Bukobawadau

150 KORTINI KWA KUJIANDIKISHA MARA MBILI DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGAKURA KWA MFUMO MPYA BVR

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema watu 152 watafikishwa mahakamani mkoani Njombe kutokana na kujiandikisha mara mbili katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo mpya wa ‘Biometric Voter Registration Kit’ (BVR).
Aidha, imeeleza kuwa kata 130 zimeongezeka kutokana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kufanya mabadiliko ya kiutawala katika kata, vijiji,vitongoji na Mitaa hivyo kulazimu NEC kuhairisha kwa wiki moja uandikishaji wa daftari uliokuwa ukianza jana kwa baadhi ya mikoa.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dk Sisti Cariah alisema hayo jana wakati akielezea kuahirishwa kwa wiki moja uandikishaji hadi Juni 16 mwaka huu kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Mara.
Akizungumzia suala la watu kujiandikisha mara mbili, alisema katika mkoa wa Njombe ambao Daftari hilo liko tayari na wiki ijayo litawekwa wazi kwa siku tano na kisha kufanyiwa marekebisho kwa siku moja na wamebaini watu 152 waliojiandikisha mara mbili.
Alisema watu hao wametenda kosa la jinai na watashtakiwa, huku akitoa onyo kwa watu kuacha kufanya hivyo kwani mashine za BVR zinagundua wanaojiandikisha zaidi ya mara moja.
Alisema wataweka wazi baadhi ya watu waliojiandikisha mara mbili kwenye mikoa yote, ambayo iko tayari.
Alisema mpaka sasa tayari wamepokea madaftari yaliyokamilika ya uandikishaji kwa mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma huku uandikishaji huo ukiwa umekamilika kwa asilimia 50 na wanatarajia kukamilisha uandikishaji mwezi Julai.
Akizungumzia suala la mipaka ya kiutawala, yaliyofanywa na Tamisemi, Cariah alisema ilifanyika wiki mbili zilizopita katika mikoa mbalimbali, jambo lililosababisha kusitisha uandikishaji katika mikoa hiyo huku mikoa ambayo tayari uandikishaji umefanyika watarekebisha wakati wa kuweka wazi daftari.
“Katika kupiga kura lazima kitambulisho kioneshe kata anayokaa mtu kwa mabadiliko haya yamefanya kata kubadilika na kuongezeka 130 hivyo kufanya madiwani watakaopigiwa kura kuongezeka hivyo kata kuendana na kitambulisho,” alisema.
Alisisitiza kuwa kutokana na changamoto hiyo mikoa hiyo mitano, itaanza uandikishaji pamoja na mikoa ya Tanga na Morogoro Juni 16 mwaka huu na baadaye Juni 25,mwaka huu wataanza uandikishaji katika mkoa wa Pwani.
Alisema sasa wanatumia Mashine za BVR 8,000 walizokuwa wanahitaji pamoja na vipuri vyake vyote ziliwasili yangu mwezi uliopita.
Alisema katika mkoa wa Dar es Salaam uandikishaji utaanza Julai2 mwaka huu kwa kutumia BVR zaidi ya 3,000, ambazo kila moja ina uwezo wa kuandikisha watu 120 na hiyo itatokana na kuwa mikoa nane, uandikishaji utakuwa umemalizika na zote kutumika katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
“Jijini Dar es Salaam sehemu zenye watu wengi kutakuwa na mashine hizo nyingi huku vituo vyote, vikifunguliwa kwa mara moja ikifuatiwa na Zanzibar, ambapo wataandikisha waliokosa sifa za kuandikishwa katika Daftari la ukaazi kwa ajili ya kupiga kura ya kumchagua Rais wa Muungano”alisema.
Akizungumzia changamoto ya watu kusubiri kwa muda mrefu katika vituo vya kujiandikisha, alisema hiyo inatokana na kuwa Printa za kusafisha picha zinatakiwa kubadilishwa kila baada ya wapigakura 400 kutokana na vumbi na muda huo wtau uona kama mashine zimeharibika lakini ni utaratibu wa kawaida.
Cariah alisema uandikishaji umekamilika kw amikoa mitano ya Njombe, Lindi, Mtwara, Ruvuma na Iringa na imefanikiwa kwa kiasi kikubwa na wanaendelea katika mikoa 12 sasa ambayo ni Katavi, Rukwa, Mbeya, Dodoma, Singida, Kigoma, Kagera, Simiyu, Mwanza, Geita na Shinyanga.
Akizungumzia mafanikio ya mikoa hiyo kuwa takwimu ilikuwa kuandikisha wapigakura 518,230 na waliandikisha watu 529,224, Mtwara walitakiwa 732,465 waliandikisha 727,565, Ruvuma wapigakura 783,296 waliandikishwa 826,779 na Iringa wapigakura 524,390 waliandikishwa 526,006.
Next Post Previous Post
Bukobawadau