Bukobawadau

TANO BORA YANGU YA CCM NI HII


CREDIT;Lula wa Ndali Mwananzela
KAMA ningekuwa ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), basi ningehakikisha kuwa napeleka majina yafuatayo matano kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa.
Kati ya majina zaidi ya arobaini ya wanachama waliojitokeza kutaka kupendekezwa kuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, naamini majina yafuatayo yatakuwa na unafuu na rahisi mmojawao kuchaguliwa kuwa mgombea wa CCM kuliko majina mengine. Baadhi ya waliotangaza nia hasa vijana sioni kama wana nafasi na uwezo wa kupewa uongozi wa taifa kwa sasa. Hawa sitotumia muda kuwajadili kwa sababu hiyo moja tu.
Hata wengine ambao ni watu wazima nimeamua kuwaacha kwa sababu mbalimbali, na hasa, kuwalinganisha uwezo na nafasi yao kupitia Chama Cha Mapinduzi.
Wengine kwa sababu ya historia zao na wengine kwa sababu ya aina ya uongozi wao ambao tumeuona mpaka sasa. Wengine kwa kutambua hulka zao za uongozi naamini ikitokea wakipewa nafasi ya uongozi wa Taifa watatusumbua sana huko mbele.
Lakini pia niseme kuwa hawa watano wangu ni watu ambao naamini wanaweza kupitishwa na CCM kuwa wagombea au hata wagombea wenza japo siamini kama wataweza kushinda dhidi ya mgombea mzuri kutoka Upinzani.
Kimsingi ninachosema ni kuwa mgombea mmojawao kati ya hawa ataweza kupambana na mgombea wa Upinzani na kama upinzani hawataendesha kampeni ya kisayansi na mikakati mizuri ya ushindi basi tusije kushangaa akashinda japo CCM iko katika wakati mbaya sana wa kutetea kiti cha urais mwaka huu.
Majina? Majina yangu kwa uzito wa uwezekano wao kuwa wagombea ni hawa Bernard Membe, Augustino Ramadhani, Mark Mwandosya, John Magufuli na Makongoro Nyerere. Nitajaribu kuelezea kwa nini hawa watano.
Bernard Membe
Kati ya watangaza nia ambao kwa kuangalia kwa haraka haraka hawana nafasi ya kusonga sana mbele Membe anaweza kuonekana yuko kundi hilo. Hii ni hasa kutokana na kile kinachoonekana ushindani wake kati yake na Edward Lowassa – mtangaza nia mwingine.
Kwa muda sasa kambi hizi mbili za Lowassa na Membe zimekuwa ni tatizo kwa CCM. Hata hivyo, CCM itapata shida sana pande zote kama itampitisha Lowassa au haitampitisha. Kwani vyovyote vile ile ilivyo Lowassa ataipasua CCM na hivyo, wanaweza kumpa kitanzi cha yeye kuondoka kwa kumpa Membe nafasi ya kwanza katika kundi la tano bora na kumwacha Lowassa nje. Hiyo ni sababu ya kisiasa zaidi.
Lakini ukiingia kwa undani zaidi unaweza kuona kuwa Membe kati ya mawaziri wote wa Kikwete ni yeye amedumu kwenye wizara hiyo labda kwa muda mrefu kuliko waziri mwingine.
Sidhani kama kuna waziri mwingine aliyekalia kiti chake muda wote wa Kikwete akifanya mabadiliko mbalimbali kuliko Membe. Wapo waliobakia katika baraza lake muda wote wa mabadiliko lakini Membe ni mmoja kati ya wachache sana (kama wapo) ambao wamebakia katika wizara ile ile. Hii ina maana moja tu: imani.
Katika wizara muhimu na nyeti sana kama ya Mambo ya Nje Kikwete amemuamini mtu mmoja tu kuweza kuwa sura ya taifa kimataifa – Bernard Membe.
Hili ni kweli hasa baada ya aliyemtangulia Wizara ya Mambo ya Nje Dk. Asha Rose Migiro (mtangaza nia mwingine) alipoteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa. Kabla ya hapo Membe kwa muda mfupi alishikilia unaibu waziri kati ya Wizra ya Nishati na Madini na kisha Wizara ya Mambo ya Ndani.
Kuaminiwa kwake tangu 2007 hadi sasa kushika wadhifa huo kunaashiria kuaminika na kuaminiwa kwake na Rais lakini pia na viongozi wengine wa kimataifa. Ni vigumu sana kwa mtu katika nafasi yake kuendelea kwa muda mrefu kama ana matatizo ama na Rais wake au na viongozi wengine au kama uwakilishi wake wa nchi kimataifa una walakini.
Katika hili hakuna mgombea mwingine ambaye sasa anaweza kumlinganisha naye. Lakini zaidi ujasiri wake katika masuala ya kimataifa wakati mwingine umemletea matatizo au kuonekana kuiletea matatizo nchi. Suala la Palestina, suala la Malawi na hata yale ya Uchaguzi wa Zimbabwe nao alionekana kuwa na msimamo mkali zaidi lakini ambao aliamini uliweka maslahi ya Taifa mbele.
Matatizo makubwa yanayomkabili na ambayo sijui yataibuliwa vipi kwenye vikao vya CCM ni madai ya kupokea fedha kutoka Libya wakati wa Muammar Gaddafi na kuhusika kwake na mradi ambao haujafanikiwa sana wa Vitambulisho vya Taifa. Hili linaweza kuwa kikwazo. Lakini akivivuka hivi, siwezi kushangaa akawa ni kama simba mwenda pole.
Augustino Ramadhani
Kati ya wanaopewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa mgombea wa CCM na hata kuwezekana kweli kuwa Rais wa Tanzania ni Jaji Augustino Ramadhani. Kutangaza nia kwake kumekuwa ni mtego kwa wagombea wengine wote.
Sifa kubwa ambayo Jaji Ramadhani ataileta ni kuwa ni mwanasheria aliyebeboa; anayejua matatizo mengine ya sheria zetu na jinsi gani mifumo yetu ya sheria inatusumbua.
Kwa kumpitisha Jaji Ramadhani CCM itakuwa imemuweka mtu kwa mara ya kwanza mwenye uzoefu wa kisheria. Julius Nyerere hakuwa mwanasheria, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wote hawakuwa wanasheria.
Uwezekano kuwa mwanasheria mwenye uzoefu, ujuzi na maono kama ya Jaji Ramadhani itakuwa ni hatua mpya kabisa. Anaweza kuleta kile ambacho tunaweza kukiona ni udikteta wa sheria badala ya mtu ambao unasumbua dunia.
Tatizo kubwa ambalo labda linasumbua baadhi yetu na amelitolea maelezo kidogo ni kuwa kwa nafasi yake kama Jaji na kuwa aliwahi kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, imeweka doa kubwa kati ya imani ya Watanzania kwa majaji ambao wengi tuliamini kuwa wako juu ya hisia na matamanio ya kisiasa. Ni vigumu kuamini kuwa suala la yeye kutaka kugombea urais limekuja juzi hasa kwa vile amekiri mwenyewe kuwa alipostaafu tu ujaji akaamua kujiunga tena na CCM (au kufufua uanachama wake).
Mark Mwandosya
Kama Jaji Ramadhani, Mark Mwandosya ni msomi aliyebobea na mtaalamu katika fani yake. Na kwa vile jina lake lilishawahi kupita huko nyuma ni vigumu kuona ni kitu gani kitafanya jina lake likatwe hata lisiwe kwenye tano bora.
Kama mgombea wa urais, Mwandosya tunaweza kusema ni technocrat yaani ni mtu ambaye si mwanasiasa bali mtu wa kazi. Baadhi ya watu wanaamini Tanzania haihitaji tena wanasiasa kushika nafasi hii, bali mtu ambaye yuko juu ya uanasiasa kwani tayari wanasiasa wanajulikana mambo yao.
Kuna namna ambayo Mark Mwandosya anawavutia zaidi watumishi wa umma na wafanyakazi kwani wengi wanajua sifa ya utendaji kazi wake.
Lakini pia ujasiri wake wa kumvaa aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa na mtu anayedaiwa kuwa karibu sana timu ya Lowassa hauwezi kupita bila kusemwa. Mwandosya katika kitabu chake cha Sauti ya Umma ni Sauti ya Demokrasia, amejaribu kuonyesha jinsi gani Apson Mwang’onda na wengine walishiriki kuhujumu nafasi yake ya 2005 ambapo alipitwa na Kikwete. Na inaonekana safari hii mgongano wa kambi hizi upo pale pale; hili linaweza kuwa ni tatizo zaidi kwa Mwandosya kwani inaweza kuonekana naye kama Lowassa anaona kama nafasi hii ya urais ni kama haki ya urithi.
John Pombe Magufuli
Kati ya mawaziri ambao waliwahi kujulikana kama “askari wa miavuli” hakuna ambaye jina lake linakumbukwa na kutajwa tajwa sana kama la Magufuli. Kiasi kwamba, ni miongoni mwa viongozi wachache ambao wamekuwa wakitarajiwa sana kugombea urais.
Sifa yake kubwa ni ule uwezo wake wa kufuatilia watu na kusimamia kile anachoamini ni sheria. Watu wanaweza kukumbuka bomoa bomoa ya Magufuli ambapo watu walibomolewa nyumba na ofisi zao hata kufikia mahali kutishia kubomoa jengo la Tanesco pale Ubungo! Kama Membe, Magufuli naye ameaminiwa sana na Kikwete kwenye wizara nyeti ya Ujenzi na Miundombinu kiasi kwamba chini yake miradi mbalimbali imeweza kutekelezwa.
Hili linaweza kuwa ni nafasi yake kubwa zaidi ya kuaminiwa zaidi kwani katika kidogo alichoaminiwa tayari ameonyesha uwezo wa kukifatilia.
Tatizo lake kubwa ambalo linaweza kumkabili ni jinsi gani baadhi ya maamuzi yake yamekuwa na hasara kwa Taifa. Uuzaji wa nyumba za serikali, kesi kadhaa ambazo serikali ilijikuta ina makosa haviwezi kusahauliwa. Haitoshi tu kuamini kuwa mtu anasimamia sheria lakini zaidi ni lazima awe na uhakika anasimamia sheria. Tanzania hii haihitaji mtu anayeamini kuwa yeye ndiyo sheria. Hili linaweza kuwa kizuizi kikubwa.
Makongoro Nyerere
Kati ya wagombea wote hadi hivi sasa hakuna mgombea ambaye anaonekana kuvutia hisia za wananchi wa kawaida kama Mako Nyerere. Sababu ziko nyingi lakini kubwa ni kuwa Makongoro anaonekana ametambua tatizo la Tanzania ni nini hasa.
Makongoro ukimsikiliza tangu alipotangaza nia yeye ameing’ang’ania CCM. Anaelewa kitu ambacho labda wengine wanakielewa, hasa wapinzani kuwa tatizo la uongozi wa Tanzania limeanzia ndani ya CCM na haliwezi kushughulikiwa bila kuishughulikia CCM. Makongoro basi anaonekana ni mtu pekee ambaye anaweza kuishikilia CCM na kuanza kuifanyia matengenezo yanayohitajika.
Lengo hili ukiliangalia linaendana sana na baadhi ya viongozi wa CCM ambao wameshapokea kibwagizo chake cha “Tuachieni Chama Chetu” wakiwaambia mafisadi waliojikunyata kwenye vyumba vya chama tawala.
Tatizo lake na inaweza kuwa ni heri yake pia ni jina la Nyerere. Kwa uzuri au kwa ubaya, Makongoro anagusa nyoyo za wazee wengi wa nchi hii ambao bado wanahisia nzuri za Baba wa Taifa hasa wakiangalia uongozi uliopo; hata baadhi ya vijana ambao wanatamani uongozi kama ule wanaouona katika Makongoro nafasi ya kujaribu kuanza upya kwa kuanza kuisafisha CCM.
Siwezi kushangaa kabisa kama CCM itapoteza urais mwaka huu, Makongoro ndani ya miaka miwili akaibuka kama kiongozi mkuu wa CCM – iliyomeguka na akajipanga kama Uhuru Kenyatta kule Kenya.
Katika hawa watano, yeyote anaweza kuteuliwa kugombea. Hiyo ndiyo tano yangu nina uhakika wengine wanazo za kwao na sababu zao.
RAIA MWEMA Toleo la 411
24 Jun 2015
Next Post Previous Post
Bukobawadau