MWANGAZA, Sehemu ya 4:
Siku moja tukiwa darasa la saba, tulichukuliwa wanafunzi wachache
tuliokuwa tunafanya vizuri darasani kwa ajili ya kwenda kushindanishwa
na shule nyingine za mkoa wa Singida. Hii ilikuwa ni wiki kadhaa kabla
ya kufanya mtihani wa moko (mock). Mashindano hayo hayakuwa na lengo tu
la kutupima akili au kutuandaa na mtihani wa mwisho, bali pia yalikuwa
na lengo kubwa la kuwapatia baadhi ya
watoto wenye uwezo mkubwa darasani lakini wenye hali duni za uchumi wa
familia zao fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari. Mwaka huo ilitokea
bahati kuwa kulikuwa na wafadhili waliojitolea kufadhili masomo ya
sekondari kwa vijana ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa na
changamoto za ki uchumi katika familia zao, huku wakitilia mkazo wale tu
wanaofanya vizuri darasani.
Kwa bahati shule yetu ilikuwa moja
ya shule zilizopata hiyo fursa kuingia kwenye shindano, na watoto
watatu tulichukuliwa kushindanishwa na watoto wengine zaidi ya 100
kutoka kwenye shule mbalimbali za vijijini mkoani Singida. Walihitajika
washindi kumi tu kati ya vijana wote ambao walitakiwa kushinda kwa
wastani wa juu sana ili kupata fursa hiyo. Mimi na Mawazo na mwenzetu
mwingine mmoja tulichaguliwa.
Licha ya kuwa nilikuwa nafanya
vizuri sana darasani, lakini bado nilikuwa sijiamini vya kutosha
kushindanishwa na watoto mahiri na wengi kutoka kwenye shule mbalimbali.
Baba yake Mawazo alitafuta mwalimu maalumu kwa ajili yetu ili
kutusaidia na maandalizi. Nilipewa ruhusa nyumbani kuhamia nyumbani kwa
kina Mawazo kwa muda wa kama mwezi mmoja hivi kabla ya siku ya shindano.
Tulisoma usiku na mchana. Mwalimu alitusaidia kufanya na kurudia
maswali ambayo mara nyingi huulizwa kwenye mitihani ya mwisho.
Siku zilienda na hatimaye siku ya shindano ilifika. Tuliondoka na
mwalimu wetu mmoja shuleni, tukapanda basi kuelekea Singida mjini. Kwa
mara ya kwanza kwenye maisha yangu nilifika mjini, nikaona magari mengi,
nyumba kadhaa za bloko na umeme kila mahali. Pia nilishangaa kuona maji
yakitoka ndani, bombani kwenye chumba tulimolala. Mimi na Mawazo
tulilala chumba kimoja, na mwalimu alitafuta chumba kwajili ya mwenzetu
wa kike tuliyekuwa naye.
Asubuhi tulipelekwa sehemu ambapo
tulikutanishwa na wenzetu wote ambao tungefanya nao mtihani. Ilikuwa ni
shule ya bweni, na tulilala hapo siku mbili huku tukiendelea kujiandaa
na mtihani na baada ya hizo siku mbili, hatimaye siku ilifika. Tulitumia
siku nzima (moja) kufanya mitihani mitatu (Hisabati, Maarifa na Lugha).
Baada ya siku hiyo ndefu tulilala tena hapo shuleni siku hiyo na kesho
yake tukaanza safari kurejea nyumbani.
Siku kadhaa baada ya
matokeo ya mitihani ya moko kutoka, tuliitwa ofisini kwa mwalimu sote
watatu. Mwalimu alianza kwa kututia moyo kuwa sote tulifanya vizuri
katika lile shindano, na hasa mimi na Mawazo kwani wastani tuliopata ni
zaidi ya asilimia 90 kwa kila somo. Pia alisema kwamba hii inaonesha
hata kama hatujapata ile nafasi ya kuchaguliwa na kusomeshwa na
wafadhili, bado tuna fursa nzuri sana ya kuchaguliwa kusoma shule za
serikali baada ya mtihani wa taifa, kwani kwa ufaulu ule, ni lazima
tutachaguliwa kusoma shule nzuri za serikali. Maneno ya mwalimu
yalinifanya nilowe jasho. Nilijua ushindani uliokuwepo lakini nilikuwa
na matumaini makubwa sana ya kuchaguliwa. Ufadhili huo kwangu ungekuwa
na maana kubwa sana, kwani sasa si tu kuwa nisingehitaji tena kujilipia
ada, bali pia wafadhili waliahidi kutoa msaada wa kifedha kwa familia za
watoto husika. Nilikuwa tayari kichwani nina ndoto kubwa kuhusu huo
ufadhili na kiukweli, japo Mawazo ni rafiki yangu niliyempenda sana
sana, siku ile nilimuonea wivu mwalimu alipotuambia kuwa ni yeye pekeake
kati yetu sote watatu aliyefanikiwa kuingia kwenye kumi bora.
Tulioneshwa alama zetu, Mawazo alikuwa amenipita kwa alama moja tu. Ila
kwa ushindani uliokuwepo, tofauti hata ya nusu alama ilimaanisha ushindi
mkubwa. Nilimtazama Mawazo na kutoa tabasamu feki, na nilitegemea
angenionesha furaha japo kidogo, lakini badala yake Mawazo alitoa
machozi. Ni dhahiri hayakuwa machozi ya furaha, kwani nikiwa bado
najiuliza swali hilo, alimuuliza mwalimu,’Hakuna uwezekano wa kugawa
nafasi yako kwa mtu mwingine kama tukiongea nao?’ Mwalimu hakumjibu,
alimtoa yule msichana akabaki na sisi wawili. Alimjua Mawazo vizuri na
alijua alikuwa akimaanisha alichouliza. Hata mimi pia nilijua kuwa
alikua akimaanisha.
Tulikaa na mwalimu wa taaluma karibu saa
nzima akijaribu kumueleza Mawazo kuwa japo sikufanikiwa kupata ile
fursa, bado nina nafasi nzuri ya kuchaguliwa tena shule nzuri sana.
Mawazo aliumia sana kiasi cha kunifanya huzuni na wivu niliojisikia
vitoweke na badala yake niliona aibu. Baadaye, alipokubaliana, alianza
kunitia moyo. Japo nilimjua Mawazo kwa undani kabla, ila siku hiyo
niligundua kuwa nina rafiki mwenye huruma sana. Kwa kiasi kikubwa
alinifanya nikubaliane na matokeo. Niliporudi nyumbani mama pia
alinisaidia kukubali matokeo yale, kwani yapo alijua kiasi gani
nilitamani sana ile nafasi, lakini hakuonesha kuvunjwa moyo
nilipomwambia sikupita. Mama alimpa pongezi za dhati Mawazo
(alinisindikiza nyumbani siku hiyo), na pia alimshukuru jinsi
alivyonisaidia kukubali, kwani alijua hali yangu ingekuwa tofauti kama
tusingekuwa wote, (japo wakati huo nilikuwa bado sijamweleza yaliyojiri
ofisini kwa mwalimu wa taaluma).
Hatimaye mwaka 2001 tulihitimu
darasa la saba. Siku ya maafali ilikuwa siku yenye hisia mchanganyiko
kwangu. Kwa upande mmoja nilikuwa mwenye furaha, nilipewa zawadi ya kuwa
mwanafunzi mtulivu zaidi kwa mwaka wetu, pia nilipewa zawadi ya usafi
na nilipewa zawadi ya kuongoza katika somo la Maarifa kwa mtihani wa
moko. Mama yangu alikuja kunipokea kila nilipotoka kupokea zawadi, na
furaha aliyoionesha usoni mwake ilifanya nijione mwenye mafanikio
makubwa. Hakuwa na zawadi kubwa ya kunipa, lakini alinizawadia kitabu
cha wastani chenye jina KUISHI NDOTO YAKO. Yeye hakuona uthamani mkubwa
wa zawadi aliyonipa, lakini mpaka leo hii ninaandika hadithi ya maisha
yangu, sitaacha kamwe kukumbuka mchango mkubwa wa kile kitabu katika
mafanikio na changamoto zote nilizopitia.
Hataivyo kwa upande
mwingine nilikuwa mtu mwenye huzuni. Kumaliza shule ya msingi
ilimaanisha mwanzo wa safari nyingine ya elimu ambayo mpaka sasa
nilikuwa sijajua itakuwaje. Kama mtoto wa kwanza, na kulingana na hali
halisi ya nyumbani kwetu, sikutegemea msaada wowote wa kiuchumi kutoka
kwa familia yetu. Nilijua lazima ningefaulu kwenda shule nzuri ya
serikali, na katika shule nilizochagua, mbili zilikua za mikoa mingine,
hivyo ilimaanisha kama ningepata kati ya hizo, ingenilazimu kwenda
kuishi mbali na nyumbani kwetu.
Niliwaza nitawezaje tena
kujisomesha elimu ya Sekondari, pia niliwaza jinsi gani nitaanza maisha
ya kuishi mbali na familia yetu ambayo kwa namna moja ama nyingine
nilionekana kama mtu anayetegemewa. Nikiwa katikati ya mawazo mengi juu
ya maisha yanayofuata, alinipiga begani Mawazo ambaye alikuwa ametoka
kuchukua sahani ya chakula. Nilimuangalia na kutabasamu japo sikuonesha
furaha kama aliyokuwa nayo yeye. Ghafula nilipata huzuni zaidi
nilipogundua kuwa miezi michache ijayo urafiki wetu utatenganishwa na
umbali wa shule tutakazokuwa tunasoma. Nilijihisi kumkosa tayari Mawazo
japo nilikuwa hata sijajua ni lini tutatengana.
Sherehe
iliendelea, tulikunywa na kula chakula kilichoandaliwa kwa michango
kidogo tuliyokuwa tumeichanga, wazazi walifurahi, wanafunzi tulipiga
picha za pamoja, na hapo ndipo nilipogundua kuwa vijana wenzangu wengi
sana tuliosoma nao walinipenda na kuniheshimu sana, kwani wengi waliomba
kupiga picha na mimi, wengi walinitambulisha kwa wazazi wao wakisema
‘huyu ndio Nathani’, na pia kuna ambao hata sikuwachukulia kama
marafiki, waliniaga kwa kunikumbatia na wengine kunishukuru. Mara
nyingine unaweza ukawa unafanya vitu ambavyo unaona ni vya kawaida tu
kwa watu, kumbe vina maana kubwa sana. Nikiwa shule, na hasa nilipoanza
kufanya vizuri darasani, mara nyingi wanafunzi wenzangu waliniomba tukae
pamoja na kufanya maswali ya nyuma (past papers) pamoja, hasa wakati wa
mitihani. Utayari wangu wa kuwasaidia wenzangu wakati mwingine hata
kuharibu ratiba zangu za kujisomea au kurudi nyumbani, sikujua kuwa
ulinijengea urafiki kwa wenzangu wengi sana. Daima sikupenda kukataa
kutoa msaada hasa wa masomo kwani nilitamani kila ninayeweza kumsaidia
afanye vizuri kwenye masomo yake, nimsaidie afanye hivyo. Kulingana na
hotuba ya mwalimu wa taaluma, mwaka huo walitegemea kupata matokeo bora
zaidi kwa vijana kwani lilikuwa darasa lenye ushirikiano mkubwa na
motisha ya juu ya kusoma. Mwalimu pia alitaja baadhi ya wanafunzi ambao
walionesha juhudi kubwa sana za kuwasaidia wenzao, nikiwemo mimi, na
nilipotajwa wanafunzi wenzangu walipiga makofi mengi mno.
Wakati wa chakula tulikuwa pamoja na wazazi wa Mawazo, na hapo mama
alipata fursa ya kuwashukuru tena wazazi wake kwa jinsi ambavyo kijana
wao amenisaidia kwa kiasi kikubwa kufanya vizuri kwenye masomo yangu.
Mama yangu alikuwa ni mtu mwenye utajiri wa shukurani. Mara zote
alinifundisha kuwa mtu anaponifanyia kitu, neno la shukurani lina
thamani kuliko pesa na mali. Nilitumia wakati huo kujichangamsha na
kujisahaulisha shida zangu kwani nilijua hii ni siku ya mwisho ya
kufurahi kwa pamoja na wanafunzi wenzangu, hivyo nilikula kwa haraka na
kisha kwenda kuendelea na stori za hapa na pale, huku tukikumbushana
miaka ya nyuma, tukicheka na kufurahi.
Katika mambo ambayo
shule yetu imefanikiwa sana, ni uandaaji wa mahafali. Tofauti na shule
nyingi za vijijini, shule ya msingi Kilimahewa inasifika kwa kuandaa
mahafali yaliyochangamka sana, na japo uandaaji wake si wa gharama
kubwa, walimu walizitumia siku hizo kuwa siku nzuri za kuwakutanisha
wazazi na wanafunzi, na pia kutenga muda wa kutosha kufahamiana,
kuzungumza na kucheka. Siku hiyo nadhani ilikuwa na furaha zaidi kwani
kulingana na mshikamano mkubwa tuliokuwa nao wanafunzi, wazazi wetu
wengi walifahamiana na hivyo hawakuwa wapweke.
ITAENDELEA...
SHARE na LIKE Ukurasa wetu wa Bukobawadau Entertainment Media
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comment:
Post a Comment