudi  kulipa kipaumbele suala la Kupunguza Athari za Maafa katika  mipango na programu za maendeleo.
“Halmashauri zinaweza kupunguza utegemezi wa rasilimali za kukabili maafa, kwa kuondokana na mtazamo wa kukabili maafa uliozoeleka ambao unatenganisha kwa kiasi kikubwa hatua za utoaji wa misaada ya kibinadamu, kurudisha hali na shuguli za kawaida za maendeleo. Kwa mantiki hii Halmashauri zetu nchini kupitia  mafunzo ya maafa zitaweza kuondokana na mtazamo huo uliozoeleka ” alisisitiza Turuka.
Aliongeza kuwa nchi yetu imekuwa ikikumbwa na majanga yakiwemo ya asili na yanayosababishwa na vitendo vya binadamu. Katika kukabili maafa hayo yamekuwa yakijitokeza mapungufu katika Halmashauri za hapa nchini, ikiwemo kutokuwepo mipango madhubuti iliyoandaliwa ya kukabiliana na maafa mara yanapotokea.
Alifafanua kuwa kila Halmashauri inaweza kuwa na uwezo wa kukabili maafa yanayoikumba kwa kuwa na jamii yenye kuhimili maafa kwa Kuzuia, kupunguza athari  na kujiandaa kama vipaumbele katika menejimenti ya maafa katika ngazi zote. Ili kuhakikisha kunakuwa na jamii hiyo, kila Halmashauri inapaswa kukaa na wadau wote katika halmashauri husika na kuainisha maeneo ya kushughulikia kwa haraka na kuwa  na mgawanyo bayana wa majukumu.
Next Post Previous Post
Bukobawadau