Bukobawadau

WADAU WA KAHAWA MKOANI KAGERA WAPEWA CHANGAMOTO YA KUANZISHA MNADA KAHAWA WA KAGERA ILI KUBORESHA BEI KWA WAKULIMA

Mkuu wa Mkoa wa Kagera  Mhe. John Mongella atoa changamoto ya kuinua ubora wa zao la kahawa na kuimarisha bei yake ili kumuinua mkulima wa Kagera, wakati akifungua Kikao cha wadau wa Kahawa  kanda ya Kagera kutoka katika Halmashauri zote za mkoa wa Kagera kilichofanyika katika mkoani hapa Mei 8, 2015.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Mongella katika mkutano huo aliwataka wadau wa kahawa kutoka katika mkoa wa Kagera kuachana na mifumo ya kizamani ambayo imekuwa wimbo wa kila siku katika utatuzi wa kudhibiti magendo ya kahawa na kuimarisha bei kwa wakulima ili kuinua uchumi wa mkoa na taifa.
Wadau wa kahawa wa Kagera walipewa changamoto ya kuanzisha mnada wa kahawa yao ya Kagera badala ya kutegemea mnada wa Moshi mkoani Kilimanjaro ambao unaongeza gharama na kumpunguzia mkulima bei jambo linalowafanya wakulima kuuza kahawa kwa njia za magendo.
Aidha Mhe. Johna Mongella aliishangaa Bodi ya Kahawa Tanzania kukata kilo 10 kila kilo 60 kutoka kwa mkulima kwa ajili ya kupeleka kwa wanunuzi kupima ubora wa kahawa ambapo alisema robo kilo inatosha sana kupima ubora lakini Bodi ya Kahawa imekuwa ikiwadhoofisha wakulima bila sababu.
Pia Mhe. Mongella aliwataka wakulima kubadilika na kuanzisha mashamba mapya  kwa kupanda miche yenye ubora na inayoweza kuzalisha kahawa kwa wingi kuliko ilivyo sasa ambapo mashamba mengi yamekuwa kama misitu na miche ni ya zamani nambapo hayahudumiwi ipasavyo ili kuzalisha kahawa bora.
Kwa upande wa wadau wa kahawa katika kikao hicho walizilalamikia  Halmashauri za Wilaya kwa kutoza kiwango kikubwa cha tozo au ushuru katika zao la kahawa jambo ambalo linapelekea kushusha bei ya kahawa hasa kwa mkulima.
 Kahawa kavu
Wadau hao waliziomba Halmashauri za Wilaya kupunguza tozo au ushuru  katika zao la kahawa aidha waliiomba serikali pia kupunguza viwango vya fedha zinazotozwa katika leseni na kupunguza wingi wa leseni ambazo zimekuwa kero kwa wanunuzi wa kahawa na kupelekea gharama kwenda kwa wakulima.
Changamoto kubwa iliyojitokeza katika kikao hicho ni kuhusu magendo ya kahawa mkoani Kagera ambapo wakulima walio wengi wanauza kahawa yao kwa njia za magendo na sababu kubwa ikiwa ni bei ndogo inayotolewa na wanunuzi wa hapa nchini lakini nchi jirani wananunua kahawa kwa bei ya juu.
Wanunuzi wa Kahawa wakizungumzia kuhusu kutoa bei ndogo ya kahawa walisema kuwa inatokana na mwenendo wa bei katika soko la dunia ambapo bei ikiwa nzuri na wao wananunua kahawa kwa wakulima kwa bei nzuri ambayo inayoridhisha  na bei ya soko ikishuka na wao wananunua kulingana na bei hiyo.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa wadau kuweka maazimio ya kuhakikisha kila mdau wa kahawa anahusika katika kudhibiti uuzaji wa kahawa kwa njia za magendo ili kuingiza mapato katika Halmashauri za mkoa wa Kagera na taifa kwa ujumla kuliko kunufaisha uchumi wan chi jirani.

Next Post Previous Post
Bukobawadau