Bukobawadau

DK. JOHN POMBE MAGUFULI AKABIDHIWA CHETI CHA USHINDI WA URAIS WA TANZANIA AWAMU YA TANO JIJINI DAR ES SALAAM LEO

 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva (kulia), akimkabidhi cheti cha Urais Rais Mteule wa Tanzania Dk.John Magufuli katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam leo. Kushoto ni Makamu wa Rais Mteule, Samia Hassan Suluhu.
 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva (kulia), akimkabidhi cheti cha Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu katika hafla hiyo.
 Rais Mteule wa Tanzania, Dk. John Magufuli (kulia), akiwapungia mkono wananchi wakati wa hafla hiyo ya kukabidhiwa cheti cha urais. Kutoka  kushoto ni mgombea urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira na mgombea nafasi hiyo kupitia Chama cha ADC, Chief Lutalosa Yemba.
 Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi (kushoto), akimpongeza Rais Mteule wa Tanzania Dk. John Magufuli baada ya kuchaguliwa kuwa rais.
 Makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakishangilia wakati Rais Mteule wa Tanzania Dk.John Magufuli alipokuwa akitoka Ukumbi wa Diamond Jubilee kukabidhiwa cheti cha urais.
 Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye hafla hiyo.
  Rais Mteule wa Tanzania, Dk.Magufuli akimuonesha Rais Jakaya Kikwete cheti cha ushindi.
 Rais Mteule wa Tanzania, Dk.Makufuli akiwa katika picha ya pamoja na wagombea urais wenzake wa vyama vingine.
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akimpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva kwa kusimamia vizuri uchaguzi mkuu wa 2015.
Rais Jakaya Kikwete na Rais Mteule Dk.John Pombe Magufuli wakiwa katika picha ya pamoja na wake zao kwenye hafla hiyo.

Na Dotto Mwaibale

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imemkabidhi cheti cha ushindi aliyekuwa mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk, John Magufuli baada ya kushinda kwa kura nyingi kuliko wenzake kwenye uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Aidha wanasiasa wamemtaka Dk. Magufuli kutekeleza mambo yote ambayo ameahidi, huku Mgombea Urais wa ACT-Wazalendo Anna Mghwira., akimtaka ahakikishe kuwa Katiba ya wananchi inapatikana ili kufanikisha dhana ya mabadiliko ambayo yalikuwa yanatajwa na wagombea wote.

Akizungumza kabla ya kumkabidhi cheti hicho katika hafla iliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam leo Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki huku akiwapongeza wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura tofauti na mwaka 2010.

Lubuva alisema katika uchaguzi huo wagombea wa nafasi ya urais ni Anna Mghwira wa ACT, Chief Lutalosa Yemba wa ADC, Dk. Magufuli wa CCM, Edward Lowassa wa Chadema, Hashim Rugwe wa Chaumma, Malik Kasambala wa NRA, Elifatio Lyimo wa TLP na Fahmi Dovutwa wa UPDP.

Alisema, tume imemtanga Dk. Magufuli kwani amefanikiwa kupata kura nyingi kuliko wagombea wenzake ambapo  walioandikishwa ni wapigakura 23,161,440, waliopiga kura ni 15,589,639 sawa na asilimia 67,31 ya waliojiandikisha.

Alisema kura halali ni 15,193,862 sawa na asilimia 97.46, kura zilizokataliwa ni 402,248 sawa na asilimia 2.58.

Jaji Lubuva alitangaza matokeo kuwa Mghwira amepata kura 98,763 sawa na asilimia 0.65, ADC amepata kura 66,049 sawa na asilimia 0.43.

Dk. Magufuli amepata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46 sawa na asilimia 58.46, Lowassa amepata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97, Rungwe 49,256 sawa na asilimia 0.32, Kasambala amepata kura 8,028 sawa na asilimia 0.05.

Wengine ni Lyimo amepata kura 8,198 sawa na asilimia 0.05, Dovutwa amepata kura 7,785 sawa na asilimia 0.05.

Kailima

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhan, alisema kura zilizopigwa zinatoka katika majimbo ya uchaguzi 264 na kata 3,957 na hakuna dosari kubwa ambayo ilitokea.

Alisema katika nafasi ya ubunge majimbo yaliyofanya uchaguzi ni 256 huku majimbo nane yakiwa hayajafanya uchaguzi kutokana na sababu mbalimbali ambazo ni vifo kwa wagombea na karatasi za wagombea kuwa na mapungufu.

Kailima alisema pia kuna Kata ambazo hazijafanya uchaguzi kutokana na mapungufu mbalimbali ambapo wanatarajiwa kufanya uchaguzi mapema iwezekanovyo.

"Mchakato  wa uchaguzi umefanyika kwa kufuata sheria hivyo tume inadiriki kusema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki kwani hakuna lalamiko lolote kutoka kwa wakala," alisema.

Alisema kifungu cha 85 kinaipa mamlaka haki ya kutangaza matokeo hata kama baadhi ya wagombea watagoma kusaini matokeo husika hivyo aliyetangazwa na tume ndiye mshindi.

Mghwira

Akizungumza baada ya tume kumkabidhi mshindi cheti, aliyekuwa mgombea wa urais kupitia ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, alisema anakubaliana na matokeo na kumtaka Magufuli ahakikishe kuwa anasimamia upatikanaji wa katiba.

Mghwira alisema, iwapo anataka mabadiliko yaweze kupatikana ni jukumu lake kusimamia upatikanaji wa katiba ya wananchi kwani ndiyo inaweza kuleta mabadiliko sahihi kwa Tanzania ya leo.

Aidha, alimtaka mshindi huyo wa nafasi ya urais kusimamia suala la usawa na umoja wa kitaifa ambao utaweza kujenga nchi kufikia maendeleo sahihi pamoja na wananchi.

"Tunahitaji uchumi imara ili kurejesha fahari ya nchi na wananchi kwani hakuna shaka kuwa wananchi wamekata tamaa na taifa lao jambo ambalo sio sahihi," alisema.

Mghwira alitumia nafasi hiyo kumkabidhi Dk. Magufuli, ilani ya chama hicho kwani ina malengo ya kuibadilisha Tanzania.

Yemba

Kwa upande wake aliyekuwa mgombea urais, kupitia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Chifu Litalosa Yemba, alisema anampongeza Dk. Magufuli kwa ushindi huku akiweka bayana kuwa tangu aanze kushiriki chaguzi uchaguzi wa mwaka huu ndio uchaguzi ambao ulikuwa huru na wa haki.

Alisema mapungufu ambayo yanalalamikiwa na baadhi ya wagombea yanapazwa kuangaliwa kwa undani zaidi ili kuhakikisha kuwa hayarejei kutokana na ukweli kuwa mchakato huo ni muhimu kwa wananchi.

Yemba alisema, anampongeza mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kwa kufanya kampeni za kistaarabu pamoja na matusi, kashfa na dharau ambazo zimejitokeza kwake.

"Tunaweza kusema mambo mengi ila ambaye ahataki kutambua mchango wa Lowassa katika siasa za Tanzania hasa upinzani atakuwa hajui siasa ninachoomba Chadema na vyama vya upinzani kudumisha nguvu hii kwani hatujaweza kupata kura zaidi ya milioni 2 tangu kuanza kwa vyama vyetu," alisema.

Aidha, ameweka bayana kuwa iwapo angefanya kampeni katika uchaguzi huu angeweza kuwa mshindi wa pili lakini kutokana na uhaba wa fedha walishindwa kufanya kampeni ila anawashukuru wananchi kwa kura ambazo wamepata.

Jonatha

Akizungumzia uchaguzi huo Kiongozi wa waangalizi kutoka Jumuia ya Madola, Rais mstaafu wa Nigeria, Godluck Jonathan, alisema uchaguzi ulikuwa huru na haki na kuzitaka nchi zingine kuiga Tanzania kwani imekuwa mfano bora.

Godluck alisema, uchaguzi ni jambo ambalo linakuwa na changamoto mbalimbali ambapo sio jambo rahisi kila mtu kukubaliana na matokeo lakini kwa mtazamo wao wanaamini kuwa uchaguzi huo umefanyika vizuri.

Nchemba

Mwigulu Nchemba ambaye ni mbunge mteule wa Jimbo la Iramba Magharibi, alisema amefurahishwa na ushindi huo kwani Dk. Magufuli ana vigezo vyote vinavyohitajika kwa kiongozi wa nchi.

Alisema watanzania wajiandae kwa kupata mabadiliko sahihi ambayo walikuwa wanayataka kwani kiongozi huyo ni mtu ambaye anasimamia uwajibikaji, uadilifu na mchapakazi.

"Vigezo vimetumika kumpata rais sahihi kwa maslahi ya Taifa, hivyo kilichobakia ni watu kufanya kazi ili dhana nzima ta hapa kazi tu ionekane na mabadiliko pia," alisema.

Mwijage

"Huyu ndiye chaguo sahihi kwa maslahi ya Taifa na pia naamini hata Mungu ndiye aliyetaka tumpate Magufuli naamini mabadilikio yataanza vijijini ili kuzuia watu kuja mijini kutafuta kazi," alisema.

Alisema watu wajiandae kufanya kazi kwani kasi ya kiongozi huyo mpya wa nchi itakuwa haina mzaha hivyo wale wakaa vijiweni watambue kuwa nafasi hiyo haipo kupitia Dk. Magufuli.

Madabida

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida, alisema ushindi huo wameupokea kwa furaha pamoja na ukweli kuwa yalikuwa ndio matarajio yao.

"Sisi hatukuwa na shaka kuhusu ushindi huo lakini pia mgombea wetu ni mtu mzuri sana katika utendaji naamini kuwa wananchi wamemuelewa hivyo watarajie kuona mabadiliko ya kweli," alisema.

Madabida alisema vyama vya upinzani vilikuwa vinatumia nguvu ya hali ya juu kuhakikisha kuwa vinashinda lakini kutokana na mikakati yao wamefanikiwa kuibuka kidedea.

Kuhusu majimbo mengi ya mkoa wake kuchukuliwa na vyama vya upinzani alisema hayo ni maamuzi ya wananchi lakini wao kama uongozi walifanya kila linalowezekana kufanikisha ushindi.

Aidha, alikanusha taarifa za kuwa wameshindwa kutokana na yeye kumuunga mkono Lowassa wakati yupo CCM na kuwa hakufanya kampeni na kuweka bayana kuwa alikuwa anamuunga mkono wakati huo ila kwa sasa alikuwa na Magufuli.

Katika hafla hiyo ya kumkabidhi cheti cha ushindi Dk. Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu Hassan, pia Rais Jakaya Kikwete, alishiriki, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Spika wa Bunge Anne Makinda, Rais wa Awamu ya Pili, Ally Hassan Mwinyi, Mawaziri Wakuu wastaafu na viongozi wengine walihudhuria pamoja na wananchi na wanachama wa CCM.


Next Post Previous Post
Bukobawadau