Bukobawadau

WANANCHI WAISHUKURU SERIKALI KUWAJENGEA UWEZO WA KUKABILIANA NA MAAFA YA UKAME

Mkazi wa kijiji cha Mgwasi wilayani Same, John Samuel akiwaangalia mbuzi wake aliowapata kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia mradi wa Kupunguza Athari za Ukame unaofadhiliwa na UNICEF,  tarehe 31, Mei 2015.
 Timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ikimsikiliza katibu wa kikundi cha Kavangere, Neema Mohamed (wa pili kulia), juu ya ufugaji wa kuku unaofanywa na kikundi hicho kijijini Mgwasi wilayani Same, kuku hao wamewapata kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia mradi wa Kupunguza Athari za Ukame unaofadhiliwa na UNICEF,  wakati wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi huo  tarehe 31, Mei 2015.
 Mratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Harrison Chinyuka (mbele) akifuatiwa na mwenyekiti wa kikundi cha Kavengere, kijijini Mgwasi wilayani Same, Stephano Hamisi na wakaguzi Hesabu za Serikali , Ofisi ya Mkaguzi Mkuu  Hesabu za Serikali nchini, wakikagua shamba la kikundi hicho wakati wa ufuatiliaji wa utekelezaji mradi wa Kupunguza Athari za Ukame unaratibiwa na  Ofisi ya Waziri Mkuu,  tarehe 31, Mei 2015.


Na. Mwandishi Maalum
Wananchi wa Wilayani  Same katika  kata ya Hedaru, Makanya na Vunta wameishukuru serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya uratibu maafa, kwa kuwajengea uwezo wa kuzuia, kupunguza na kukabiliana na maafa yanayotokana na ukame ambao umekuwa ukizisumbua kata hizo Kutokana na mabadiliko ya Tabia Nchi.
Idara ya uratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Mradi wa kujengea jamii uwezo wa kukabili maafa ya ukame imefanikiwa kujenga uwezo huo kupitia vikundi vya maendeleo vya wilayani humo, ikiwa vikundi kumi (10) kutoka kata tatu za wilaya hiyo vimepatiwa  Mbuzi 40, kuku 50, mbegu za mihogo, viazi, mtama, mboga mboga pamoja na kutoa miche ya miti kwa shule moja kila kata na vifaa vya kutunza bustani.  
Akiongea wakati Idara hiyo ilipokuwa ikifuatilia utekelezaji wa mradi huo hivi karibuni,  wilayani humo katika kata ya Makanya,  kijijini  Mgwasi, Mwenyekiti wa kikundi cha Kavangere, Stephano Hamisi, alieleza kuwa wananchi wa kata hiyo kupitia ufadhili wa mradi huo wameweza  kulima na kufuga hali inayowajengea uwezo wa  kupunguza na kukabiliana na maafa yanayotokana na ukame
 “Tunaishukuru serikali kwa mradi huu,  kwani tunao uwezo wa kuzuia, kupunguza na kukabiliana na maafa yanayotokana na ukame kwa kuwa tulipewa mbegu za mazao yanayo himili ukame na yanayo stawi haraka kwa kipindi kifupi cha mvua, kwa mantiki hiyo tunao uhakika wa chakula lakini pia uhakika wa kipato kwa  kilimo cha bustani, ufugaji wa mbuzi na kuku ambazo tumewezeshwa na mradi huu ” alisema Hamisi.
Aliongeza kuwa katika vikundi ambavyo vimewezeshwa na mradi huo wanao utaratibu wa kila mwana kikundi kupata mbuzi (5) na wengine ambao hawapati mbuzi hupewa kuku (5) ambapo wanakikundi hubadilishana mifugo hiyo kwa kadri wanavyo endelea kuzaliana lengo likiwa ni kila mwanakikundi kufuga mbuzi pamoja na kuku.
Mratibu maafa wilayani Same, Ally mngwaya anaeleza kuwa mradi huo umeweza pia kuzijengea jamii uwezo wa kuzuia maafa ya ukame kwa kuhamasisha upandaji miti, ambapo shule za wilayani humo zimeshirikishwa ili kujenga kizazi chenye uwezo wa kukabiliana na kupunguza vihatarishi vinavyoweza kusababisha maafa ya ukame katika kata zao.
“ Kwa kata tatu zinazofadhiliwa na mradi huu tumechagua shule moja kila kata na tayari viriba vya miche 2500 vimegawiwa katika shule za wilaya hii ikiwa lengo ni kufikia miche 5000. Tukipanda miti ya kutosha katika kata hizi na tukaachana na  shughuli za kibinadamu zinazochangia sana kutokea kwa ukame kama ukataji na uchomaji wa miti ovyo na uharibifu wa vyanzo vya maji, ninaamini tutakuwa na uwezo mkubwa wa kuzuia, kukabili na kupunguza athari zitokanazo na ukame” alisisitiza Mngwaya.
Awali akiongea katika kata hizo, Mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Mradi huo, Harrison Chinyuka alifafanua kuwa mradi huo umefanikiwa kuwajengea uwezo wananchi  wilayani Same kwa kuwa umewatumia  wataalam waliopo katika ngazi ya Kata za wilaya hiyo katika   kuijengea uwezo jamii hiyo  wa kuzuia, kupunguza na kukabiliana na maafa yanayotokana na ukame.
“katika kutekeleza mradi huu tumewatumia  wataalam wa Sekta ya Kilimo, Mifugo, Afya, Elimu na Utawala wa kata za wilaya hii kwani wataalamu hawa wapo karibu na jamii inayopata athari za ukame, kupitia wataalamu hawa jamii hii imeweza  kuelewa vihatarishi vinavyoweza kusababisha maafa ya ukame na  matumizi ya mbegu na pembejeo za kilimo, mifugo na misitu pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu na mifugo”  alisema Chinyuka.
Mradi Wa Kuijengea Jamii Uwezo Wa Kupunguza Athari Za Maafa Kwa Mikoa Iliyoathirika Zaidi Na Ukame umefadhiliwa na Benki ya Dunia na kusimamiwa na UNICEF chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu Maafa, na Halmashauri husika wakiwa Watendaji Wakuu wa Mradi huo. Mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 uliozinduliwa Wilayani  Same, mkoani Kilimanjaro tarehe 11 Desemba 2013.
 -Mwisho-
Next Post Previous Post
Bukobawadau