Bukobawadau

BUKOBA LIVE:Ushindi wa Dkt. John Magufuli Urais Tanzania Bara.

Amsha amsha Mjini Bukoba Muda mchache baada ya Mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama cha CCM John Pombe Magufuli kutangazwa Kuwa Rais mteule wa taifa la Tanzania kufuatia uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili.
Akitoa matokeo hayo mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema kuwa Magufuli alijipatia kura 8,882,935 ikiwa ni aslimia 58.46 huku mpinzani wake wa karibu Edward Lowassa wa chama cha Chadema akijipatia kura 6,072,848 ikiwa ni asilimia 39.97 ya kura zote.
Haya ndiyo matokeo kamili kama yalivyotangazwa na Jaji Lubuva:
 Mjini Bukoba Wafuasi wa chama cha CCM wameanza kusherehekea ushindi wa Bw Magufuli
  Mbele ya Jengo la Makao Makuu ya CCM Wilaya Bukoba
Bi Teddy Mboto akifurahia Ushindi wa Mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama cha CCM John Pombe Magufuli
 Wakazi wa kasai wakimiminika kuelekea zilipo ofisi cha Chama cha mapinduzi Mjini hapa
 .Wananchi wakipiga 'Push Up'
 Picha Nyuma Mkuu wa Mkoa wa Kagera Bw John Mongella akiteta jambo na Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Kagera Bw. Hamim
 Shangwe za hapa na pale zikiendelea Viunga vya miji wa Bukoba
Wafuasi wa chama cha CCM wakiendelea kusherehekea ushindi wa Mh.Magufuli

Awali kabla ya kutolewa kwa matokeo hayo vyama vya siasa vilivyokubaliana na matokeo vilitia sahihi matokeo hayo. Lakini chama cha Chadema, chake Bw Lowassa hakikuwakilishwa. Chama hicho kimepinga matokeo hayo.
Akivihutubia vyombo vya habari mgombea wa urais kupitia chama hicho Edward Lowassa amepinga matokeo yoyote ya uchaguzi huo na kujitangaza mshindi wa uchaguzi kwa kupata asilimia 62 ya kura zilizopigwa.
Lowassa amedai kwamba tume ya uchaguzi nchini humo imeshirikiana na chama tawala CCM kufanya udanganyifu katika shughuli hiyo, madai ambayo tume hiyo imekanusha.
"Hatuna hata chembe ya wasiwasi kwamba mchakato huu ulifuata sheria na ni halali," alisema Jaji Lubuva muda mfupi kabla ya kutangaza matokeo.
Aidha, amesema tume iliendesha mchakato wote "bila shinikizo".
Akizungumzia kutoidhinishwa kwa matokeo hayo na wawakilishi wa Chadema, mkurugenzi wa uchaguzi katika tume Bw Ramadhan Kailima alisema sheria inawaruhusu kuendelea na kutangaza matokeo hata bila chama chochote kile kuwakilishwa au kuidhinisha matokeo husika.
Kwenye uchaguzi huo, kati ya wapiga kura 23,161,440 waliojiandikisha, ni 15,589,639 waliopiga kura, ambao ni asilimia 67.31 ya wapiga kura wote. Kura 402,248 ziliharibika.
Kufuatia kutangazwa kwa matokeo hayo, tume hiyo ya uchaguzi sasa inatarajiwa kumkabidhi Bw Magufuli cheti cha kuwa mshindi wa urais.
Muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo, chama hicho kimeanza kusherehekea kwenye mtandao wa Twitter huku wafuasi wake nao wakianza kusherehekea katika barabara za miji.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

CCM inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa wana-CCM na kwa umma:

MALALAMIKO YA CCM KUHUSU MATOKEO KWENYE BAADHI YA MAJIMBO

Chama cha Mapinduzi hakijaridhishwa na utaratibu wa kukusanya na kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya majimbo. Katika majimbo manne kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi, hasa katika kujumlisha matokeo, uliopelekea wabunge wa upinzani kutangazwa washindi. Majimbo hayo ni Iringa Mjini, Mikumi, Ndanda na Kawe. Wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo haya wamevuruga uchaguzi. Kutokana na utata uliokuwa umejitokeza wakati wa zoezi la kujumlisha kura, CCM iliomba kura zihesabiwe upya lakini ikanyimwa haki hiyo ya msingi ambayo iko kwenye sheria. Kwenye baadhi ya majimbo, ikiwemo Nyamagana, wapinzani walipewa haki ya kura kuhesabiwa upya. Kwa msingi huo, CCM imeamua kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo haya. Tunataka sote tujiridhishe kwamba utashi wa wananchi umeheshimiwa. Bado tunaendelea kukusanya taarifa za maeneo mengine kama kulikuwa na ukiukwaji mkubwa uliobadilisha matakwa ya wapiga kura. Hata hivyo, tunakiri kwamba kwenye maeneo mengi tulikopoteza viti vya Ubunge, tumepoteza kihalali, hatuna malalamiko, tunaheshimu maamuzi ya wananchi, na tutafanya tathmini baada ya uchaguzi ili tubaini makosa na kuyarekebisha.

MAONI YA WAANGALIZI WA UCHAGUZI

CCM imepokea maoni ya awali ya waangalizi wa uchaguzi. Tumefarijika kwamba karibu wote wametoa kauli ya pamoja kwamba uchaguzi huu ulikuwa wa haki na huru, uliofanyika kwa uwazi na kwa amani – na kwamba changamoto zilizojitokeza ni ndogo na zimetokea katika maeneo machache kiasi zisingeweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa sasa. Tumepokea mapendekezo waliyoyatoa kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha mchakato wa uchaguzi kwa miaka ijayo, na hivyo kuimarisha demokrasia nchini mwetu. Kwa kauli za waangalizi hawa, kwamba, kwa jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa, matokeo yanayotangazwa sasa ni kielelezo sahihi cha utashi wa Watanzania kuhusu viongozi wanaowataka.

MALALAMIKO YA UKAWA

Tumesikia malalamiko ya viongozi wa UKAWA kupitia mkutano wao na waandishi wa habari jana. Tumeshangazwa na kauli kwamba hawakubali matokeo ya Urais yanayotangazwa na Tume. Hata hivyo, matokeo ya Ubunge wanayakubali na, kule wanakoshinda, wanayasheherekea. Tunashangazwa kwasababu Tume iliyoandaa uchaguzi wa Rais ni hiyo hiyo iliyoandaa uchaguzi wa Wabunge, wasimamizi ni walewale, vituo ni vilevile, na sheria na taratibu zilizotumika ni zilezile. Hata fomu ya matokeo walizosaini wakala wao kwenye vituo vya kupiga kura, zimegawanywa katika sehemu (columns) tatu: Urais, Ubunge na Udiwani. Mawakala wao walisaini fomu hizo kwenye vituo vya kupiga kura.  Wameanza kuwa na matatizo na matokeo haya baada ya kuona mwelekeo wa kushindwa. Kama mwelekeo ungekuwa tofauti, wangekuwa na imani na Tume, wasimamizi na taratibu zote.

Tunaomba ifike pahala sasa kwamba, katika kuijenga demokrasia yetu na kuliimarisha taifa letu, tuanze utamaduni mpya wa anayeshindwa kunyanyua simu kumpigia anayeshinda na kumpongeza. Nafasi ya mwisho aliyonayo Mgombea wa UKAWA kuendelea kujijengea heshima katika jamii yetu, na kuwa mwanademokrasia, ni kwa kufanya hivyo siku Dkt. Magufuli atakapotangazwa mshindi. 

Kwetu sisi CCM, kuchagua wagombea bora na kuwanadi na kutengeneza sera bora na kuzinadi, pamoja na rekodi yetu katika uongozi wa nchi, ndio njia zetu pekee za ushawishi. Katika uchaguzi huu, wananchi wamefanya maamuzi yao kwa uhuru na utashi, ikiwemo kuwaangusha mawaziri sita ambao tuliwasimamisha kama wagombea wetu katika majimbo mbalimbali. Nguvu na utashi wa wananchi umejidhihirisha katika uchaguzi huu.

Mchakato wa uchaguzi sasa unakaribia kufikia ukingoni, tutawapata madiwani, wabunge na Rais, tunapaswa kuendelea na maisha na tuwape nafasi watutumikie. Jitihada tunazoziona sasa za viongozi wa UKAWA za kuendeleza siasa za uchaguzi kwenye mitaa ya miji yetu kwa njia za vurugu na maandamano hazikubaliki hata kidogo. Tunalaani kitendo cha wafuasi wa UKAWA kuchoma ofisi za CCM katika Wilaya ya Mbozi.  Amani ya nchi hii ina thamani kuliko hitaji la madaraka la mtu yoyote. Wenzetu wa UKAWA wana haki ya kulalamika lakini hawana haki ya kuiingiza nchi yetu machafukoni kwa kuwakusanya vijana na kuwaingiza mitaani wafanye vurugu na kuhatarisha maisha, kuharibu mali na kusimamisha shughuli za watu wengine. Tunawaomba Watanzania waendelee na shughuli zao kama kawaida huku kila mmoja akitambua wajibu wake wa kuilinda amani ya nchi yetu.



January Makamba

Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM

28.10.2015
Next Post Previous Post
Bukobawadau