Bukobawadau

NEC YAKABIDHI POLISI MAJINA YA WATU 52,078 WALIOJIANDIKISHA ZAIDI YA MARA MBILI KATIKA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

 Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhan (kushoto), akimkabidhi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Benedict Wakulyamba orodha ya majina 52,078 ya watu waliojiandika katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa BVR zaidi ya mara mbili Dar es Salaam leo, kwa ajili ya uchunguzi na baadae hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika.
 Masanduku ya BVR yakiwa yamehifadhiwa Bohari ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
 Mkurugenzi wa Idara ya Daftari la mpiga kura, Dk. Sisti Cariah (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu hatua waliyoifikia kuhusu daftari hilo na shughuli mbalimbali zinazoendelea kufanywa na NEC kuelekea uchaguzi mkuu.
 Mtaalami wa Tehama wa NEC, Fatuma Mkanguzi akiwaelezea wanahabari jinsi mfumo wa Tehama unavyofanyakazi.
 Fundi, Francis Skale akiwa kazini.
 Mafundi wa NEC wakiendelea na kazi.
 Mtaalamu wa mfumo wa ulinzi wa NEC, Adolf Kinyelo akitoa maelekezo ya jinsi ya mfumo huo unavyofanya kazi.
 Wanahabari wakichukua taarifa mbalimbali kuhusu NEC inavyofanyakazi zake na hatua waliyofikia kuelekea uchaguzi mkuu. 
Picha hii ni baadhi ya watu waliojiandikisha zaidi ya mara mbili katika daftari hilo.

Na Dotto Mwaibale


TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imelikabidhi jeshi la polisi orodha ya majina ya watu zaidi ya 52,000 ambao wamebainika kujiandikisha zaidi ya mara moja kwenye daftari la kupigia kura kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR), akiwemo Diwani wa Kata ya Kimara, Pascal Manota (Chadema).

Idadi hiyo ilibainishwa Dar es Salaam leo na Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima wakati wa ziara na waandishi wa habari katika bohari ya utayarishaji wa vitambulisho vya kupigia kura kwa mfumo wa BVR.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi orodha ya majina hayo kwa Jeshi la Polisi, Kailima alisema watu hao watachukuliwa hatua kisheria kwani kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa kisheria huku akiwatoa hofu wananchi waliojiandikisha na kutoonekana majina yao.

"Mchakato wa kutoa majina ni suala ya kisheria kwa sababu ukiangalia kifungu namba cha sheria ya uchaguzi namba 11 (a) kinasema baada ya kuboresha daftari tume itaweka wazi majina hayo ili watu waweze kupitia, lakini kifungu namba 23 cha sheria hiyo hiyo kinasema, iwapo mtu hataliona jina lake kwenye daftari anapaswa atoe taarifa kwa mkurugenzi wa uchaguzi au ngazi ya halmashauri ili taarifa zake ziweze kufanyiwa marekebisho,"alisema

Akizungumzia namna ya kupiga kura kwa walemavu wasioona, Kailima alisema hadi sasa wapo kwenye mchakato wa kuleta vifaa vya kupigia kura kwa kundi hilo ili kuwe na usiri wakati wa upigaji kura na kuepusha watu kupiga kura zaidi ya mara moja.

"Ijumaa (leo) mtashuhudia tukifanya maridhiano ya mwisho na kundi hilo, tumewashirikisha kwenye kikao chetu cha ndani na tukawapa wenyewe kazi ya kwenda kubuni aina ya karatasi za kupigia kura na tumewapa uhuru ambapo tutakubaliana nao na tuone mahitaji yao wenyewe kwa wale wanaojua kusoma maneno yao na wasioweza wapige kura,"alisema.

Kwa upande wa Msimamizi wa Kitengo cha Kufanya Marekebisho ya 'BVR Kit' na Kuchakata data, Aguta Obala alisema tuhuma za vitambulisho feki vilivyokamatwa hivi karibuni si ya tume ya uchaguzi.

"Hizo taarifa sina uhakika kwa sababu sijaona kama taarifa zinafanana na za hapa tume, lazima wahakikishe wametoa taarifa za vitambulisho hivyo kwenye BVR Kit ipi,"alisema.

Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Benedict Wakuryamba baada ya kupokea orodha hiyo alisema baada watu hao na taarifa zao zitafanyiwa upelelezi na kufikishwa mahakamani endapo atakutwa na hatia.

Naibu Katibu Mkuu wa Teknlojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wa NEC, Dk. Sisti Cariah alisema kwa kutumia mfumo wa BVR ni vigumu mtu kujiandikisha zaidi ya mara moja kwani mfumo huo ni rahisi kumgundua huku akibainisha kurekebisha kasoro ndogo ndogo. 

Manota ajibu tuhuma

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili kuhusu kutuhumiwa kujiandikisha zaidi ya mara moja, Manota alisema tuhuma hizo si za kweli na kwamba alijiandikisha mara moja ambapo jina lake katika kitambulisho hicho halikuonekana vizuri.

Alisema kutokana na hali hiyo ilimpasa arudie kujiandikisha upya katika kituo hicho hicho huku ikiwa muda ni tofauti kutokana na msongamano wa watu katika mchakato wa uandikishaji.

"Nilipojiandikisha mara ya kwanza jina langu lilififia kwenye kitambulisho na hapo ndipo nilipoomba nijiandikishe tena ambapo nilivua koti na kupiga picha," alisema na kuongeza kuwa muandikishaji huyo alishindwa kurekebisha data 'edit'.

Manota alisema baada ya kujiandikisha upya kitambulisho cha awali alikiacha na kwamba kitambulisho hicho kipo halmashauri ya manispaa hiyo huku akiamini hiyo ni siasa na kumpigia kampeni.

Rufaa za ubunge 

Katika hatua nyingine, NEC imesema hadi kufikia jana rufaa za wagombea ubunge na udiwani katika maeneo mbalimbali nchini zilikuwa zimefikia 60.

Pia, imesema hadi kufikia Agosti 30 ya wiki ijayo rufaa 31 zitakuwa zimetolewa uamuzi, hivyo tume itakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia hilo.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa NEC, Ramadhan Kailima alisema rufaa za ubunge zilikuwa 31 na udiwani 29 lakini zinaweza kuongezeka .

Hata hivyo, alitoa mwito kwa vyama ambavyo vitaona havikuridhika na matokeo kwa njia moja ama nyingine katika maeneo waliyogombea kuwasilisha rufaa zao tume hiyo kutokana na kutoridhishwa na wakurugenzi wa uchaguzi katika maeneo yao.

Alisema miongoni mwa chama kilichowasilisha rufaa zake tume ni ACT -Wazalendo ambacho kinalalamikia wagombea wake kutotendewa haki.
Next Post Previous Post
Bukobawadau