Bukobawadau

AUAWA KISA LAKI 7

 Wakazi wa Kijiji cha Kindi Tarafa ya Kibosho Wilayani Moshi Mkoani
Kilimanjaro, wakiwa kwenye  mazishi ya marehemu Eugeni Mboro mfanyabiashara
wa mahindi aliyeuawa kwa kukatwa na shoka nyuma ya shingo yake na kuporwa
sh700,000.
Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Anthony wa Padua, Kijiji cha Kindi
Tarafa ya Kibosho Wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro, Padri John Senya,
akiongoza ibada ya mazishi ya marehemu Eugeni Mboro mfanyabiashara wa
mahindi aliyeuwa kwa kukatwa na shoka nyuma ya shingo yake na kuporwa
sh700,000.

Na Woinde Shizza,Moshi

WANANCHI wa Kijiji cha Kindi Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro
wamesema ili kukomesha mauaji ikiwemo tukio la kukatwa na shoka nyuma
ya shingo kwa Eugeni Mboro kwa sababu ya sh700,000 wauaji hao
wachukuliwe hatua.

Mkazi wa kijiji hicho Richard Massawe alisema jana chanzo cha kifo
hicho ni sh700,000 alizokuwa nazo Mboro baada ya kuuza mahindi yake
ndipo baadhi ya watu aliokuwa nao kupanga njama za kumuua na
kuzichukua fedha hizo.

“Tunaomba serikali ichukue hatua kwani Mboro alikuwa ni mjasiriamali
mdogo anayeibukia hapa Kindi na asiyekuwa na tatizo na mtu ila hao
kina Gasto na Kisimati walishikwa na tamaa ya kumuua ili wachukue
pesa,” alisema Massawe.

Mjomba wa marehemu Joseph Mwacha aliiomba serikali kuchukua hatua kwa
wahusika wote wa mauaji hayo kwani ndugu yao hakudhulumu kitu cha mtu
ila ni roho mbaya zilizosababisha kifo hicho na kumpora sh700,000
zake.

Hata hivyo, akiongoza ibada ya mazishi hayo, Paroko wa kanisa katoliki
parokia ya Anthony wa Padua, Padri John Senya, aliwataka wakazi wa eneo hilo kupiga vita matukio ya
uuaji kwa mtu asiye na hatia.

“Tunapaswa kubadiliwa jamani watu Kindi kwani itafikia siku mtu
ukisema umetoka Kindi watu watakuangalia mara mbili mbili hivyo
unasema umetoka Kibosho badala ya kutaja eneo hili tulipozaliwa,”
alisema Padri Senya.

Kwa upande wake, kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Ramadhan Mungi
alisema mwili wa Mboro ulikutwa kwenye shamba la Michael Makabili huku
akiwa na jeraha nyuma ya shingo lililotokana na kupigwa na kitu chenye
ncha kali.
Kamanda Mungi alisema pia marehemu aliibiwa fedha zake sh700,000 na
wanawashikilia watuhumiwa wawili kwa uchunguzi akiwemo Gasto Costa
(25) mkazi wa kijiji cha Kindi na mtu mwingine ambaye hakumtaja jina
lake.

“Huyu mtuhumiwa Gasto tulifanya upekuzi kwenye nyumba yake na kukuta
kuna shuka lenye damu na nguo za marehemu Mboro ila huyu mtuhumiwa
mwingine bado tunaendelea na uchunguzi juu yake,” alisem aKamanda
Mungi.

 
Next Post Previous Post
Bukobawadau