CCM inapenda kutoa taarifa kuhusu masuala kadhaa kwa wanachama, wapenzi na mashabiki wake na kwa umma wa Watanzania.
Kufunga Kampeni
CCM itafunga kampeni zake kwa utaratibu mpya na kwa kishindo. Kampeni
za CCM zitafungwa kitaifa kwa mikutano mikubwa ya kampeni katika mikoa
mitano. Mikutano hiyo itaongozwa na viongozi wa CCM kitaifa waliopo
madarakani na wastaafu. Mikoa hiyo na viongozi wakaoongoza mikutano hiyo
ni kama ifuatavyo:
1. Mwanza – Ndugu Jakaya Mrisho Kikwete,
Mwenyekiti wa CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, Mgombea Urais, na Ndugu
Samia Hassan Suluhu, Mgombea Makamu wa Rais
2. Tanga – Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM
3. Mbeya – Ndugu Benjamin William Mkapa, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu
4. Mtwara – Ndugu Ali Hassan Mwinyi, Mwenyekiti wa CCM Mstaafu
5. Kigoma – Ndugu Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM
6. Kilimanjaro – Ndugu Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu
7. Mara – Ndugu Joseph Warioba, Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu Mstaafu
Kati ya leo na kesho, maeneo mengine yanaweza kuongezeka. Mikutano hii
itaanza saa sita mchana na itarushwa, yote kwa pamoja, kwa matangazo ya
moja kwa moja ya vituo vya televisheni vitano na vituoa vya redio 67.
Vilevile, watakaohudhuria katika mikutano hii wataunganishwa moja kwa
moja na mkutano wa Mwanza, alipo Mwenyekiti, Mgombea na Mgombea Mwenza,
na wataweza kusikiliza hotuba ya Dkt. Magufuli moja kwa moja kupitia
screens zitakazokuwa katika viwanjani vyote hivi saba.
Namna hii
ya ufungaji wa kampeni itakuwa ni ya kihistoria, na inadhihirisha nguvu
ya CCM inayoiwezesha kufanya mikutano mikubwa ya kampeni kwa siku moja
katika maeneo mbalimbali nchini. Lakini pia tutafanya historia katika
tasnia ya utangazaji wa televisheni hapa nchini kwa kutangaza na
kuunganisha kwa pamoja matukio saba kwa wakati mmoja.
Kwa upande
wa Dar es Salaam, tutafanya mkutano mkubwa wa ufungaji wa kampeni za
Mkoa wa Dar es Salaam, katika Uwanja wa Jangwani, kesho, Ijumaa, tarehe
23 Oktoba 2015. Siku ya Jumamosi, tarehe 24 Oktoba 2015, Wagombea Ubunge
katika majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam watafunga kampeni katika maeneo
ya majimbo yao kwa namna mahsusi.
Tathmini ya Kampeni
Kama Chama, tumeridhika na ubora na ukubwa wa kampeni tulizofanya licha
ya changamoto za hapa na pale. Dkt. Magufuli na Ndugu Suluhu wamefanya
kazi kubwa, na kwa bidii kubwa, na maarifa makubwa. Wamekuwa barabarani
kwa siku 57 wakifanya mikutano kati ya 8 hadi 12 kwa siku. Imani yetu ya
ushindi inatokana na kazi kubwa waliyofanya. Pia, CCM inawashukuru
viongozi, wapenzi wa washabiki wake – wa makundi mbalimbali ya kijamii -
kote nchini kwa kazi kwa kazi kubwa ya kampeni waliyoifanya.
Kutokana na kazi kubwa na nzuri iliyofanyika, na kutokana na mwenendo wa
tafiti huru na tafiti zetu za ndani, CCM inategemea ushindi wa asilimia
zisizopungua 69.
Uchaguzi wa Amani
CCM haitachoka
kuendelea kusisitiza uchaguzi wa amani na utulivu. Sisi kama chama
kikubwa cha siasa nchini, chenye wafuasi wengi zaidi, na chenye dhamana
ya uongozi wa dola, tutatimiza wajibu wetu wa kuhimiza utulivu kwa
wapenzi, washabiki na wanachama wetu. Tunawataka na wenzetu wafanye
hivyo.
Kauli za wenzetu kwamba kura zitaibiwa ni kauli za
kutojiamini na kujiandaa kufanya vurugu. Kauli za kwamba washabiki wa
UKAWA wakishapiga kura wabaki vituoni kulinda kura si kauli za wanaotaka
uchaguzi wa amani.
Kwa utaratibu wetu wa uchaguzi, utaratibu wa
pekee kwa Chama kulinda kura zake ni kwa kupitia wakala wa vyama waliopo
kwenye kila kituo cha kupiga kura na wenye nguvu na mamlaka ya kisheria
ya kushuhudia zoezi zima, kuanzia kupiga kura, kuhesabu kura hadi
kutangaza matokeo. Kura zinapigwa na kuhesabiwa vituoni mbele ya
wasimamizi wa uchaguzi, mawakala wa vyama na waangalizi wa uchaguzi wa
ndani na nje ya nchi. Mawakala wa vyama na wasimamizi wa uchaguzi
wanaweka sahihi kwenye fomu za matokeo, na matokeo hayo yanatangazwa na
kubandikwa kwenye kituo. Kwenye kituo kikuu cha Tume cha kujumlisha
matokeo, mawakala wa vyama pia huwepo na Tume hujumlisha matokeo kutoka
kwenye fomu za matokeo za vituo vya nchi nzima zilizosainiwa na mawakala
wa vyama kwenye kila kituo. Kwa viongozi wa UKAWA kuwaambia watu
waingie barabarani au kuvizunguka vituo vya kupigia kura eti ili kulinda
kura hakuna maana yoyote zaidi ya kutafuta namna ya kuhalalisha vujo,
vurugu na uporaji na kuwazuia watu wengine, hasa wanawake, kupiga kura.
Tunaviomba vyombo vya ulinzi na usalama vizuie hili jambo kwasababu
halina nia njema.
Mkakati wa UKAWA ni kufanya vurugu baada ya
kushindwa na kutengeneza mazingira ya mgogoro wa kisiasa ili Jumuiya ya
Kimataifa iingilie kati na kupendekeza kugawana madaraka. Mkakati huo
hautafanikiwa. Tunaviomba vyombo ya ulinzi na usalama vihakikishe ulinzi
na usalama wa watu wote na mali zao siku ya uchaguzi na baada ya
uchaguzi.
CCM haitakubali hata kidogo ushindi wake kuhojiwa au kutiliwa shaka kwasababu tu ya vurugu zilizoanzishwa na watu wengine.
Siku ya Jumamosi, CCM itatangaza namba maalum za simu kwa Watanzania
wote ili siku kabla ya uchaguzi, siku ya uchaguzi na mara baada ya
uchaguzi, waweze kupiga simu au kutuma ujumbe pale watakapokuwa
wanabaini au kushuhudia vitendo vya kuvuruga amani na kuvuruga utaratibu
mzima wa uchaguzi.
Kupokea Matokeo
CCM imeweka utaratibu
wa kupokea matokeo kwa kutumia mawakala wake moja kwa moja vituoni na
kupitia mtandao wa Chama. CCM inategemea kuwa na matokeo ya uchaguzi
nchi nzima ifikapo saa nne usiku, siku ya uchaguzi, tarehe 25 Oktoba
2015.
Imetolewa na:
January Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni
22 Oktoba 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comment:
Post a Comment