Bukobawadau

SAKATA LA ESCROW:Mahakama imetupilia mbalimbali kesi dhidi ya Maazimio ya Bunge

#‎TegetaEscrow‬ Mahakama imetupilia mbalimbali kesi dhidi ya Maazimio ya Bunge kuhusu wizi wa Escrow.
Maazimio 8 yaliyopitishwa na Bunge kuhusu akaunti ya Tegeta Escrow

1 Bwana Harbinder Singh Seth na wengine

Bunge linaazimia kwamba, TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Vyombo vingine husika vya Ulinzi na Usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, dhidi ya watu wote waliotajwa na Taarifa Maalumu ya Kamati, kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na Miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusika katika vitendo vya jinai.


2 Mitambo ya IPTL

Bunge linaazimia kwamba, Serikali iangalie uwezekano wa kuichukua mitambo ya kufua umeme wa IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa mujibu wa Sheria za nchi.

3 Mapitio ya Mikataba ya Umeme ( Azimio la Kamati teule ya Richmond)

Bunge linaazimia kwamba, Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti la Mwaka 2015/2016, Serikali iwasilishe Taarifa ya Utekelezaji wa Mapitio ya Mikataba ya Umeme;

4 Kitengo cha Rushwa kubwa

Bunge linaazimia kwamba; Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria iliyounda TAKUKURU, kwa lengo la kuanzisha Taasisi mahususi itakayoshughulikia kupambana na kudhibidi vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa Taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

5 Majaji

Bunge linaazimia kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi, kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania. (Makofi)

6 Benki ya Stanbic na Benki Nyingine

Bunge linaanzimia kwamba, mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow kuwa ni Taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (Institutions of Money Laundering Concern).


7 Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu na Bodi ya TANESCO

Bunge linaazimia kwamba, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe kwa kuishauri Mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wao.

8. William Ngeleja, Victor Mwambalaswa na Andrew Chenge

Bunge linaazimia kwamba, Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao kwenye Kamati husika za Kudumu za Bunge.
Next Post Previous Post
Bukobawadau