Bukobawadau

WAKODI WANAUME KUTOKA NCHINI KENYA


Rombo. Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Lembris Kipuyo amesema tatizo la ulevi kupindukia wilayani humo, limewaathiri wanaume kiafya na kuwataka watendaji kulivalia njuga.

Kutokana na ulevi huo, kuna madai kuwa baadhi ya wanawake wanaoishi kwenye ndoa wilayani huo, wamelazimika kutafuta wanaume nchi jirani ya Kenya ili wapate mimba kutokana na waume wao kuzidiwa na ulevi, hivyo kushindwa kuwahudumia.

Kipuyo alisema tatizo la ulevi wilayani humo limefikia hatua ya hatari zaidi na jitihada za haraka zinahitajika.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo, Kipuyo alilitaja eneo lililozidiwa na ulevi kuwa ni Kikelelwa lililopo Tarakea, mpakani mwa Tanzania na Kenya.

“Tatizo la ulevi wilayani Rombo na matumizi ya pombe zisizokuwa na viwango ni kubwa sana na linahitaji nguvu ya pamoja kulikabili,” alisema na kuongeza:

“Imefikia mahali wanaume wengi wanashindwa kumudu kufanya tendo la ndoa na kuwalazimu wanawake wao kukodi wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya tendo hilo.”
Alisema ni vizuri mamlaka husika, zikiwamo Serikali za vijiji kuhakikisha ulevi unakwisha ili kuepuka Tarakea kuwa kizazi cha Wakenya.

Alisema kuwa viongozi na watendaji wakisimamia vyema suala hilo, unywaji wa pombe hasa zile zisizokuwa na viwango litakwisha.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Anthony Tesha alisema viongozi wameshindwa kukemea suala la ulevi na badala yake wameliacha suala hilo kwenye ofisi yake.
Tesha alisema watendaji kwa kushirikiana na madiwani wana uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha Rombo inaondokana na ulevi.
CHANZO;MWANANCHI
Next Post Previous Post
Bukobawadau